RIPOTI MAALUM: Yanga, Azam zaongoza kuathirika na viwanja vibovu

BAADA ya uchunguzi wa Mwanaspoti kubaini takribani viwanja 14 vinavyotumika na timu za Ligi Kuu havikidhi vigezo vya mwongozo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, athari tatu zimebainika kusababishwa na uduni huo.

Athari hizo ni majeraha kwa wachezaji, wachezaji kushindwa kufanyia kazi vyema ufundi na mbinu na pia kupunguza mapato kupitia fedha za viingilio zinazotolewa na mashabiki kwa ajili ya kutazama mechi viwanjani.

Imethibitika kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya ubora mdogo wa viwanja na majeraha kwa wachezaji hasa kwa kwa vile ambavyo havina maeneo mazuri ya kuchezea na vinavyokosa huduma kama vile meza ya masaji na huduma ya maji moto na baridi ambazo ni miongoni mwa vigezo vya msingi vya mwongozo wa CAF.

Daktari wa viungo wa Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa, Dodoma ambaye amewahi kuzitumikia kwa nyakati tofauti timu ya taifa ya soka la ufukweni na Singida Fountain Gate, Alfred Amede alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya eneo lisilokidhi la kucheza. “Ubora wa kiwanja una nafasi kubwa ya kuwalinda wachezaji na majeraha ingawa zipo sababu nyingine ambazo zinaweza kusababisha majeraha kwa mchezaji. Majeraha makubwa ambayo mchezaji anaweza kuyapata kutokana na uduni wa eneo la kuchezea ni yale ya enka na magoti.

“Pia anaweza kupata majeraha ya maeneo mengine ya mwili ikiwa ataanguka vibaya,” alisema Amede.

Kocha wa zamani wa mazoezi  ya viungo wa Simba, Mohammed Aymen Hbibi alisema viwanja kuwa na vitanda vya masaji na huduma ya maji moto na baridi ni ili kuwaepusha au kupunguza uwezekano wa kupata majeraha ya misuli na nyama za paja. “Mchezaji anapokuwa uwanjani anatumia nishati kubwa na viungo vingi vya mwili vinafanya kazi wakati mwingine zaidi ya uwezo wa kawaida wa kuhimili. Hivyo anapomaliza anapaswa kufanyiwa masaji ili kuweka sawa tishu za mwili na pia matumizi ya maji baridi yanasaidia kupoza mwili, kurudisha misuli katika hali yake na hata kuonyesha majeraha au maumivu na kuyapatia matibabu kwa haraka.

“Hizi zote ni huduma muhimu kwa mchezaji na asipozipata anajiweka katika hatari ya kupata majeraha ya misuli na nyama za paja ambayo hayatibiki ndani ya muda mfupi,” alisema Hbibi.

Awali uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti ulibaini kuwa ni viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex ndivyo vina huduma za vitanda vya masaji, maji moto na baridi.

Hali hiyo imechangia baadhi ya timu kama Simba, Yanga na Azam kutumia ndoo kubwa za plastiki za maji kuwekea mabarafu na maji baridi kwa ajili ya wachezaji kupooza misuli baada ya mechi zinapocheza nje ya viwanja vya Mkapa na Azam Complex.

Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti kutoka katika idara za tiba za klabu umebaini wachezaji 74 wa timu 16 zilizoshiriki Ligi Kuu msimu huu walipata majeraha yahusianayo na ubora duni wa eneo la ku-chezea kwenye viwanja kwa maana ya enka na goti, lakini pia ukosefu wa huduma bora ya masaji na kupoza misuli ambayo ni maumivu ya misuli na kuchanika nyama za mapaja.

Yanga na Azam FC ndizo timu ambazo zimeathirika zaidi ambapo idadi ya wachezaji waliokumbana na changamoto hizo kwa kila timu ni 10, zikifuatiwa na Simba, Ihefu na KMC ambazo kila moja imepata majeruhi wanane.

Namungo FC imekuwa na majeruhi sita, Tanzania Prisons watano, Mashujaa, Kagera Sugar, Singida Fountain Gate na Geita Gold kila moja wanne. Zilizokuwa na majeruhi watatu ni Tabora United na Mtibwa Sugar wakati Coastal Union mmoja.

Tukio la beki wa Simba, Henock Inonga kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro baada ya kuteleza na kuanguka pasipo kuchezewa rafu wakati anajaribu kumdhibiti mshambuliaji Samson Mbangula ni uthibitisho wa namna ubora duni wa eneo la kuchezea unavyoumiza wachezaji.

Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry aliliambia Mwanaspoti kuwa kuwakosa wachezaji wengi kutokana na majeraha kumelipa wigo mdogo benchi la ufundi katika upangaji wa kikosi.

