KAMA ulidhani ishu ya udanganyifu wa umri ipo katika ngazi ya juu tu ya soka la Tanzania, basi ulikuwa unajidanganya, unaambiwa zaidi ya wachezaji 10 wamerudishwa nyumbani baada ya kubainika kuwa na umri mkubwa katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Chujio lililofanywa na wasimamizi wa michuano hiyo liliwanasa wachezaji walioonekana kuwa na umri wa zaidi ya miaka 14 inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa katika mashindano hayo makubwa kwa shule za msingi.
Licha ya kutowafanyia vipimo rasmi, mratibu wa UMITASHUMTA Mkoa wa Dar es Salaam, Harun Rashid amesema kupitia uzoefu wake anaweza kumtambua kijana wa miaka 14, hivyo wale wote ambao walikuwa wakiwashuku ni kweli walibainika kuwa na umri mkubwa na walirudishwa nyumbani.
“Tunataka kupata wachezaji wenye umri chini ya miaka 14 na sio wenye miaka 15 wala 16, hata kama bado wanasoma shule za msingi, tupo macho kusimamia hilo na naamini tutapata kile tunachokihitaji ili kuunda kikosi bora na imara kitachotuwakilisha vizuri kama mkoa,” alisema maratibu huyo.
Miongoni mwa wachezaji waliobainika kuwa na umri mkubwa (jina limehifadhiwa), alionekana kuwa mnyonge wakati akiondolewa kwenye moja ya michezo iliyokuwa ikichezwa kwenye viwanja vya Jitegemee.
Kuwa na misuli mingi mikononi huku sura yake ikionekana kukomaa ni kati ya vigezo ambavyo wasimamizi walimtilia shaka mchezaji huyo wakimtofautisha na wengine hadi kubainika kuna udanganyifu uliofanyika.
Kinondoni na Temeke ni kati ya wilaya zinazoonekana kutesa katika mashindano hayo huku wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kimkoa na kesho, Alhamisi mabingwa katika michezo mbalimbali watafahamika.