Huduma ya maji yarejeshwa Hanang, wakazi 26,900 kunufaika

Hanang. Baada ya uharibifu wa miundombinu ya maji Wilaya ya Hanang mkoani Manyara uliosababishwa na maporomoko ya udongo, Shirika la WaterAid Tanzania limekarabati chanzo cha maji cha Nangwa kinachotegemewa na wananchi 26,900.

Desemba 3, 2023, yalitokea mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyoambatana na mawe, magogo na maji kutoka Mlima Hanang na kusababisha vifo vya watu 89 na wengine 137 wakijeruhiwa, maelfu wakipoteza makazi yao.

Baada ya maafa hayo, Serikali ilianza kurejesha miundombinu ya barabara na umeme katika wilaya hiyo sambamba na kuwajengea nyumba waliopoteza makazi, kazi ambayo bado inaendelea.

Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid, Anna Mzinga (kulia) akikabidhi nyaraka za makabidhiano ya mradi wa maboresho ya chanzo cha maji cha Nangwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Issa (kushoto).

Shirika la WaterAid nalo lilijitolea kusaidia kurejesha miundombinu ya maji iliyoharibiwa na mafuriko hayo kwa kukarabati chanzo hicho cha maji kinachotegemewa na kata 17 za Hanang kwa gharama ya Sh127 milioni.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhino ya mradi huo leo Aprili 18, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amesema shirika lake liliamua kukarabati chanzo hicho cha maji kwa kuwa wanaamini binadamu anahitaji majisafi na salama.

“Kufuatia changamoto hii iliyoikuta Wilaya ya Hanang mwishoni wa mwaka 2023, ilitufanya sisi kuwa hapa siku ya leo kwa sababu ili maisha ya mwanadamu yawe na utu na stara, tunaamini anapaswa kuwa na huduma za majisafi na salama pamoja na choo bora.

“Hivyo basi, tulisukumwa sisi kama shirika linalotekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira, kukarabati chanzo hiki cha maji cha Nangwa kilichoharibiwa vibaya sana na mvua kubwa,” amesema Mzinga.

Sambamba na ukarabati wa chanzo hicho cha maji, Shirika la WaterAid limetoa elimu ya usafi wa mazingira na vyoo bora katika ngazi ya kaya kwa watoa huduma za afya, wenyeviti wa kata na vijiji ili jamii kuwa na utayari wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Issa amesema amelishukuru shirika hilo kwa msaada walioutoa kwa wananchi wa Hanang na kuahidi wataitunza miundombinu hiyo ili idumu zaidi.

“Msaada huu ni mkubwa na tunawashukuru sana na niwaombe wananchi, muutunze vizuri miundombinu hii kwa kuwa mkiiharibu, mtakosa maji. Kwa hiyo kila mmoja awe mlinzi ili maji yaendelee kupatikana,” amesema Issa.

Wakazi waliohudhuria hafla hiyo wameshukuru kurejeshwa kwa huduma ya maji wakisema itawafanya waishi maisha mazuri kama waliyokuwa wakiishi kabla ya kutokea kwa mafuriko, mwishoni mwa mwaka jana.

“Tunaamini maji haya yatatufanya tuendelee na maisha yetu hata baada ya kupoteza kila kitu kwenye mafuriko yale. Tunawashukuru WaterAid kwa msaada huu, waendelee kusaidia na wengine,” amesema Isaack Lotu, mkazi wa Nangwa.

Related Posts