Karatu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, linamshikilia mhasibu mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu akidaiwa kutengeneza risiti bandia za kielektroniki (EFD) na kuzitumia kukusanya mapato kwa wafanyabiashara wa samaki katika eneo la Mang’ola.
Mbali na mhasibu huyo pia jeshi hilo linamtafuta mtumishi mwingine wa halmashauri hiyo kwa tuhuma hizo.
Kutokana na sababu hiyo, Halmashauri hiyo imesema kutafanyika uchunguzi katika vyanzo vyake vyote vya mapato ili kubaini kama kuna uchepushwaji wa makusanyo ya mapato.
Jana Mei 28, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Juma Hokororo, alisema Mei 23, walibaini watumishi hao wawili wametengeneza mfumo mwingine unaotoa risiti bandia za EFD zinazoonyesha zimetolewa na
Alidai kuwa katika eneo hilo gari moja hutozwa ushuru wa Sh1.5 milioni ila wao walikuwa wanatoza Sh1 milioni na kutoa risiti bandia hizo na fedha kutokuingia kwenye mfumo wa halmashauri.
“Hadi sasa hatua ambazo zimechukuliwa ni kushikiliwa kwa mhasibu huyo ambaye alikamatwa katika eneo hilo la Mang’ola, huku mtuhumiwa mwingine akikimbia.
“Askari wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa aliyekuwa Mang’ola pia ambaye ndiye alikuwa akizalisha risiti na licha ya kukimbia tulifanikiwa kukamata simu zake mbili, kompyuta mpakato moja na tumeona mawasiliano yaliyokuwa yanaendelea kati yao na kulikuwa na miamala inatoka kwa mtuhumiwa wa kwanza kwenda kwa huyo wa pili,”amesema na kuongeza;
“Hii ina athari kwa sababu Serikali inakosa mapato na wananchi wanakosa huduma mbalimbali, ufuatiliaji tumeachia polisi na wanaendelea kuhoji watu mbalimbali na mimi mwenyewe nimehojiwa. Leo tulikuwa na kikao, wakuu wa Idara nimewaeleza uchunguzi hauishii kwenye mapato ya samaki bali tutaenda kwenye vyanzo vyote vya mapato.”
Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka huu walikadiria kukusanya Sh300 milioni na mpaka sasa wamekusanya zaidi ya Sh600 milioni.
Hata hivyo, amesema wanaamini wangekusanya zaidi ya fedha hizo, lakini wataangalia kama kuna ubadhirifu katika vyanzo vingine ikiwemo kwenye ushuru wa mabango kwa sababu mtuhumiwa wa kwanza anasimamia pia eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema bado wanaendelea na kazi ya kufuatilia suala hilo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, mkurugenzi huyo alieleza kuwa waliweka mtego wa magari mawili ambayo baada ya kutoka na samaki walipowakamata waliwakuta na risiti mbili na kila moja ilikuwa ya gharama ya Sh1 milioni badala ya Sh1.5 milioni na fedha hizo hazijaingizwa kwenye mfumo wa halmashauri.
“Nilipewa taarifa nikaenda mwenyewe nilikesha Mang’ola tukavizia magari, mawili tuliweka mtego walikatiwa risiti feki na fedha hazikuingia kwenye mfumo wa halmashauri,” alisema.