Mume alia kunyimwa unyumba kwa miaka tisa

Mbarali. “Ni kama picha ya kuigiza kumbe kweli nimepitia vipindi vigumu katika maisha  ya mahusiano,  nimeambulia vipigo manyanyaso, kunyimwa unyumba na hata kutelekezewa familia.”

Ni kauli ya Elia John (48) mkazi wa Igurusi wilayani Mbalari Mkoa wa Mbeya ambaye amedai kupitia visa na mikasa kutokana na mwenza wake kumsaliti kwa miaka tisa baada ya kumfungulia duka la vinywaji.

“Maisha ya tabu yalinifika baada ya kumfungulia biashara ya vinywaji mwenza wangu, alipoanza kushika fedha ndipo dharau manyanyaso na hata vipigo vilikuwa ni haki kwangu,” anadai John ambaye ni baba watoto wawili.

Mwandishi wa gazeti hili alifika Kata ya Chimala Kijiji cha Mahenje na kufanya mahojiano na John ambaye pia ni mtoa huduma katika moja ya kituo cha afya Kata ya Igurusi.

John akiwa amevalia shati na suruali zote zikiwa na rangi nyeusi, anaonyesha furaha iliyochanganyika na huzuni.

Johna anasema mwaka 2015 baada ya kufiwa na mke wa kwanza, aliingia kwenye uhusiano na mwanamke mwingine aliyemuoa kwa taratibu zote za kimila na walifanikiwa kupata watoto wawili wa kiume.

Anasema mwaka 2017 aliona si vyema mwenza wake akaishi pasipo kujishughulisha wakati yeye ni mtumishi katika kituo cha afya na anapokea mshahara, hivyo alilazimika kukaa chini na mkewe huyo na wakapanga mipango mikakati ya kuongeza kipato ndani ya familia.

John anasema baada ya majadiliano, alimfungulia mkewe duka la vinywaji baridi kwa mtaji wa Sh1 milioni.

“Tuliendelea na safari ya maisha yetu, biashara ilikuwa nzuri na hata mahusiano, lakini ghafla tabia ya mke wangu ilianza kubadilika akawa anarudi usiku wa manane amelewa nikimuuliza ananiambia wateja walikuwa wengi,” anasimulia John.

 Anadai kuwa aliendelea na tabia hiyo, lakini kwa kuwa yeye ni mwanamume, alilazimika kuwa mvumilivu kwa sababu alikuwa bado anampenda mkewe.

John anadai kuwa licha ya kumvumilia, ilifikia hatua kila akimuomba unyumba mkewe alikuwa mkali na hata akimpa sio kwa upendo kama wakati wanaingia kwenye uhusiano.

“Ilikuwa inafikia wakati ananiuliza nimekupa penzi  mara ngapi kwa wiki hii, kwa kweli hili jambo lilikuwa linaniumiza sana kisaikolojia na limeniathiri mno, najikuta nakosa haki yangu ya msingi wa kupata tendo la ndoa,” anadai John.

Hata hivyo,  mkewe akaanza kurudi nyumbani alfajiri na hata kusahau majukumu ya kuwatunza watoto.

Johna anasema kazi hiyo akawa anafanya yeye ikiwamo kuwaogesha wanawe kuwafulia nguo na kuwapikia chakula.

Hata hivyo, mwandishi alimtafuta mkewe wa John, aliyejitambulisha kwa jina la Victoria Nsemwa (34) Mkazi wa Kijiji cha Luanyo Wilaya ya Mbarali anayesema kuna sababu nyingi zilizomfanya amnyime tendo la ndoa.

“Huyo ni mume wangu, mzazi mwenzangu, kwa kweli ni mvivu kufanya kazi, sio kwamba nilipenda kumuacha bali kwa vitendo alivyokuwa ananifanyia wakati naumwa,” anadai.

Nsemwa anadai kuwa kabla hajaugua ugonjwa wa akili, walipata watoto wawili na ndiyo hao waliobaki na mumewe baadaye familia yake ikaamua kumchukua kwa ajili ya matibabu aliyokuwa anafanyiwa na waganga wa  kienyeji.

