KIPIGO cha pili mfululizo kwa Simba kutoka kwa watani wao wa Yanga, kunawapa wakati mgumu mabosi wa Msimbazi kwani kwa sasa wana kazi ngumu ya kurejesha tabasamu usoni mwa wanasimba kutokana na hali ilivyokuwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa klabu hiyo baada ya dakika 90 za Kariakoo Dabi.
Simba ilipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Yanga katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni miezi michache tangu ilipofumuliwa mabao 5-1 na kupoteza mechi mbili kwa msimu mmoja mbele ya watani kama ilivyokuwa msimu wa 2015-2016 ilipochapwa 2-0 nje ndani na wababe hao wa Jangwani.
Mwanaspoti linakukusanyia matukio mbalimbali yaliyojiri katika dabi hiyo, likiwa la beki wa kati wa Simba, Hussein Kazi aliyekuwa na wakati mgumu wa kumwaga machozi baada ya kipyenga cha mwamuzi Ahmed Arajiga kupulizwa kuashiria pambano limeisha na Simba kulala mbele ya Yanga.
Kitendo cha Kazi kulia kama mtoto uwanjani, kiliwafanya mastaa wa Yanga na Simba akiwamo Khalid Aucho kushindwa kujizuia na kujikuta wakitumia muda mrefu kumbembeleza kama njia ya kumfariji kwani ni yeye aliyekuwa hoi zaidi kuliko wanasimba wengine walioumizwa na pambano hilo la Ligi Kuu Bara.
Wakati wachezaji wa Yanga wakiondoka kwa kicheko, baadhi ya mastaa wa Simba kama Hussein Kazi,alijikuta akiangua kilio kulichofanya mastaa wengine wa upande wa pili (Yanga) waingiwe na huruma na kuanza kumbembeleza.
Beki wa Simba, Hussein Kazi alijikuta katika wakati mgumu katika dakika yake ya kwanza tu tangu alipoinngia uwanjani kuchukua nafasi ya Henock Inonga aliyeumia. Kazi alipoteza mpira mbele ya Stephane Aziz KI, ambaye alipounasa tu haraka akaingia ndani ya boksi la Simba kwa kasi, sasa wakati Kazi akijaribu kuurudisha mpira katika himaya yake akajikuta akimchezea madhambi Aziz Ki na kusababisha penalti ambayo staa huyo wa Burkina Faso aliifunga mwenyewe katika dakika ya 20.
Mastaa wa Yanga waliokwenda kumnyamazisha Kazi alikuwa ni kiungo Khalid Aucho na beki Bakari Mwamnyeto, sambamba na Stephane Aziz KI aliyemponza kusababisha penalti iliyozalisha bao la kwanza la Yanga lililofungwa na kinara huyo wa mabao wa Yanga na katika Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa nayo 15.
Mbali na nyota wa Yanga kumuonea huruma Kazi, pia mastaa wenzake wa kikosi hicho cha Msimbazi walionekana kumfariji kwa kumtuliza aache kulia akiwamo nahodha wa timu hiyo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Fondoh Che Malone, Freddy Michael na kocha msaidizi, Seleman Matola.
Kama hujagundua kitu ni kwamba katika pambano la juzi, makocha wakuu wa timu hizo, Abdelhak Benchikha na Miguel Gamondi wote walipigilia mavazi meusi.
Dakika chache kabla ya mchezo huo kuanza makocha wa timu zote walitoka katika vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa wamevaa nguo nyeusi.
Alianza kutoka Benchikha akiwa amevaa tisheti nyeusi, suruali ya track nyeusi, raba nyeusi na saa nyeusi (smartwatch) ambapo muda mfupi baadae Gamondi wa Yanga naye alitoka na mtoko huohuo wa nguo nyeusi kama mwenzake japo yeye chini akitupia raba nyeupe na mkononi ni saa smart nyeusi.
Dakika chache kabla ya mchezo huo kuanza kiungo wa timu ya Simba, Fabrice Ngoma alionekana akimuelekeza jambo golikipa wake Ayoub Lakred ambapo hata wakati mpinzani wao alipopata penalti alienda kumtia moyo kabla ya kupigwa kwa penati hiyo iliyozaa goli la kwanza kwa Yanga.
Kiungo huyo ambaye aliyezichezea klabu kama za Raja Casablanca, AS Vita na Al Hilal alionekana akitoa hamasa kwa wachezaji wenzake, kuhakikisha hawatoki mchezoni.
