Wiki chache zilizopita bendera ya Tanzania ilipepea huko Nigeria kwa mchezaji wa Ligi Kuu Bara, Benjamin Tanimu kutoka Ihefu (Singida Black Stars) kuitwa na kucheza katika kikosi cha Super Eagles kilichokuwa na mastaa kama vile Nathan Tella (Bayer Leverkusen), Victor Osimhen (Napoli), Kelechi Iheanacho (Leicester City) na Alex Iwobi (Fulham FC).
Tanimu ambaye ni beki wa kati mwenye uwezo pia wa kucheza kulia alikuwa gumzo wakati akiingia katika vitabu vya historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Ligi Kuu Bara kuitwa na kucheza kwa dakika 78 katika mchezo wa kwanza kirafiki ambao Super Eagles iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ghana kabla ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Mali huku beki huyo wa Ihefu akiwa benchi.
Mitandao mbalimbali nchini Nigeria ilibidi kuandika safari ya soka ya mchezaji huyo ambaye aliwahi kuhusishwa kwenda Hispania kucheza soka la kulipwa kabla ya kutua Tanzania tena kujiunga na timu ambayo inaonekana kuwa katika daraja la kati tofauti na vigogo, Simba na Yanga maarufu Afrika.
Miongoni mwa mitandao hiyo ni pamoja na Daily Post Nigeria. Lakini Tanimu sio jina geni kwani baadhi ya wadau wa soka nchini humo wanamfahamu beki huyo kwa yale ambayo aliyafanya wakati akicheza soka la kulipwa akiwa na Bendel Insurance, alikokuwa akitajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora chipukizi huku akipachikwa jina la ‘The Wall’.
The Wall ni nini? Ni muundo wa wima, mara nyingi hutengenezwa kwa mawe au matofali, ambayo hugawanya au kuzunguka kitu, hivyo walimaanisha pindi awapo katika ukuta wa timu ni ngumu kupitika na timu yake huwa salama.
Mara baada ya kitasa hicho cha Mecky Maxime kurejea nchini, gazeti hili lilikiafuta na kufanya nacho mahojiano ambapo amefunguka mengi ikiwa ni pamoja na alivyopokea wito wa kulitumikia taifa lake, maisha ya kambini na mastaa wakubwa ambao wanacheza soka la kulipwa Ulaya.
“Kiukweli kabisa ilikuwa ni sapraizi kwangu, sikutegemea kama nitaitwa timu ya taifa lakini namshukuru Mungu kwa ukuu wake kwangu, na viongozi wa shirikisho la soka Nigeria pamoja banchi la ufundi kwa kuona kuwa nastahili heshima hiyo ya kulitumikia taifa langu,” anasema beki huyo.
“Nakumbuka nilikuta nimetumiwa ujumbe mwingi na marafiki zangu wa Nigeria. Nilistuka kwa sababu haikuwa kawaida kwa wakati mmoja. Nilipofungua mmoja baada ya mwingine nilihisi ni kama nipo ndotoni.”
Baada ya kuitwa, Tanimu alipongezwa na wachezaji wenzake wa Ihefu na mara moja aliitikia wito na kwenda Nigeria kwa ajili ya kambi ya siku chache kujiandaa na michezo hiyo ya kirafiki kwa mujibu wa kalenda ya Fifa.
“Nilifurahia sana maisha ya kuwa kambini na wachezaji wakubwa ambao wanacheza soka la kulipwa Ulaya, ulikuwa wakati mzuri kwangu. Nilijifunza mambo mengi kutoka kwa wachezaji wazoefu nikajikuta nina kiu zaidi ya kutamani na mimi kucheza soka la kulipwa Ulaya jambo ambalo naamini kuna siku nitalifanikisha tu,” anasema Tanimu.
Wachezaji ambao waliripoti kambini na Tanimu alipata nafasi ya kufanya nao mazoezi pamoja na kucheza katika michezo hiyo miwili ya kirafiki ambayo yote alicheza makipa ni Stanley Nwabali (Chippa United, Afrika Kusini); Francis Uzoho (AC Omonia, Cyprus); Ojo Olorunleke (Enyimba FC, Nigeria).
Mabeki: Gabriel Osho (Luton FC, England); Chidozie Awaziem (Boavista FC, Ureno); Bright Osayi-Samuel (Fenerbahce FC, Uturuki); Tyronne Ebuehi (Empoli FC, Italia); Bruno Onyemaechi (Boavista FC, Ureno); Kenneth Omeruo (Kasimpasa FC, Uturuki); Oluwasemilogo Ajayi (West Bromwich Albion, England); Calvin Bassey (Fulham FC, England); Jamilu Collins (Cardiff City, Wales).
Viungo: Wilfred Ndidi (Leicester City, England); Raphael Onyedika (Club Brugge, Ubelgiji); Alhassan Yusuf (Royal Antwerp FC, Ubelgiji); Frank Onyeka (Brentford FC, England); Alex Iwobi (Fulham FC, England) Fisayo Dele-Bashiru (Hatayspor, Uturuki).
Washambuliaji: Nathan Tella (Bayer Leverkusen, Ujerumani); Victor Osimhen (Napoli, Italia); Kelechi Iheanacho (Leicester City, England); Sadiq Umar (Real Sociedad, Hispania); Moses Simon (FC Nantes, Ufaransa); Ademola Lookman (Atalanta FC, Italy); Taiwo Awoniyi (Nottingham Forest, England); Cyriel Dessers (Glasgow Rangers, Scotland)
“Ninafuraha na maisha ya Tanzania, najivunia kwamba nilifanya maamuzi sahihi ya kujiunga na Ihefu, mwanzoni nilikuwa nikipata tabu ya vyakula lakini kwa sasa nimevizoea, wachezaji wenzangu na benchi la ufundi wamenisaidia kuendana kwa haraka na maisha ya hapa,” anasema Tanimu.
“Ligi ya Tanzania ni ngumu kwa sababu inahitaji mchezaji ambaye yupo timamu kimwili kama haupo fiti inaweza kukuwia vigumu hasa kwa mchezaji ambaye anacheza nafasi kama yangu kumudu kuwadhibiti washambuliaji.”
Tanimu aliwahi kuhusishwa na klabu ya daraja la tano ya Uhispania, Lleida Esportu. Hata hivyo, klabu yake ya zamani, Bima ya Bendel, ilieleza kutopokea ofa yoyote hivyo aliendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho kabla ya kutua Ihefu.
Tanimu safari yake ya soka ilianza mwaka 2018 alipojiunga na Bendel Insurance, upande wa Ligi Kuu Nigeria (NPFL). Tangu wakati huo, amejidhihirisha kuwa ni beki wa nguvu katika safu ya ulinzi ya timu hiyo, na hivyo kupata heshima ya mashabiki na wachezaji wenzake.
Kwa uchezaji wake dhabiti na kujitolea kwake bila kuyumbayumba, Tanimu alijiimarisha haraka kama mchezaji muhimu wa Bendel Insurance.
Mchango wake uliifanya Bendel Insurance kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) 2023 na hilo limemfanya kuacha alama isiyofutika kwenye klabu hiyo na alikuwa mmoja wa nyota ambao walioteuliwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa kikosi hicho.