Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania, imesema kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanaharakati Alphonce Lusako dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akipinga malipo ya Sh7.6 bilioni haina mashiko, hivyo imeitupa.
Kupitia kesi namba 16 ya 2023, Lusako alikuwa akipinga malipo ya fedha hizo zilizotumwa kwa sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kujenga jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, akisema malipo hayo yalikiuka sheria.
Lusako alimfungulia kesi CAG kama mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa pili katika kesi hiyo ambayo ilitolewa hukumu Mei 27, 2024 na Jaji Deo Nangela wa Mahakama Kuu Dodoma.
Katika msingi wa kesi hiyo, Machi 30, 2023, CAG aliwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ripoti ya ukaguzi kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2021 ambayo pamoja na mambo mengine, ilionyesha matumizi hayo ya Sh7.697 bilioni.
Mwanaharakati huyo kwa mujibu wa hukumu hiyo, alisema matumizi ya fedha hizo zilizotolewa kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwa kukiuka sheria za nchi, lakini CAG na AG katika majibu yao wakasema, malipo hayo yalifanywa kwa mujibu wa bajeti.
Katika maombi yake, mwanaharakati huyo aliiomba Mahakama itamke kuwa kutolewa kwa fedha hizo kwenda sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza kulikiuka ibara za 136(1)(a), 136(1)(b), 137(6), 143(2)(a) na (b) ya Katiba ya Tanzania.
Aliomba Mahakama itoe tamko utoaji wa fedha hizo kwenda kwa sekretarieti hiyo ulikiuka ibara ya 47(1(a) ya Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014.
Pia, aliiomba Mahakama itamke kuwa kitendo cha AG kushindwa kumshauri Rais na Baraza la Mawaziri kwa usahihi kuhusu Katiba na Sheria, alikiuka ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliiomba Mahakama imwagize CAG ashauri kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliohusika na uvunjifu wa Katiba na sheria katika utoaji wa fedha hizo na imwagize CAG kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa amri hiyo ya mahakama.
Jaji Nangela alisema Wakili John Seka alirejea hoja ya mteja wake akiiomba Mahakama kukosoa namna na staili ambayo fedha hizo zilitolewa kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwenda kwa Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza.
Mwanaharakati huyo alijenga hoja kuwa, kulingana na ripoti ya CAG, fedha hizo hazikuwa zimetengwa katika bajeti wala kuombwa na sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ikizingatiwa kuwa ujenzi huo haukuwa umepangwa katika mwaka huo wa fedha.
Kwa mujibu wa hoja zake, CAG katika ripoti kwa Rais alieleza kutolewa kwa fedha hizo kutekeleza shughuli ambayo haikuwa kwenye bajeti, kunaathiri utekelezaji wa shughuli zilizopangwa na kutoa mwanya wa ubadhirifu.
Kwa maoni ya mwanaharakati huyo, suala hilo halikupaswa kuishia tu kwa CAG kutoa mapendekezo yake kwa Serikali Kuu badala yake, hatua kali zilipaswa kuchukuliwa kwa waliohusika kwani vitendo vyao vilikiuka Katiba ya nchi.
Alieleza kuwa Serikali Kuu na CAG hawakuzingatia utaratibu uliowekwa na Katiba wakati wa kupeleka fedha hizo kwa sekretarieti ya Mwanza hivyo kuiomba mahakama iyakubali maombi yake na amri ambazo zilioombwa.
CAG na AG kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a alisema hoja ya msingi katika kesi hiyo imeegemea katika matumizi mabaya ya fedha za umma lakini ikasisitiza utoaji wa fedha hizo haukukiuka Katiba wala sheria.
Hoja za kuamuliwa na Mahakama
Katika kesi hiyo, Mahakama ilibainisha hoja nne ili kuamua mabishano ya mleta maombi na wajibu maombi (CAG na AG) na moja ni kama ripoti ya ukaguzi ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2021 inafaa kuaminiwa.
Hoja ya pili ni kama kutolewa kwa fedha hizo kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwenda sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ulifuata kanuni za utoaji fedha kama zilivyoainishwa na vifungu mbalimbali vya Katiba vilivyotajwa na mdai.
