BAADA ya kuwepo kwa tetesi za nahodha wa taifa Stars, Mbwana Samatta, kuandika barua ya kustaafu kuitumikia timu hiyo, baba wa supastaa huyo ameibuka na kutolea ufafanuzi.
Mzee Ally Pazi Samatta amesema ingawa hakuzungumza na mwanaye, alizisikia taarifa hizo kwa watu wake wa karibu, ila anachomsisitiza straika huyo asikate tamaa kulitumikia taifa lake.
“Samatta hakunishirikisha juu ya kuandika barua hiyo, alijua wazi nitamkataza kuchukua uamuzi huo, changamoto haziwezi kukosekana sehemu yoyote ya kazi, kikubwa aangalie wale wanaomuunga mkono kulitumikia taifa lake na ajitume kwa ajili yao,” alisema na kuongeza;
“Baada ya kulifuatilia suala lake kwa kina, niliambiwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemkatalia ombi lake na kumtaka aendelee kuitumikia timu hiyo, ninachoweza kumshauri kijana wangu, aungane na Watanzania wanaopenda anachofanya, hao ndio wampe nguvu ya kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.
“Nafahamu yapo mambo yanayoumiza na kukatisha tamaa, mbaya zaidi Mbwana siyo muongeaji na ndio maana hakutaka kushauriana na mimi, ingawa niliipata barua aliyoandika baada ya kuletewa na mtu hapa nyumbani, nikaisoma na sikumuuliza chochote, najua akitulia atakuja kunielezea kwa kinywa chake.”
Mmoja wa vigogo kutoka TFF, alisema chanzo cha Samatta kuandika barua hiyo ni kutokana na jinsi ambavyo baadhi ya watu wanashindwa kutoa heshima kwa wachezaji.
“Kwanza ni nahodha anayesimamia posho za wachezaji kuhakikisha wanazipata kwa wakati, ni mfano wa kuigwa kwa nidhamu na kuhamasisha wengine kupambana na anapenda kuona vijana wanapata nafasi zaidi.
Aliongeza: “Ishu iliyomkwaza wakati timu ya taifa inashiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), nchini Ivory Coast, kulitokea kutoelewana kati ya benchi la ufundi na beki Dickson Job, Samatta alimkalisha chini mchezaji na kumtaka aombe radhi na akafanya hivyo, ajabu akashangaa vitu vinasambaa mtandaoni.
“Samatta anaamini yapo baadhi ya mambo yakitokea kambini yanaweza yakamalizika, bila kelele za mtandaoni ambako vinaweza vikaenda vitu visivyo sahihi.”
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Samatta kutojiunga na Stars baada ya awali kuomba kutojumuishwa kwenye kikosi kilichocheza mechi mbili za michuano mipya ya kirafiki ya Fifa Series iliyofanyika huko Baku, Azerbaijan, ambapo Stars ilifungwa bao 1-0 na Bulgaria Machi 22 na kisha kuichapa 3-0 Mongolia Machi 25. Job pia hakuitwa katika kikosi hicho.
Kwenye timu ya Taifa Stars, Samatta amefunga mabao 23, sawa na aliyoyafunga Simon Msuva, huku Mrisho Ngassa ndiye anayeongoza kwa mabao 25.
Hata hivyo, alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema habari za Samatta zimefafanuliwa kwenye mitandao ya kijamii ya TFF.
TIMU ALIZOCHEZA SAMATTA
2010/2011: (Simba SC), 2011–2016 (TP Mazembe),
2016–2020: (Genk)
2020: (Aston Villa)
2020–2023: (Fenerbahçe)
2021/2022: (Antwerp (mkopo)
2022/2023: (Genk, mkopo) na 2023 (PAOK).