Dar es Salaam. Licha ya dhamira ya Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika utoaji wa huduma ya vivuko kati ya Kigamboni na Magogoni, huenda mpango huo ukabaki kuwa ndoto isiyotimia kwa miaka kadhaa.
Hilo linatokana na mazingira ambayo si rafiki kwa sekta binafsi kutoa huduma katika eneo hilo.
Nia ya Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika utoaji huduma ya vivuko katika eneo hilo, iliwahi kuwekwa wazi na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 11, 2022. Katika hotuba yake alipozindua mradi wa maji Kigamboni, Rais Samia alionyesha nia ya kushirikiana na sekta binafsi, akilenga kuboresha huduma za vivuko.
“Tunatambua kuna kivuko kinafanyiwa matengenezo, kuna kivuko kipya kinajengwa. Tutaingia mkataba na sekta binafsi ili kuendesha huduma za vivuko,” alisema.
Kivuko kinachoendelea na matengenezo ni Mv Magogoni, kilichopo Kenya chini ya mkandarasi African Marine General Engineering Company Limited (AMGECO).
Kivuko hicho kinachotengenezwa kwa gharama ya Sh7.5 bilioni, kilipelekwa nchini humo Februari mwaka jana, kikitarajiwa kukamilika kwa miezi sita lakini hadi sasa hakijarejea.
Kauli ya Rais Samia ilitokana na hoja ya mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile aliyelalamikia huduma mbovu za vivuko katika eneo hilo.
Dk Ndugulile aliiomba Serikali iiruhusu sekta binafsi iwekeze katika utoaji wa huduma za vivuko ili kuongeza ufanisi.
“Tunaomba kama inawezekana kivuko hicho kikabidhiwe kwa sekta binafsi,” alisema.
Licha ya ombi na nia iliyopo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwepo mazingira ya kibiashara yasiyoshawishi sekta binafsi kuwekeza katika uendeshaji wa vivuko hivyo kwa sasa.
Utashi wa kisiasa unatajwa kuchangia ugumu wa sekta binafsi kuwekeza katika utoaji wa huduma za vivuko katika eneo la Kigamboni na Magogoni.
Hilo linathibitishwa na mmoja wa maofisa wa Serikali aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, akisema dhamira ipo, lakini hakuna mazingira wezeshi na shawishi.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, ndani ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), sekta binafsi inataka uhuru wa kupanga mambo yake ili ifanye biashara.
Kwa upande wa Serikali, alisema bado kuna mtazamo wa utoaji huduma na si hivyo tu, inang’ang’ana kupanga kiwango cha nauli kwa mwekezaji atakayetaka kuwekeza katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Serikali imetoa sharti kwa mwekezaji yeyote atakayewekeza katika eneo hilo, asitoze nauli zaidi ya Sh300 kwa kila abiria.
“Kiwango hicho cha nauli hakiwezi kurudisha gharama za uwekezaji, itakuwa hasara kwa mwekezaji, ndiyo maana wawekezaji wanaogopa,” amesema.
Amesema kuna haja ya Serikali kuona umuhimu wa kumwachia mwekezaji apange bei kulingana na gharama za uendeshaji, ili naye apate faida na Serikali ibaki kukusanya kodi zake.
“Angalau wangeruhusiwa kutoza Sh500 ingekuwa sawa, lakini kwa Sh200, hakuna mwekezaji aliye tayari kuja hapa,” amesema.
Hata hivyo, Mwananchi lina taarifa kuwa Temesa ilizifuata kampuni kadhaa, ikiwemo Azam Marine Ltd, kwa ajili ya kuomba ushirikiano nayo katika utoaji huduma, lakini kampuni hizo hazijaonyesha nia.
“Wamefuatwa mara kadhaa na wameahidi kuandaa pendekezo, lakini imeshapita miaka miwili tangu waahidi kila wakiulizwa wanajibu hawajakamilisha,” amesema mmoja wa maofisa wa Temesa.
Mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu wa Azam Marine Ltd aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa sababu ya itifaki za kikazi, amesema maandalizi ya pendekezo yanaendelea.
Pendekezo hilo, anasema ndilo litakaloamua mustakabali wa uwekezaji wa kampuni hiyo katika huduma za vivuko Kigamboni.
“Lakini kinachopaswa kujulikana ni kwamba sisi ni wafanyabiashara na tunaangalia masilahi ya kibiashara, siyo fumba na kufumbua,” amesema.
