Afrika Kusini. Wakati wananchi wa Afrika Kusini wakipiga kura leo Mei 29, 2024, wafungwa katika gereza la Pollsmoor la Cape Town nao wamepiga kura kwa mujibu wa taarifa za serikali.
Chini ya Kifungu cha 24B cha Sheria ya Uchaguzi, wafungwa nchini Afrika Kusini wanaruhusiwa kupiga kura katika wilaya wanazoshikiliwa.
Gereza la Pollsmoor lina umuhimu wa kihistoria ya kuwashikilia wafungwa maarufu zaidi wa kisiasa chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi, akiwemo rais wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela, ambaye alishikiliwa hapo kabla ya kupelekwa gereza la Victor Verster na kuachiliwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi Walter Sisulu na Ahmed Kathrada pia walifungwa kwenye gereza hilo.
Chama cha EFF chalia rafu
Wakati huohuo, chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimelaani kutofanya kazi kwa mashine za orodha ya wapigakura katika vituo kadhaa vya kupigia kura
Katika taarifa yao iliyochapishwa katika mtandao wa X, EFF wamesema kushindwa kufanya kazi kwa mashine hiyo, kumesababisha kutumika kwa orodha ya wapigakura ya maandishi, hivyo wapiga kura kukata tamaa na kutoendelea na hatua hiyo ya kuchagua viongozi kidemokrasia.
“Jambo ambalo ni la kusikitisha, kwani linachukua muda na pia linahatarisha usahihi wa mfumo wa kupigia kura.
“Hii inahatarisha mchakato wetu wa kidemokrasia. EFF inatumaini kuna hitilafu halisi katika mfumo na huu sio ujanja wa IEC (Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini) kwa ajili ya siku ya pili ya upigaji kura isiyopangwa na kuwa na karatasi za kura kulala nyumbani kwa maofisa wanaosimamia uchaguzi,” kimeongeza.
“Chama kiliitaka tume ya uchaguzi kutatua tatizo hilo na kwa wafuasi kuwa na subira.”
Vituo vitano vya kupigia kura vyafungwa
Katika eneo la Eastern Cape baadhi ya vituo vya kupiga kura vilifungwa kutokana na maandamano.
Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa Times Live baadhi ya wapiga kura walizuiwa kupiga kura katika Jimbo la Eastern Cape waliandamana kutokana na ukosefu wa umeme na maji imeripoti.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa wa uchaguzi wa IEC eneo la Eastern Cape, Kayakazi Magudumana amesema vituo vitano vya kupigia kura vilifungwa kutokana na watu kuandamana kuhusu masuala ya utoaji wa huduma.