Dar es Salaam. Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka kampuni 22 wakiambatana na maofisa wa serikali kutoka nchini Ufaransa, wapo nchini kutafuta fursa mpya za biashara katika sekta nishati, miundombinu, utalii, usafirishaji na uendelezaji wa miji.
Ujio wa wafanyabiashara hao, unakoleza uhusiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Ufaransa ambao sasa unalenga kuchochea ushirikiano kwenye ubunifu, Pia kunufaisha pande zote mbili kupitia kubadilishana utaalamu na uwekezaji katika sekta muhimu.
Takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, zinaonyesha biashara kati ya Tanzania na Ufaransa imekuwa na kufikia Sh95.5 bilioni mwaka 2022 kutoka Sh27.8 bilioni ya mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 27,2024 , kiongozi wa ujumbe wa wafanyabiashara hao, Gerard Wolf amesema wapo tayari kufanya uwekezaji nchini haraka iwezekanavyo.
“Tunatafuta fursa na kupata washirika sahihi kwenye soko hasa kupitia sekta tofauti, tuna matarajio makubwa sana na Tanzania kwa sababu ina rasilimali nyingi sana,”amesema.
Kwa mujibu wa Wolf,Tanzania ina fursa nyingi katika sekta ya kilimo ambayo manufaa yake yatachochewa zaidi na usafiri wa Reli ya Kisasa (SGR) na Reli ya zamani (MGR) kwa ajili ya kusafirisha bidhaa kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kuipeleka nje ya nchi.
“Ikiwa tutashirikiana na Tanzania katika SGR, tutasafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda, ingawa MGR ina fursa kwetu kwa sababu bomba la Hoima kutoka Uganda hadi Tanzania tutaagiza mafuta ghafi Tanzania na kuyauza kwa nchi nyingine duniani,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Haijaoui amesema Ufaransa inazingatia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukuza maendeleo endelevu kupitia mfululizo wa mazungumzo na mikutano ya kimkakati kwa kukutanisha wafanyabishara kutoka Ufaransa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Ubalozi unashiriki mikutano mikakati na kampuni za Tanzania, mawaziri, na taasisi za Serikali huko Zanzibar. Lengo ni kuimarisha biashara na uwekezaji kwa kutoa lango la kimataifa la biashara kutoka nchi zote mbili kufanikiwa.
“Kupitia mikutano yetu tuna fursa ya kushirikiana na wawakilishi kutoka taasisi kubwa za kifedha kama vile Benki ya Dunia, Shirika la Kimataifa la Fedha la ushirikiano nchini Ufaransa, Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (BEI)” amesema.
Kutokana na ujio wa wekezaji hao, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Ali Mwadini amesema ujio wa wageni nchini ni kutokana na kuvutiwa na fursa zilizopo.
“Tuna sababu nyingi za kufanya kazi pamoja kwa sababu eneo letu ni la kipekee, tunazungukwa na nchi nyingi ambazo tunashirikiana mipaka, hivyo ili kuvutia uwekezaji tumekuwa tukibadili sera zetu mara kwa mara,”amesema.
Kwa mujibu wa balozi huyo, sasa mazungumzo yanaendelea na kampuni kutoka Ufaransa kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa SGR. Akizungumzia mabadiliko katika uchumi, demografia na matumizi ya dijitali, balozi huyo amesema lengo la Serikali zote mbili ni kukuza uhuru wa makampuni na ujasiriamali.
Kwa lengo hilo, Balozi huyo amesema wanachukua hatua zinazoruhusu kampuni kunufaika na mazingira mazuri ya kisheria, kiuchumi, kodi, kijamii,