Kikosi bora cha Mwanaspoti Ligi Kuu Bara 2023-24

PAZIA la msimu wa 2023/2024 wa Ligi Kuu Bara limehitimishwa rasmi baada ya vita ya vuta nikuvute huku kila timu ikivuna ilichopanda. Yanga imetwaa ubingwa wa tatu mfululizo, Azam imemaliza ya pili na kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku Simba iliyomaliza ya tatu na Coastal Union (4) zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika, ambalo hata hivyo CAF ilisema liko mbioni kufutwa.

Wakati ligi hiyo pendwa na namba 5 bora barani Afrika ikimalizika, wapo wachezaji waliofanya vizuri kutoka klabu mbalimbali na kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea kikosi chake bora cha nyota 11 kutokana na takwimu na ubora wao katika msimu uliomalizika.

DJIGUI DIARRA (YANGA)
Diarra ni moja ya makipa bora kwa sasa katika Ligi Kuu Bara. Ameshinda tuzo ya Glovu za Dhahabu ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo na msimu huu alikuwa anawania kwa mara ya tatu mfululizo akiwa na ‘clean sheets’ 14, kabla ya kupitwa katika mechi ya mwisho ya kufungia msimu na Ley Matampi wa Coastal Union mwenye ‘clean sheets’ 15. Diara hakucheza mechi ya mwisho ambayo Yanga ilishinda 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons, huku katika lango la timu ya wananchi akisimama Abutwaleeb Mshery.

Ukiachana na sifa hiyo, jambo jingine linalombeba Diarra ni kuipa ubingwa Yanga kwa mara tatu mfululizo huku akiwa ni kipa aliyeruhusu mabao machache zaidi (13) akishirikiana na mabeki, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kuunda ukuta imara.

KOUASSI YAO (YANGA)
Beki wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomari aliwahi kuandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram “Kazini kwangu kuna kazi” akimaanisha mtu aliyeletewa katika nafasi yake kikosini, Kouassi Yao sio wa mchezomchezo kabisa kutokana na ubora wake.

Yao ambaye huu ni msimu wake kwanza hapa nchini tangu ajiunge na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast amekuwa ni moja ya mabeki bora wa kulia ambapo hadi sasa amefunga bao moja la Ligi Kuu Bara huku akitoa asisti za mabao mengine saba. Ndiye beki aliyechangia mabao mengi zaidi msimu huu.

MOHAMMED HUSSEIN ‘TSHABALALA’ (SIMBA)
Licha ya Simba kutokuwa na msimu bora ila unapotaja wachezaji waliofanya vizuri msimu huu hutoacha kutaja jina la nyota wa kikosi hicho, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutokana na ubora anaoendelea kuuonyesha katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

Tshabalala ni mchezaji kiongozi ambaye amekuwa akitekeleza majukumu yake vizuri kuanzia kwenye kupeleka mashambulizi na wakati huohuo akirudi nyuma kuzuia na kuthibitisha hilo amehusika katika mabao sita ya kikosi hicho msimu huu.

DICKSON JOB (YANGA)
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amekuwa akifanya mabadiliko mengi katika eneo la beki wa kati ila ubora wa Dickson Job msimu huu umetosha kuendelea kuaminiwa kikosini na kumfanya nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto kusugua benchini.

Job ni moja ya mabeki bora nchini ambao kama taifa tunapaswa kujivunia kutokana na ubora anaoendelea kuuonyesha huku kwa kiasi kikubwa akichangia kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kuruhusu pia mabao machache (14) kati ya timu 16 za ligi hiyo.

IBRAHIM HAMAD ‘BACCA’ (YANGA)
Tangu nyota huyo amesajiliwa na Yanga Januari 14, 2022 akitokea klabu ya KMKM ya Zanzibar hakuna ubishi kwamba amekuwa tegemeo katika eneo la beki wa kati wa timu hiyo licha ya kucheza na mabeki tofauti wakiwemo, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.

Kiwango chake bora ndicho kilichowafanya mabosi wa Yanga kumuongezea mkataba hadi 2027 wakiamini atakuwa chachu ya mafanikio haya yanayoendelea kuonekana ikiwemo kuisaidia timu hiyo kutetea taji lake la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara.

KHALID AUCHO (YANGA)
Hii ndio injini ya Yanga msimu huu na amekuwa katika kiwango bora kikosini humo licha ya kupambana na wachezaji nyota wa timu hiyo wakiwemo, Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao wote wamekuwa wasisubiri kwa Mganda huyo.

