KIPA wa Coastal Union ya Tanga, Ley Matampi amefunguka siri ya mafanikio yake ya kuongoza kwa clean sheet, akimtaja kipa wa Yanga Djigui Diarra ambaye amempiku msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkongomani huyo amesema jambo pekee lililomfanya kuwa bora ni ushirikiano wa makocha na wachezaji wenzake.
Matampi ambaye ameweka rekodi ya kucheza mechi 24 na kutoruhusu bao katika mechi 15, amesema anajivunia sana mafanikio yake hasa kuiwezesha Coastal Union kufuzu ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Amesema hii sio mara yake ya kwanza kuwa kinara wa ‘clean sheets’ katika maisha yake ya soka kwani alishawahi kufanya ubabe huo pia wakati anacheza nchini kwao DR Congo.
“Nimefurahi kulinda hadhi yangu kwa kuongoza kwa clean sheets, lakini kubwa kwangu ni namna ambavyo nimeweza kuisaidia timu yangu kupata mafanikio. Kikosi changu sasa kinakwenda kushiriki michuano ya kimataifa, jambo ambalo sikulitegemea sana ila juhudi za timu kwa ujumla ndio zimekamilisha malengo yetu,” alisema Matampi.
Aliongeza kuwa; “Ligi ya Tanzania sio, rahisi ina wachezaji bora na ina ushindani mkubwa, hivyo kwa mara ya kwanza nilivyocheza nikagundua nahitajika niwe na utulivu mkubwa ili kufanikisha malengo.”
AMTAJA DIARRA
Aidha, Matampi aliweka wazi kuwa kati ya makipa bora aliowahi kukutana nao ni Diarra akasema ukiachana na kushindana naye lakini anaheshimu uwezo wake.
“Ni kipa bora wa kisasa na anastahili hata kuongoza tena kwani ni kipa mwenye sifa zote zinazohitajika na wako wachache wenye kipaji kama chake.”
Mkongomani huyo huu ni msimu wake wa kwanza kuchezea Coastal Union akitokea Jeunesse Sportive Groupe Bazano ya Congo.