T: Utata akidaiwa kupelekwa akiwa hai mochwari

Moshi. Ni tukio la kutatanisha. Hii ni baada ya   mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Saimon Macha kudaiwa kwamba jana akiwa hospitalini KCMC alikokuwa amelazwa, alikufa na baadaye akabainika kuwa bado yuko hai akiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Baada ya taarifa hizo kuvuma na baadhi ya wanafamilia kuzipata, waliamua kuweka msiba nyumbani kwake Mtaa wa Kwa Sawaya, Kata ya Majengo, Wilayani Moshi mjini.

Hata hivyo, leo asubuhi waomboleza waliokuwapo nyumbani hapo waliambiwa mzee huyo hajafariki dunia kama ilivyoelezwa jana.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumanne Mei 28, 2024, shuhuda aliyelala msibani hapo amesema; “Tulipata taarifa za msiba wa mzee Macha jana mchana kutoka kwa ndugu, basi tukafunga maturubai hapa na msiba ukaanzishwa, lakini leo asubuhi zikaja taarifa kuwa mzee Tesha hajafa yuko hai ila amelazwa ICU.”

Anasema baada ya taarifa hizo, waombolezaji waliokuwa wamejikusanya nyumbani hapo kwa mshangao mkubwa ikabidi waondoke na maturubai yaliyofungwa yakafunguliwa.

Hata hivyo, zikaja taarifa za pili kuwa amefariki dunia kweli. Anasema taarifa za kuwa mzee Macha amefariki dunia leo, wamepewa na ndugu ambao walienda hospitali kumuona leo mchana na kukuta amefariki dunia kweli.

“Taarifa ya pili ya Mzee Macha kufa, tumepewa joni hii na ndugu ambao walienda KCMC kumuona ndiyo wamekuta amekufa kweli, tumebaki tunashangaa, ndiyo tunaendelea sasa na msiba tena,” amesema shuhuda huyo.

Mmoja wa wanafamilia ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa bado familia haijamteua msemaji amesema kilichotokea ni mkanganyiko wa taarifa tu.

“Maneno yamekuwa mengi sana, hata hivyo sisi kama familia hatuna malalamiko yoyote dhidi ya hospitali na wala hatumlaumu mtu,” amesema kwa kifupi.

Ulipotafutwa uongozi wa Hospitali ya KCMC uzungumzie tukio hilo, Ofisa Uhusiano, Gabriel Chisseo,  amesema kilichotokea ni mkanganyiko wa taarifa kwa ndugu hao na kwamba, mgonjwa alipofikishwa hospitalini hapo ubongo wake ulikuwa tayari umeshakufa.

“Huyu mgonjwa aliletwa kwetu ubongo wake ukiwa umekufa, kitaalamu ubongo ukifa moyo unaweza ukawa unapiga na hata huyo mtu mnaweza kukaa naye hata miaka 10, anakuwa ni nusu mfu.”

“Yaani ubongo ukiwa umesimama ni Mungu mwenyewe ndiye anabaki kuwa mwamuzi, watalamu hufikia mahala wanakuwa hawana uwezo tena wa kuuamsha ubongo huo, kwa hiyo alikuja tayari ubongo umelala,” amesema.

Kuhusu mgonjwa kupelekwa mochari akiwa hai, Chisseo amesema si kweli.

“Wala hakupelekwa mochuari kama taarifa zilivyovuma, pale wodini hata mke wake hakuwepo, na baada ya mgonjwa kugundulika ubongo umesimama alipelekwa moja kwa moja ICU, na si chumba cha kuhifadhia maiti,” amesema.

Anasema hata ndugu wa marehemu walielezwa kuhusiana na tatizo la ubongo kusimama kufanya kazi.

“Na ili kuondoa mashine ya kupumulia ni lazima wataalamu wawili wakutane wasaini na ndugu wasaini, kisha wanaelezwa kwamba wanaizima mashine, lakini jana wakati utaratibu huo unataka kufanyika, ndugu hawakuwepo kwa hiyo haikufanyika,” amesema Chisseo.

“Sasa asubuhi kukatokea sintofahamu huko kwenye familia kwamba sisi tumesema mgonjwa ni mzima, kitu ambacho sio kweli kama hospitali hili ni jambo la kitaalamu sana,”amesema Chisseo.

Hata hivyo amesema mkanganyiko wa mawasiliano baina ya ndugu wenyewe ndiyo uliozua hayo yote.

“Hapa naweza kusema ni mawasiliano kati ya msimamo wa kitabibu na jamii ilivyopokea taarifa hiyo, ndiyo yakazushwa haya yaliyozuka,” amesema na kuongeza;

“Na sio kwamba mgonjwa alipelekwa mochwari halafu akarudishwa, ili maiti iende mochwari ni lazima ipimwe kwanza na daktari athibitishe kwamba kweli amefariki ndiyo anapelekwa mochwari, hapelekwi kienyeji,” amesema.

Related Posts