Kiwango bora alichonacho msimu huu licha ya kukosa michezo kadhaa ya timu hiyo kutokana na majeraha ikiwemo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ila hakuna shaka anaingia kikosi bora cha msimu huu.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’ (AZAM FC)
Huu ni msimu bora kwa nyota huyu aliyetua Azam FC msimu uliopita akitokea Yanga ambapo tangu amejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam amehusika katika jumla ya mabao 26 kati ya 63 yaliyofungwa na timu nzima.

Feisal amefunga mabao 19 ya Ligi Kuu Bara na kutoa asisti za mabao mengine saba na kuwa katika vita nzito na nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ambaye hatimaye alimbwaga staa huyo anayejulikana pia kama Zanzibar Finest katika siku ya mwisho na kushinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa msimu.

Msimu uliopita, Feisal alifunga mabao sita tu ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya aliyofunga akiwa na Azam FC jambo ambalo ni wazi linamfanya kuingia moja kwa moja katika kikosi cha wachezaji 11 bora waliofanya vizuri kwa msimu huu.
 

MAROUF TCHAKEI (SINGIDA FG/ IHEFU)
Raia huyu wa Togo anaingia pia katika kikosi bora cha msimu huu kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha huku ukiwa ni msimu wa kwanza tu kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na klabu mbili tofauti akianzia Singida Fountain Gate kisha Ihefu.

Tchakei amefunga mabao 10 ya Ligi Kuu Bara huku akikosa michezo kadhaa ya msimu huu kutokana na majeraha.

Nyota huyu kwa mara ya kwanza alitua nchini na kujiunga na kikosi cha Singida Fountain Gate akitokea AS Vita Club ya DR Congo na baada ya kuonyesha kiwango bora mabosi wa Ihefu walivutiwa na huduma yake na kumsajili katika dirisha dogo la Januari mwaka huu.

KIPRE JUNIOR (AZAM FC)
Unapotaja miongoni mwa mawinga bora msimu huu hutoacha kutaja jina la nyota huyu raia wa Ivory Coast ambaye msimu huu tu amehusika katika jumla ya mabao 18 kati ya 63 ya Ligi Kuu Bara yaliyofungwa katika kikosi chote cha Azam FC.

Msimu huu amefunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara na kutoa asisti tisa na kumfanya kuonyesha kiwango bora kutokana na kuivuka idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita ambapo aliishia kufunga mawili tu msimu mzima.

WAZIRI JUNIOR (KMC)
Wakati mashabiki wa soka wakipiga kelele na kuuliza kwa nini vita ya ufungaji bora imehamia kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya kiungo tofauti na washambuliaji ila, msimu huu moja ya washambuliaji waliofanya vizuri zaidi ni Waziri Junior wa KMC.

Junior amekuwa na msimu bora akiwa ndiye mshambuliaji pekee miongoni mwa waliokuwa katika nafasi tatu za juu za waliowania tuzo ya mfungaji bora akiwa amefunga mabao 12 nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga (21) na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC mwenye 19.

Msimu bora kwake tofauti na sasa ni ule wa 2019-2020, akiichezea Mbao ya jijini Mwanza ambapo alifunga mabao 13 ya Ligi Kuu Bara.

STEPHANE AZIZ KI (YANGA)
Kiungo huyu nyota raia wa Burkina Faso alijiunga na Yanga Julai 15, 2022, akitokea klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambapo katika misimu miwili aliyoichezea timu hiyo ameonyesha kiwango bora cha kutamanisha miamba mikubwa barani Afrika.

Aziz Ki kwa sasa ndiye mfalme ndani ya Yanga. Ameshinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akihusika katika jumla ya mabao 29 kati ya 67 yaliyofungwa na timu nzima akiwa amefunga 21 na kutoa asisti nane katika mechi 27 alizocheza msimu huu ikiwa ni msimu bora zaidi kwake ndani ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.

Ni wazi nyota huyu anaingia katika kikosi bora cha msimu huu kutokana na jinsi namba zake zinavyombeba huku akiivunja rekodi aliyoiweka msimu uliopita ambao alifunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho cha Jangwani.

KOCHA: MIGUEL GAMONDI (YANGA)
Katika kikosi hicho cha wachezaji 11, kocha wake mkuu atakuwa ni Muargentina, Miguel Gamondi wa Yanga ambaye licha tu ya kuifundisha timu hiyo kwa msimu wa kwanza ameonyesha ni jinsi gani anaweza kuwatumia vizuri wachezaji wa kila aina.

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, mwaka jana akichukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco, mbali na kutetea tu ubingwa wa ligi ila amekiwezesha kikosi hicho kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga ilikuwa haijafuzu makundi la Ligi ya Mabingwa kwa miaka 25 kabla ya Master Gamondi kufanya yake.
 
MFUMO: (4-1-3-2)

Related Posts