Mabadiliko tabianchi yanavyowakimbiza jamii ya wafugaji

Arusha/Manyara. “Tulikuwa na ng’ombe watano na mbuzi 10. Ukame ulipozidi ng’ombe wote walikufa na kubakiwa na mbuzi watano pekee.”
Ni kauli ya Helena Leiyan, mama wa watoto wanne aliyeachwa na mume wake tangu mwaka 2019.

Helena, anayeishi katika Kijiji cha Terrat wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara anasema hali ya ukame ilipozidi, mume wake aliuza mbuzi waliosalia kisha kutoweka.
“Maisha yalizidi kuwa magumu baada ya baba kuondoka.

Awali alikuwa akifanya kazi za vibarua kwenye mashamba ya watu na shughuli nyingine, lakini haikutosha. Ilibidi aondoke bila kuaga. Hatujui kama yuko hai au amekufa, hajawahi kuwasiliana nasi,” anasema Helena, ambaye watoto wake wana umri wa miaka tisa, 11, 16, na 17.

Helena Leiyan mama wa watoto wanne aliyetelekezwa na mume wake tangu 2019, baada ya maisha kuwa magumu. Kushoto ni mwandishi wa gazeti hili Halili Letea. Picha na Ombeni Daniel

Helena anasema mume wake, Leiyan Nelukendo alipoondoka aliendelea kulea wanawe kwa shida hadi mwaka 2023 hali ilipozidi kuwa ngumu zaidi, akatafuta msaada kwa ndugu wa mume wake.

“Tulikuwa wake wawili, mwenzangu na watoto wake wawili walirudi kwao baada ya mume kuondoka. Nilikaa hadi mwaka jana nilipokuja hapa, walinikaribisha,” anasema.
Helena na watoto wake wanaishi kwa kaka wa mume wake, Isaya Nelukendo.
Watoto wawili walikuwa shuleni wakati huo, ingawa ilikuwa Jumamosi kwa sababu wanajiandaa kwa mtihani wa Taifa.

“Tunashukuru kuwa na mahali pa kuishi, lakini nahitaji kuwa na shamba au mifugo. Mume wangu hakuacha, lakini kama nikipata nitampunguzia mzigo huyu baba,” anaeleza.

Isaya anasema, “Hatujui alipo (Leiyan), niliwahi kusikia yuko Mirerani. Hii ni familia yake (Helena na watoto wake), kwa hivyo ni yangu pia, na nina wajibu wa kuwasaidia.”

Akizungumzia kuhusu kumpatia Helena ardhi au mifugo, Isaya anasema angefanya hivyo kama angekuwa navyo, lakini alichonacho hakitoshi.

“Tutakula tulicho nacho Mungu atakavyojalia. Pia watakaa hapa hadi watakapoweza kujitegemea,” amesema.

Kuondoka kwa wanaume na kuacha familia zao si jambo geni katika maeneo haya. Nilikutana na mama wa makamo aliyejitambulisha kwa jina la Naitapuaki Lukas anayeishi katika Kijiji cha Oloswaki.

Naitapuaki, anayeishi na mume wake mzee anasema: “Tulikuwa na watoto wawili, walipokua waliondoka na hatujui walipo.”

Anaamini wanawe wapo mjini akisema, “Sijui kama wako Mirerani au Dar es Salaam. Hawajawasiliana nasi kabisa tangu walipoondoka.”

Naitapuaki na wanawake wengine sita wanaeleza si kijiji chao pekee, wanaume wameondoka kutoka vijiji jirani pia.
Kuna wanaume ambao licha ya ugumu wa maisha, wameendelea kujihusisha na shughuli nyingine.

Nilikutana na Noah Lukas katika Kijiji cha Oloswaki, anayejishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na ufugaji.

“Ufugaji umekuwa mgumu kutokana na kupungua ardhi ya malisho. Ingawa nina mbuzi wachache, lengo langu kuu ni kilimo. Tunashukuru Serikali kuleta maji karibu. Nauza mboga na naweza kusaidia familia yangu,” anasema.

Katika maeneo mengine ya mijini kama vile Dar es Salaam na Zanzibar, kuna watu wa Kabila la Masai wanaojihusisha na biashara ndogondogo, kazi za ulinzi na wengine wanajihusisha na ususi wa nywele.

Katika eneo la Mwenge, Dar es Salaam, nilikutana na Naranda Saling’o, anayefanya biashara ndogo ndogo za kuuza pochi, mikanda, vikatakucha na vitambaa katika maeneo ya jirani.
Licha ya kuishi Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka saba tangu alipoondoka nyumbani kwao Engarenaibor wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, anakiri kupoteza mawasiliano na ndugu zake.

“Sina simu,” anasema kijana huyo, anayedai maisha yake hayajabadilika sana kwa sababu fedha anazopata hazitoshi kumudu maisha yake, ikiwemo kupata mahali pa kulala.
“Usiku ukiingia, ninalala popote. Hata nguo hii ndiyo pekee niliyonayo, naifua na kusubiri ikauke nivae.