“Sio kazi rahisi kucheza mechi nyingi mfululizo za ligi huku timu ikiwa na kikosi ambacho sio kipana kutokana na majeraha. Tumewakosa wachezaji wengi muhimu kutokana na majeraha jambo ambalo limechangia kutopata matokeo mazuri kwenye baadhi ya mechi.

“Lakini niwapongeze wachezaji wangu wengine kwa kazi nzuri ya kuipatia timu matokeo mazuri katika kipindi ambacho wenzao wanauguza majeraha hadi kutufanya tusitoke nje sana ya malengo tuliyojiwekea,” alisema Ferry.

ATHARI ZA KIMBINU      NA UFUNDI

Baadhi ya makocha na wachezaji wameliambia Mwanaspoti kuwa kuchezea viwanja visivyo na ubora kumekuwa kukilazimisha matumizi makubwa ya nguvu, huku wakishindwa kuonyesha ubora kiufundi na namna wanavyozifanyia kazi mbinu.

Timu nyingi zimefichua kuwa zinalazimika kutumia mbinu ya kucheza mipira ya juu badala ya kupiga pasi za chini mara kwa mara na pia wachezaji kutokaa sana na mpira na kuonyesha ufundi ili kuepuka kupotea kwa mipira na kunufaisha wapinzani wao.

Kocha wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah ‘Baresi’ aliliambia gazeti hili kuwa wanapocheza katika viwanja ambavyo havina eneo zuri la kuchezea hawawezi kutumia sana mbinu za kumiliki mpira kwa muda mrefu.

“Uwanja ukiwa sio mzuri sio rahisi kumiliki sana mpira na pia unaweza kusababisha majeraha kwa wachezaji hivyo mara nyingi tunapokutana na mazingira kama hayo huwa tunaamua kutokaa sana na mpira ili kuepuka majeraha na pia kuzuia kufanya makosa ambayo wapinzani wanaweza kutumia kutuadhibu,” alisema Baresi.

Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula alisema kuna uhusiano mkubwa baina ya kucheza vizuri na ubora wa uwanja. “Uwanja ukiwa mzuri, mchezaji unakuwa na ari kubwa ya kujiamini na unaweza kuamua kufanya lolote kwa vile utakusapoti lakini kama haupo vizuri muda mwingi utakuwa unacheza kwa tahadhari jambo ambalo linapunguza ufanisi wako uwanjani,” alisema Mbangula.

Beki wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ na Simba Queens, Fatuma Issah alisema hucheza kwa tahadhari kubwa wanapotumia viwanja ambavyo havina eneo zuri la kuchezea.

“Unapokuwa uwanjani, jambo la msingi ni kwanza kujilinda mwenyewe na pia kumlinda mwenzako kwani majeraha yamekuwa yakituathiri sana na ndio yamekuwa yakichangia kuturudisha nyuma,” alisema.

Mwezi uliopita, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alishangazwa na uamuzi wa kutumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kwa mchezo wao na JKT Tanzania akidai ulifanya timu yake kutoonyesha kiwango bora kutokana na hali ya maji ambayo yalituama katika baadhi ya maeneo.

“Kupata alama moja kwenye uwanja kama ule ni kitu kizuri tu kwangu. Unawezaje kushinda kwenye uwanja kama ule? Sijui ni uamuzi gani huu umefanyika.

“Huwezi kucheza mpira wa kuvutia kwenye Uwanja kama ule, tunaona soka la Tanzania linapiga hatua ni jambo zuri, lakini Uwanja kama huu unakwenda kuiweka wapi heshima hiyo, kwanini ilazimishwe mechi kuchezwa pale ingekuwa sawa hata kusogeza mechi mbele au kuhamishwa kupelekwa Uwanja mwingine,” alisema Gamondi.

Viwanja ambavyo vina viti vichache kwa ajili ya mashabiki kukaa wanapokwenda kutazama mechi, hapana shaka vinapoteza mapato milangoni kutokana na mashabiki wengi kusita kwenda kutazama mechi kwa kuhofia kujikuta wakilazimika kusimama muda mechi zinapoendelea.

Mara nyingi hutokea kwa mechi zinazohusu timu zenye mashabiki wengi hususan Yanga na Simba. Shabiki wa Yanga, Sharmila Salehe aliliambia gazeti hili kwamba hakwenda kutazama mechi katika viwanja vya Manungu Complex na Meja Jenerali Isamuhyo kutokana na majukwaa machache  ya kukaa mashabiki.

Bavon Choga aliyejitambulisha ni shabiki wa Simba alisema husafiri mara kwa mara mikoani kutazama timu yake lakini hukacha mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini kutokana na uwanja kutokuwa na mahali pa kukaa mashabiki.

Related Posts