Mshauri wa masuala ya usalama wa kitaifa wa Israel Tzachi Hanegbi amesema vita hivyo huenda vikadumu kwa miezi saba zaidi na kwamba mapigano yataendelea hadi pale watakaposambaratisha uwezo wa kijeshi na kiutawala wa kundi la Hamas na kundi dogo la wanamgambo wa Islamic Jihad.
Wapalestina huko Rafah wameripoti hii leo mapigano makali katika mji huo wa kusini uliokuwa kimbilio la mwisho kwa mamilioni ya Wapalestina waliokimbia mapigano katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.
Hadi sasa zaidi ya watu 36,000 wameuawa, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka zinazodhibitiwa na Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.
Soma pia: UNCEF yasema watoto 17,000 Gaza hawana ndugu wa karibu
Kambi za wakimbizi wa Kipalestina zimekuwa zikilengwa na mashambulizi ya Israel. Watu 45 waliuawa hivi majuzi huko Rafah, katika shambulio ambalo Israel ilisema lilikuwa kosa. James Elder, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF): amesema:
” Ni lugha gani inayofaa kuelezea uharibifu ambao haujawahi kushuhudiwa kwa nyumba na shule, katika eneo kubwa ambalo watoto wamekumbwa na kiwewe. Nadhani kwa hakika, swali linalopaswa kuulizwa ni je, ni makosa mangapi zaidi ambayo ulimwengu utavumilia? ”
Waziri wa Afya ya Wapalestina Majed Abu Ramadan, ameitolea wito Marekani kuishinikiza Israel kufungua kivuko cha mpakani cha Rafah, kilichokuwa kikitumiwa kuingiza misaada ya kibinadamu na vifaa vya matibabu, akisema kwa sasa hakuna dalili zozote kwamba Israel itafungua kivuko hicho hivi karibuni.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kufungwa kwa kivuko hicho kumeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kupeleka vifaa muhimu vya matibabu katika Ukanda wa Gaza, ambao umekuwa ukilengwa na mashambulizi makali ya Israel tangu Oktoba 7 pale Hamas ilipovamia kusini mwa Israel.
Harakati za kidiplomasia za mataifa ya kiarabu
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amekutana leo Jumatano mjini Madrid na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammad Mustafa na viongozi wengine kutoka nchi kadhaa za kiarabu ambazo ni Saudi Arabia, Qatar, Jordan, Uturuki pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu.
Viongozi hao wamekutana pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania José Manuel Albares. Akiwa mjini Madrid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi amesema:
” Mustakabali wa eneo la Mashariki ya Kati hauwezi na haupaswi kuwekwa hatarini na serikali yenye itikadi kali ya Israel inayoendelea na uchokozi wake wa wazi dhidi ya watu wa Palestina, kwa kutozingatia kabisa sheria za na matakwa ya jumuiya ya kimataifa na kukiuka maamuzi ya ICJ na maazimio ya baraza la usalama, pamoja na kukiuka maadili yetu ya pamoja ya kibinadamu.”
Hayo yanajiri baada ya Uhispania, Ireland na Norway kuitambua rasmi hapo jana Palestina kama taifa huru, hatua iliyopingwa vikali na Israel na ambayo haitakuwa na matokeo ya moja kwa moja katika vita vinavyoendelea huko Gaza, lakini inachukuliwa kama ushindi mkubwa kwa Wapalestina na inaweza kuhimiza mataifa mengine ya Magharibi kuiga mfano huo.
Som apia: UNRWA yasema Wapalestina milioni moja wakimbia Rafah
Rais Xi Jinping amesema China “imehuzunishwa mno na hali mbaya” inayoendelea huko Gaza. Wiki hii, China itakuwa mwenyeji wa mkutano na viongozi kadhaa wa Kiarabu mjini Beijing ambapo miongoni mwa mambo mengine watajadili kuhusu mahusiano kati ya China na nchi za Kiarabu lakini pia vita vinavyoendelea huko Gaza.
(Vyanzo: Mashirika)