Naoga mtoni na maeneo ninayoona kuwa ni safi,” anasema Naranda.
Akiwa na umri wa miaka 25, hana mipango ya kuanzisha familia kwa sababu hana mahali pa kumweka mwenza. Anasema hawezi kumudu mahitaji yake ya kila siku.

“Sina pesa, familia inahitaji pesa. Na ataishi wapi?” anahoji.
Kijana mwingine Joseph Nendukai, mlinzi wa moja ya majengo katika mitaa ya Sinza anasema alikuja Dar es Salaam mwaka 2017 kutafuta riziki.

“Nilikuwa na ng’ombe 20 na mbuzi 50, walikufa wakaacha ndama watatu tu na mbuzi 10. Hakukuwa na malisho na wengine walipata magonjwa,” anasema kijana huyo kutoka Kijiji cha Nanja, wilayani Monduli.

Nendukai anasema alimuacha mke na watoto wake wawili nyumbani chini ya uangalizi wa kaka yake. Anaeleza huwasiliana nao na huwasaidia.
Anasema huwa akiwatembelea angalau mara moja kwa mwaka au baada ya miaka miwili.

“Jamii zetu zimeathiriwa na ukame, mifugo mingi ilikufa, ndiyo maana wengi wetu tuliondoka nyumbani kutafuta riziki ili kusaidia familia,” anasema.

 

Kukiwa na matukio ya baadhi ya wanaume kuondoka na kuacha familia zao, viongozi wanasema si kwa kiwango kikubwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Medukenya, anasema shughuli kuu za wakazi wa kijiji hicho ni kilimo na ufugaji.

Anasema kilimo kimekuwa kikienea zaidi kutokana na hali ngumu kwa ufugaji.
Anasema ukame umeathiri upatikanaji wa malisho na ustawi wa kaya nyingi.

“Kuna kesi nyingi tunazoshughulikia zinazohusu migogoro ya kifamilia inayosababishwa na ugumu wa maisha, watu wanahangaika kutafuta chakula na mifugo yao inakufa… wengine wameondoka na kuacha familia zao, ingawa si kwa kiwango kikubwa,” anasema.

Kiongozi wa kimila wa Kimasai, maarufu kama Laigwanani, Lesira Samburi anasema kuna kesi nyingi za watu kuondoka, hasa vijana.

“Watu wanakimbia kaya, hasa vijana. Unajua, maisha yamebadilika sana. Licha ya kuwapo kwa ukame siku hizi, mifumo ya maisha imeathiri vijana,” anasema.
Anaeleza kuwapo kwa vifaa vya mawasiliano na ukosefu wa maadili miongoni mwa vijana waliosoma ni sababu nyingine ya wao kuhama.
Samburi anasema vijana wengi waliosoma wanasahau walikotoka.

“Nawaambia vijana wasisahau walikotoka, hapa ni nyumbani kwao,” anasema.
Kuhusu wanaume kukimbia kaya na familia zao kutokana na ugumu wa maisha, Laigwanani huyo anasema:

“Kamati ya kijiji, kwa kushirikiana na jamaa wa karibu wa mume, inajadili suala hilo, na wale wasio na mifugo wanapewa kiasi kidogo ili waendelee kukaa na familia zao.”

 

Takwimu kutoka Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhamaji wa Ndani Duniani (IDMC) zilionyesha kufikia mwaka 2020 hali mbaya ya hewa ilisababisha zaidi ya watu milioni 24 kuhama makazi yao, wakati Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitabiri kufikia mwaka 2050, athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa mabadiliko makubwa hayatafanyika sasa yatasababisha mamilioni ya watu zaidi kuhama.

Wakati huohuo, mtandao wa Groundswell unakadiria zaidi ya watu milioni 216 watahama, watatu kati ya watano watatoka Bara la Afrika.

Mhadhiri katika Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Pius Yanda, anasema katika maeneo yanayoathiriwa na ukame, mafuriko au ukosefu wa malisho ya mifugo, watu wanalazimika kuhama kwenda mengine.

Profesa Yanda anasisitiza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ambayo watu wanahama yawe na miundombinu ya kuwasaidia, hivyo kuzuia migogoro katika maeneo wanakohamia.

“Miradi kama vile BBT – Jenga Kesho iliyo Bora inatoa msaada mkubwa, lakini inahitaji kupanuliwa ili kufikia maeneo mengi zaidi. Miundombinu ya umwagiliaji na utafiti wa kusaidia kilimo endelevu ni muhimu,” anasema.

Dk Wessam El Beih kutoka Kituo cha IDMC alisema baadhi ya sera zinazoweza kuwalinda watu walio katika hatari kubwa ya kuhamishwa ni kuimarisha mazingira ya watu kustahimili, hasa kwa jamii za vijijini.

Anasema hilo linaweza kufanikiwa kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za msingi, fursa za kujipatia kipato na hatua za kupunguza athari za majanga kama vile mafuriko na ukame.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Related Posts