Dar es Salaam. Madaktari bingwa bobezi wanne kutoka Hospitali ya Apollo ya India wametua nchini kuweka kliniki katika Hospitali ya Kitengule iliyopo jijini hapa kushughulika na wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza.
Katika kliniki hiyo ya siku mbili kuanzia kesho Mei 30, 2024 utatolewa ushauri kwa wagonjwa wa moyo, ubongo na uti wa mgongo, mishipa ya fahamu, mfumo wa mkojo na wa uzazi kwa wanaume, saratani na aina mbalimbali za uvimbe ikiwamo tezi dume.
Sambamba na ushauri wataalamu hao watatoa mafunzo kwa madaktari wa Kitanzania, kushirikiana na wabia wa sekta ya afya pamoja na kutoa matibabu, lengo ikiwa ni kuwahudumia wagonjwa ambao kimsingi hawana uwezo wa kwenda India.
Aidha, imeelezwa kuwa hatua hiyo inakuja ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kutoa matibabu hayo pamoja na kuchochea sera ya tiba utalii hapa nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2024 jijini hapa wataalamu hao wamesema maradhi yasioambukiza yameendelea kuwa tishio ulimwenguni, hivyo ushirikiano baina ya wataalamu kati ya nchi na nchi kubadilishana ujuzi unahitajika kwa kiasi kikubwa.
Mmoja ya wataalamu hao, Profesa Venkatesh Tekur amesema wameamua kusafiri kutoka kwao India kuja nchini wakati ambapo matatizo kama ya moyo yakizidi kupaa.
Dk Anil Kamath mbobezi wa matibabu ya saratani amesema maradhi hayo yanazidi kushika kasi hata India, hivyo pia kuja kwao Tanzania ni sehemu ya kujifunza mengi zaidi kwa kushirikiana na Watanzania.
“Matatizo katika eneo hili yaliyopo Tanzania na India yanafanana hivyo kliniki hii itakuwa ni bora na muhimu kati yetu,” amesema Dk Kamath.
Hata hivyo, watashirikiana na madaktari wa Tanzania katika matibabu hayo sambamba na kuwapatia ujuzi wa kitaalamu zaidi ili watakapoondoka wautumie kama alivyobainisha Alex Kanyaitoju ambaye ni mwakilishi wa hospitali hiyo hapa Tanzania.
Kwa upande wa Meneja Mkuu wa Ushirikiano na Uangalizi kwa wagonjwa kutoka hospitali ya Apollo, Abu Bakker amesema uwepo wa kambi hiyo ya matibabu nchini ni fursa kwa Watanzania wanaotamani kwenda kutibiwa matibabu nchini India huku wakiwa hawana uwezo.