‘Energy drinks’ zaibua mjadala Baraza la Wawakilishi

Unguja. Sakata la madhara yanayosababishwa na vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) limeibukia katika Baraza la Wawakilishi, ikielezwa kuna utafiti unaonyesha kinywaji hicho ni hatari kwa afya ya binadamu.

Katika swali la msingi leo Mei 29, 2024, mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe ametaka kujua ni kwa kiwango gani Serikali inafahamu tatizo hilo akieleza kuna ripoti nyingi za kitabibu zinaonyesha kuwapo ongezeko la matatizo ya moyo yanayowapata watumiaji wa kinywaji hicho, pamoja na vifo vinavyoweza kuepukika.

Amesema hali hiyo inaigharimu na kuiongezea mzigo wa matibabu Serikali.

“Je, Serikali haioni kuwa sasa ni muda muafaka wa kupiga marufuku uzalishaji na utumiaji wa kinywaji hiki kwa lengo la kupunguza madhara kwa wananchi wake,” amehoji.

Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh amesema Serikali inalifahamu tatizo hilo na kupitia Shirika la Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) inaendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vinywaji hivyo kupitia vyombo vya habari.

Hata hivyo, amesema kinywaji hicho kinaruhusiwa kwa mujibu wa taratibu za nchi na hakina madhara iwapo kikitumiwa inavyotakiwa.

“Kinywaji hiki kina tabia ya kuuchangamsha mwili kutokana na kiambata kilichomo ndani yake, kama tunavyofahamu kitu chochote kikitumiwa zaidi kitaleta madhara,” amesema.

Naibu waziri huyo, amesema Mei, 2023 ZFDA ilifanya ukaguzi wa bidhaa ya energy drink sokoni.

Amesema asilimia 90 ya sampuli zilizochukuliwa katika soko la Zanzibar zilipita kwenye vipimo vya maabara kwa mujibu wa kiwango cha Zanzibar cha energy drink ZNS 60:2015 na TZS 838:2021.

Hivyo, ZFDA ilijiridhisha kuwa vinywaji hivyo havina tatizo, ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Hata hivyo, amesema tathimini ya ufuatiliaji wa matumizi ya bidhaa hizo ilionyesha watumiaji hawafuati maelekezo ya matumizi yake  kama yanavyoelekezwa kwenye vifungashio.

Amefafanua maelekezo hayo yanamtaka mnywaji asizidi mililita 500 kwa siku, asinywe mtoto, mjamzito na mama anayenyonyesha, pia kutokunywa muda mfupi kabla ya kulala.

Amesema Serikali inaendelea kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya bidhaa hiyo.

Related Posts