Katika pambano la juzi makocha wa timu zote walilazimika kufanya mabadiliko bila kupenda ya mabeki kutoka DR Congo, ilianza kwa Yanga kwa kuumia kwa Joyce Lomalisa kisha muda mchache baadaye beki wa kati wa Simba, Inonga naye aliumua na kutoka.
Baada ya kutibiwa na madaktari wa timu zote mbili ilionekana kuwa hawataweza kuendelea na mchezo. Nafasi ya Lomalisa aliingia Nickson Kibabage aliyepo Jangwani kwa mkopo kutoka Singida FG na dakika tano baadaye ikawa ni zamu ya Inonga aliyetolewa na kumpisha Hussein Kazi aliyesajiliwa na Simba akitokea Geita Gold ambao walimudu vyema nafasi hizo na kucheza kwa dakika zote zilizosalia hadi pambano lililopisha.
Usimkatie mtu tamaa huenda ni msemo mzuri kutumia hapa ambapo washambuliaji hao wakiwa wamesajiliwa katika dirisha dogo wamefunga katika dabi yao ya kwanza tangu wasajiliwe huku mashabiki wa timu zote mbili walikuwa wakilalamikia viongozi wao kuwa wachezaji hao ni wazito ingawa tayari kabla ya mechi hii walikuwa wamefunga.
Alianza Guede kuzitikisa nyavu za Simba baada ya kuutegua mtego wa kuotea na kukontroo kiufundi pasi ya kiwango cha juu kutoka kwa Aucho kabla ya kumpiga chenga kipa Lakred na kuipatia timu yake bao la pili huku katika kipindi cha pili Simba walifanya mabadiliko yaliyowaingiza ndani Fredy Michael na Luis Miquissone ambapo dakika chache baadaye Fredy aliifungia Sim ba bao akimlambisha sakafu Ibrahim Bacca, mchezo ukimalizika kwa mabao 2-1.
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alionekana akielekeza mastaa wake, huku mkononi akiwa ameshika faili mara baada ya kurejea kutoka mapumziko, huku akionekana akilisoma na kuwaelekeza nini anataka wafanye ingawa pia sura yake ilikuwa ikionyesha kutofurahia mchezo huo na mara kwa mara alionekana akiwa anaangalia faili na kushauriana na wasaidizi wake nini kifanyike kubadili matokeo ya mchezo huo.
Ikumbukwe ni mechi ya tano mfululizo Simba inatoka bila ya ushindi ikiwa ni siku chache tangu iondolewe kwenye Ligi ya Mabingwa kwa kufungwa nje ndani na Al Ahly pia Mashujaa iliwatoa kuwania Kombe la Shirikisho (ASFC) na kutoka sare na timu ya Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi.
Wakati wa mchezo huo ukiendelea mastaa mbalimbali wa timu zote waliokuwa benchini walionekana wakiinuka katika mabenchi yao na kuanza kuwaelekeza wenzao waliokuwa uwanjani nini wafanye ili kuweza kushinda mchezo huo.
Mastaa hao ni Luis Miquissone na Inonga aliyetoka baada ya kuumia na Mzamiru Yassin walionekana wakielekeza wenzao, kwa upande wa timu ya Yanga ni Yao Kouassi, Lomalisa pamoja na Clement Mzize walioelekeza kwa kunyoosha vidole ili wenzao waweze kuelewa kwa uharaka.
Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo mashabiki wa Simba walionekana wakiwa wamekata tamaa baada ya timu hiyo kufungwa 2-1 Wengi waliondoka wakilaumu na wengine walichelewa kutoka wakikaa kinyonge sana majukwaani.
Licha ya kuwa nje ya nchi katika majukumu ya uenyekiti wa shirikisho la klabu Afrika, rais wa klabu ya Yanga, Hersi Said aliuwahi mchezo huo.
Mara baada ya mchezo Rais huyo alifika katika benchi la timu yake na kuwakumbatia baadhi ya mastaa waliokuwa wamekaa hapo ikiwa ni ishara ya kufurahishwa na matokeo hayo yaliyoiacha Yanga ikifikisha pointi 58 kileleni, huku Simba ikisaliwa na alama zake 46 japo wanatofautiana mchezo mmoja.
Yanga imecheza mechi 22, wakati Simba ikiwa na 21, huku Azam FC iliyozitenganisha timu hizo ikiwa nafasi ya pili na pointi 51 imecheza mechi 23 na zote zipo kwenye mbio za ubingwa kwa msimu huu.