Matampi amfunika Diarra ‘clean sheet’ Ligi Kuu

MKALI wa kulinda nyavu ‘clean sheet’ katika Ligi Kuu Bara msimu huu ameibuka kuwa kipa Ley Matampi wa Coastal Union baada ya kumaliza akiwa nazo 15 ukiwa ni msimu wake wa kwanza katika mashindano hayo.

Matampi aliyempiku Djigui Diarra wa Yanga ambaye huu ni msimu wake wa tatu, tayari ameshinda tuzo hiyo misimu miwili mfululizo akimshusha Aishi Manula wa Simba aliyewahi kujiwekea utawala wake kwa misimu sita mfululizo tangu akiwa Azam FC kabla ya kuhamia Simba 2017. 

Matampi huu ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na Coastal Union akitokea Klabu ya Jeunesse Sportive Groupe Bazan ya Congo.

Matampi amecheza mechi 24 kati ya 30 za ligi, sawa na dakika 2160 na kumzidi kipa wa Yanga, ambaye amecheza mechi 21 kati ya 30 akifikisha jumla ya dakika 1846 na jumla ya clean sheet 14.

Makipa wote hao wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu zao kwa msimu huu kwani Diarra ameiwezesha Yanga kutetea taji lake la ligi, huku Matampi akiiwezesha Coastal Union kumaliza nafasi ya nne na kufuzu Kombe la Shirikisho msimu ujao.

Coastal imepata nafasi hiyo baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo na kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza.

Baada ya hapo ndipo michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.

Kitendo cha Matampi kuweka rekodi hiyo kilikuwa gumzo kwenye vijiwe vya gahawa jana Jijini Tanga huku wapinzani wao African Sports wakitaka kuona watafanya nini msimu ujao kimataifa.

Related Posts