“Nilipata tatizo la ugonjwa kama kichaa nilikuwa natoka nyumbani usiku na mtoto mgongoni natembea mpaka alfajiri, lakini mwenzangu alishindwa kunihudumia na badala yake akawa ananifungia ndani,” anadai Nsemwa.

Hata hivyo, anasema baada ya kutibiwa kwa waganga hao wa kienyeji, alipona na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Anadai kuwa baada ya kurejea nyumbani kwa mumewe alikuta ameoa mke mwingine, na yeye akachukua uamuzi wa kuolewa tena.

“Unajua nami ni binadamu mwili unahitaji chakula, baada yeye kuoa na mimi nikapata mwenza wangu ambaye mpaka sasa naishi naye na familia yangu inamtambua,” anadai Nsemwa.

Anakanusha kwamba alikuwa akimnyima unyumba mumewe kwa makusudi, “nilikuwa naumwa na nilikuwa sitambui kama nilikuwa namnyima, hayo ni maneno yake tu bwana.”  

Anadai kuwa, sio kwamba jukumu la kutunza alimuachia mumewe, Nsemwa anasema alikuwa akiwalea. “Hata mtoto wetu wa kwanza ambaye ameishia darasa la tano, nilimpeleka kusoma ufundi.”

Hata hivyo,  alipoulizwa sababu ya mtoto kushindwa kuhitimu elimu ya msingi, hakuwa na majibu.

Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Igurusi, Mkoa wa Mbeya, Casmiri Pius akizungumza na mwandishi wa habari hii. Picha na Hawa Mathias

Kuhusu upendo kwa mwenza wake

Anasema moyo wa kumrudia John ulishakufa kwa kuwa alianza kumsaliti ikiwamo kumtelekeza wakati anaumwa pasipo huduma.

Kuhusu kufunguliwa biashara kuwa chanzo cha usaliti, Nsemwa anadai kuwa si kweli bali yeye alikuwa akiuza uji na si kama alivyoeleza mumewe.

Hata hivyo, mumewe alipoulizwa kwa mara nyingine anasema alimfungulia duka la vinywaji baridi lakini biashara ya uji haifahamu.

Mwanamume afunguka zaidi kuhusu kuoa

Mume huyo wa Nsemwa anasema hana wazo la kuoa tena hasa anapokumbuka machungu anayopitia.

John anasema alifikia hatua ya kumuoa Nsemwa baada ya mke wake wa awali kufariki dunia na kumuachia mtoto mmoja, hivyo akaona ni vema akaoa mke mwingine wasaidiane kumlea huyo mtoto.

Hata hivyo, anasema kutokana na hiki kilichotokea limekuwa funzo kwake na hafikirii kuoa tena.

John amewataka kufunguka kwa sababu idadi kubwa wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kunyimwa tendo la ndoa, vipigo lakini usiri ndio unapelekea kufikia hatua mbaya hata kufanya mauaji ya  wenza wao au kujikatisha uhai wenyewe.

“Mwandishi… kunyimwa unyumba ni kitendo cha ukatili wa hali ya juu kutokana na maumbile ya mwanamume kwa muda ule anapohitaji na ndio maana tunajikuta kuwa katika kipindi kigumu,”anadai.

Anasema ifike wakati Serikali itambue wapo wanaume wengi wanafanyiwa  vitendo vya unyanyasaji,  hali inayosababisha wasio na uvumilivu kufanya matukio ya mauaji ya watoto na wenza wao.

“Elimu ikitolewa msongo wa mawazo huchochea vitendo vya ukatili na hata dharau kwa wanandoa ikiwamo mwanamke kumiliki uchumi mzuri, “anasea John.

 Kauli ya Ustawi wa Jamii

Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Igurusi, Casmiri Pius amekiri kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kimwili na kunyimwa unyumba  kwa wanaume.