Hoja ya tatu ni kama vitendo vya CAG kuhusiana na utoaji wa fedha hizo ulizingatia kifungu cha 47(1)(a) cha sheria ya bajeti, na nne kama kitendo cha kutomshauri vizuri Rais na Baraza la Mawaziri kulikiuka ibara ya 59(3) ya Katiba.
Jaji alisema kwa kuzingatia ofisi ya CAG ni ya kikatiba chini ya ibara ya 143(1), hakuna mtu atatilia shaka uhalisia wa ripoti na zaidi maudhui ya ripoti zake, hivyo hoja ya kwanza inajibiwa kuwa zinaaminika.
Kulingana na Jaji, aliamua kujibu hoja ya pili na ya tatu kwa pamoja akisema kwa mtazamo wake, CAG ana majukumu mawili, moja ikiwa ni kufanya ukaguzi na ya pili fedha zote zinazotolewa zinafuata Katiba ya nchi.
Jaji alisema swali la msingi la kujiuliza ni je vifungu vya Katiba alivyovianisha mdai vilikiukwa kama inavyodaiwa, akisema fedha zinazohifadhiwa na kutunzwa katika mfuko mkuu wa Serikali ni fedha za umma.
“Kwa msingi huo, Katiba imeweka masharti magumu kuhusu matumizi ya fedha hizo. Hakuna fedha zinaweza kutolewa labda tu kwa ajili ya matumizi yaliyoidhinishwa na Katiba ya nchi au sheria,” alisema Jaji.
“Kama matumizi hayo yameidhinishwa na sheria ya fedha au kwa sheria iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo ibara ya 136(1(a) na (b) ya Katiba inaeleza hivyo,” alisema.
“Vile vile ibara ya 136(3) ya Katiba inasema hakuna fedha itakayotolewa katika mfuko mkuu wa Serikali kwa ajili ya matumizi ya Serikali isipokuwa matumizi hayo yamepata idhini kutoka kwa CAG na lazima zitolewe kwa mujibu wa sheria.”
Jaji alisema kwa maoni yake anaona anachotoa CAG ni ‘Grant of Credit’ kwa mlipaji mkuu wa Serikali na lazima awe amepokea maombi kutoka kwa mlipaji mkuu, akasema haoni kosa katika hatua hizo.
Akirejea hoja za mdai, Jaji alisema ni msingi wa kisheria kuwa hakuna matumizi yanaweza kufanywa nje ya bajeti ambayo yameidhinishwa na sheria ya fedha ambayo hutungwa na Bunge baada ya kumaliza kupitisha bajeti.
“Katika shauri tulilonalo, hakuna ubishi kuwa, wakati CAG anatekeleza jukumu lake la ukaguzi kwa mwaka ulioishia Juni 2021, kwanza alitoa kile alichokibaini na hitimisho kuwa ujenzi wa jengo hilo haukuwa umejumuishwa kwenye bajeti.”
Jaji akasema katika hukumu yake kulingana na ripoti ya CAG, sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ilipokea Sh8.33 bilioni kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba, sehemu ya fedha hizo yaani Sh7.697 bilioni ndizo zilitoka Hazina.
“Zaidi ya hilo na kulingana na ripoti ya CAG, fedha hizo alizipa alama kuwa ni ‘unbudgeted funds’ au fedha ambazo hazikuwepo kwenye bajeti na kupendekeza kuwa kwa siku zijazo, Serikali ihakikishe inazingatia sheria ya bajeti,” alisema Jaji.
Alisema hakuna ubishi kuwa katika ripoti hiyo, CAG alinukuliwa akisema kutolewa kwa fedha kutekeleza miradi ambayo haikuwa katika bajeti kunaathiri utekelezaji wa miradi iliyoko kwenye bajeti na inatoa mwanya wa ubadhirifu.
Hata hivyo, Jaji alisema kwa kuwa maoni hayo yalitolewa na CAG na kuibua hoja, lakini ukisoma wasilisho la mdai kuhusu fedha hizo, yeye anashawishika kuwa fedha hizo awali zilikuwa zimepangwa kwa ajili ya matumizi husika.