Dar es salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania( TPA) Madeni Kipande (66) na wenzake watano wanaokabiliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Kipande na wenzake wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya dola za Marekani 1.85 milioni sawa na Sh4.2 bilioni.
Wakili wa Serikali, Winiwa Samson ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Mei 29, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Samson amesema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Mabutu, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika, aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama umekamilika.
Hakimu Mabutu alikubaliana na maelezo hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 27, 2024, itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Mbali na Kipande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2022 ni Peter Gawile (58) aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini, Casmily Lujegi (65) mkazi wa Mbezi Juu na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Andrew John.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara ya Sh4.2 bilioni.
Pia, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17,2015 washitakiwa kwa pamoja wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .
Shitaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020 eneo la TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni, hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya dola za Marekani 1.8 milioni ambazo ni sawa na Sh4.2 bilioni.