Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Serikali itaingia mkataba wa msaada na mkopo nafuu wa Dola za Marekani 2.5 bilioni sawa na Sh5.2 trilioni kutoka Serikali ya Korea Kusini.
Waziri Makamba amesema fedha hizo zitaelekezwa katika uboreshaji wa sekta ya elimu, afya na miundombinu, akisema Korea imekuwa na mchango mkubwa katika maeneo hayo.
Amesema makubaliano hayo ni mapya ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Serikali ya Tanzania na Korea na mkataba mkubwa kati ya saba itakayoingia Juni 2, 2024 kati ya Taifa hili na nchi hiyo.
Waziri Makamba amesema hayo leo Mei 29, 2024 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea Kusini itakayoanza kesho Mei 30 hadi Juni 6, 2024 ambapo Serikali ya Tanzania na Korea zitasaini mikataba saba ya kuimarisha ushirikiano.
“Ziara hii itakuwa na sehemu kuu mbili, mosi ni ziara rasmi kati ya Tanzania na Korea, pili Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi za Afrika na Korea.
“Kuanzia Juni Mosi hadi , 2024 Rais Samia atakuwa na ziara kati ya Tanzania na Korea kwa mwaliko rasmi na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake yatakayojikita katika ushirikiano baina ya mataifa haya mawili yatakayofanyika Ikulu ya Korea,” amesema Makamba.
Amefafanua kuwa Tanzania na Korea zina ushirikiano wa miaka 32 katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu na baada ya mazungumzo ya viongozi wakuu hao mikataba ya ushirikiano saba itasainiwa.
Mikataba hiyo ni pamoja na hati ya makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi na Miamba na Madini ya Korea, ushirikiano utakaojikita katika utafiti, uchoraji ramani, rasilimali na shughuli za maabara.
Mingine ni ushirikiano katika maendeleo ya uchumi wa buluu, kutambua vyeti ya mabaharia, tamko la pamoja la uanzishwaji wa majadiliano kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi.
“Nchi zetu hizi zimeamua kuingia katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na maeneo mengi, sasa kabla ya kuanza majadiliano tutasaini tamko la pamoja la kisiasa la kuanza mchakato huo,” amesema Waziri Makamba.
Waziri Makamba amesema kutakuwa na hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Viwanda na Biashara ya Korea kuhusu ushirikiano wa kuchambua na kufanya utafiti wa madini mkakati.
Pia, kutasainiwa mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na Shirika la Ukarabati wa Migodi na Rasilimali za Madini la Korea.
Waziri Makamba amesema ziara hiyo itaanzisha ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Korea cha Usafiri wa Anga na Tanzania ili kuboresha soko la usafiri wa anga na uendeshwaji wa biashara ya sekta hiyo. Pia uendeshaji na uratibu wa viwanja vya ndege, utalaamu, utafiti na huduma.
“Wenzetu Korea wamepiga hatua katika sekta hii, tutakuwa na ushirikiano katika hili,” amesema Makamba.
Mbali na hilo, Waziri Makamba amesema kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye menejimenti ya usafiri wa anga nchi ikiwemo miundombinu, ukarabati na ujenzi wa viwanja, udhibiti na ufufuaji wa usafiri wa anga.
Chuo Kikuu cha Masuala ya Anga cha Korea kitamtunuku Rais Samia shahada ya heshima ya udaktari katika menejimenti ya usafiri wa anga.
Hatua hiyo itawezesha Rais Samia kutunikiwa tuzo tano zilizotolewa katika vyuo vikuu vya Tanzania, Zanzibar, India na Uturuki alizofanya ziara ya kikazi kwa nyakati tofauti.
Katika hatua nyingine, Rais Samia atashiriki mkutano wa wakuu wa nchi kati ya Korea na Afrika utakaoanza Juni 3 hadi 4 na mkuu huyo wa nchi atapata nafasi ya kuhutubia na kuzungumza katika jopo moja kati ya manne yatakayokuwapo.
“Kutakuwa na majopo manne yanayozungumzia ajira, nishati, miundombinu, kilimo, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
“Pia mkutano huu wa utakuwa kipande kingine cha biashara yatakayokutanisha kampuni kubwa za Korea zitakazokutana na viongozi ili kuangalia fursa za kuwekeza Afrika. Rais Samia atashiriki mkutano na kufanya mazungumzo mahsusi na kampuni hizo kuhusu uwekezaji nchini,” amesema.
Waziri Makamba amesisitiza mkutano huo ni muhimu wa kufungua fursa ya ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi za bara la Afrika na Korea iliyochagua mataifa saba ya kipaumbele kuhudhuria shughuli hiyo.