Mwananchi ilimtafuta mmoja wa viongozi wa moja ya kampuni binafsi inayojishughulisha na utoaji wa huduma za vivuko, ambaye amesema ni vigumu kuwekeza katika eneo hilo.
Ameeleza ingewezekana kuwekeza iwapo angepewa fursa ya kupanga nauli kwa kila abiria kupitia tathmini ya gharama za uendeshaji na si kupangiwa.
“Nauli za mabasi zinaongezeka kila siku kwa sababu ya kuongezeka kwa bei ya mafuta, huwezi kunipangia bei ya nauli ya kivuko wakati najua gharama ninazoingia katika uendeshaji wake.
“Kingine, sisi ni sekta binafsi, hatutoi huduma kama Serikali, mimi sina ruzuku, nitakachopata kama faida ndicho nitakitumia kugharimia uendeshaji,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa chombo kinachodhibiti usafiri wa majini ndicho kiwe msimamizi wa wadau wote wa usafirishaji majini na hata nauli kihakikishe zinatozwa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
Mbali na mwekezaji huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Ltd, Major Songoro amesema bado hana fikra ya kufanya uwekezaji huo.
Songoro amesema haoni kama atafaidika, akisisitiza watoa huduma wengine wa vivuko wanaweza kwenda kuwekeza.
“Sisi hilo halipo kwenye mipango yetu na hatuna nia hiyo kabisa, labda kama kuna watoa huduma binafsi wa vivuko (wengine) waende kuwekeza,” amesema.
Imebainika kuwa wawekezaji waliowahi kufuatwa mara kadhaa na Serikali kwa ajili ya kutakiwa kuwekeza, wamekuwa wakisitia kwa sababu za kutoona faida katika uwekezaji huo.
Mhadhiri wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Juma Kapaya amesema kuna umuhimu wa Serikali kuita wawekezaji wote kutoka sekta binafsi kwa ajili ya mazungumzo.
Ameeleza mazungumzo yalenge kujadili gharama za utoaji huduma katika eneo hilo, kisha wasikilizwe wawekezaji wangehitaji kutoza kiasi gani cha nauli ili kumudu uendeshaji.
“Kwa sababu mwekezaji anaangalia gharama, Serikali yenyewe ni kama mzazi anahudumia, lakini sekta binafsi inafanya biashara, kwa hiyo wakae meza moja wajadili hilo,” amesema.
Kwa mtazamo wa Kapaya, kuwepo kwa sekta binafsi katika eneo hilo, kutaboresha huduma za vivuko na kuwanufaisha wananchi
Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala amesema mpango wa kushirikiana na sekta binafsi upo na tayari mazungumzo na wawekezaji kadhaa, akiwemo Azam Marine Ltd yanaendelea.
Alipoulizwa kuhusu Serikali kulazimisha nauli ya kutoza, alisema kwa kuwa majadiliano na wawekezaji yanaendelea, utafika wakati kila kikwazo kitatatuliwa.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema tayari ameukutanisha Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Kampuni ya Azam Marine Ltd, kujadili namna bora ya kushirikiana ili kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni.
Kauli hiyo ya Bashungwa inakuja ikiwa ni siku ya tatu baada ya gazeti la Mwananchi kuchapisha mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu changamoto ya huduma za vivuko katika eneo la Magogoni-Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Msingi wa ripoti hiyo ni uchunguzi uliofanywa kwa takribani miezi mitatu na kuibua changamoto ya ubovu wa vivuko hivyo, unaosababishwa na kutofanyiwa matengenezo kwa wakati, kama inavyoelekezwa katika sheria ya Usalama wa Vyombo vya Majini (SOLAS) ya mwaka 1974.
Uchunguzi huo wa Mwananchi umekwenda mbali zaidi na kubainisha namna Temesa inavyopata hasara katika ukodishaji wa vivuko kutoka Azam Marine Ltd, ikilipa kwa kampuni hiyo binafsi Sh300 kwa kila abiria ilhali yenyewe inakusanya Sh200 kwa kila abiria.
Kauli ya kuikutanisha Temesa na Azam, Bashungwa ameitoa jana katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), huku akisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.
“Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutaweka machaguo kwa abiria ambao watakuwa na chaguo. Ukitaka kutumia kivuko cha Temesa sawa, au ukitaka cha Azam muda mchache kuvuka kwa sababu zile ni ndogo, siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja,” amesisitiza Bashungwa.