Anasema kwa kipindi cha mwaka 2023 ni matukio matano  tu yameripotiwa lakini yapo mengi ambayo wahusika wanaona aibu kuripoti na kuishia kwenye ngazi ya familia

“Matukio ni mengi  lakini wapo wanaume ambao wanaona aibu kufika kwenye ofisi za kata au dawati la jinsia la polisi kufungua kesi hali inayosababisha kupata manyanyaso,  mateso ndani ya ndoa  na hata wengine kutelekezewa familia na wenza wao kwenda kuishi na wanaume wengine, ”anasema.

Pius anasema umefika wakati sasa wanaume kufunguka na sio kukaa kimya na  kufanya uamuzi mgumu ambao mwisho wa siku unawagharimu na kusababisha familia kuishi maisha ya tabu.

Msaidizi wa dawati ya jinsia Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Inspekta Loveness Mtemi anasema changamoto kubwa ni wanawake kuwa na maneno magumu kwa wenza wao pindi wanapomiliki uchumi mzuri.

“Ni kweli  wanacheza vikoba na kuwa na fedha lakini isiwe chanzo cha kutoa maneno makali kwa wenza wao ikiwamo mwanamume suruali, haya tunayasikia pindi wanawake wakipigwa wanapokuja kufungua kesi,” anasema.

Mtemi anasema kejeli za wanawake zinasababisha wanaume kufanya uamuzi mgumu ya kujiua, kuua watoto na wenza wao.

“Changamoto matukio ya wanaume kunyanyaswa na wenza  zipo lakini hawafiki kufungua kesi badala yake kufanya uamuzi mgumu kufanya mauaji ya wenza wao au  watoto jambo ambalo halimpendezi Mungu,”amesema.

Telesea Joel (45),   mkazi wa Sabasaba Jijini Mbeya anasema mifumo ya maisha ni kiini cha  wanandoa au walio katika uhusiano  hujikuta wakitengana na mmoja wao kubaki na familia.

“Mabadiliko ya maisha mwanamume kuona hana jukumu la kutunza watoto na ndio hapo vita inapoanza na wanawake wengi kujikuta kusaliti  kutoka nje ya ndoa ili  kupumua na kutelekeza watoto,” anasema.

Imeelezwa asilimia 50 kwa 50 ni changamoto kubwa inayosababisha wanaume kudharaulika na kujikuta kuishi katika kipindi kigumu wanapokuwa tayari wamepata familia.

Chriss Fredy, anasema alitelekezewa familia baada ya maisha yake kuyumba hali iliyomsababisha kupitia vipindI vigumu vya maisha namna ya kutunza familia hali iliyomfanya kupitia ukatili wa kihisia.

 Mwanasheria wa kujitegemea, Philipo Mwakilima anasema sheria ya mtoto mara baada ya kufarakana baba na mama wanaangali wa nani wa  kuweza kuwa simamia endapo shauri lipo  Mahakamani .

“Ila kiuhalisia mwenye jukumu la kutunza familia ni baba ingawa anapaswa mtoto akiwa na miaka saba ndio akabidhiwe kwa baba  mbali na kuwepo kwa migogoro ya ndoa ya kanisani au mahusiano ambayo yalipeleka  kupata familia.

Amesema kuhusu haki katika mgawanyo wa mali haijalishi nani alinunua bali sheria zitaangali pande zote kila mmoja anatapa mgawanyo kulingana na zilizochumwa wakati wakiwa kwenye uhusiano.

“Inaweza kutokea mwanamume akaonyesha hati za kumiliki hizo mali kwa kigezo mwanamke alikuwa hafanyi kazi, hilo halitambuliki kwa kuwa tayari mwenza wake alikuwa akitoa huduma ikiwamo ya kimwili, kufua na kumhudumia mahitaji mbalimbali kama mwenza wake,” anasema.

Imamu wa Msikiti wa Isanga, Sheikh Ibrahim Bombo anasema misingi ya kidini inamtaka wazazi wote wawili kwa pamoja wabebe jukumu la kutunza familia.

Anasema misingi ya imani kuna taratibu zinazofuatwa pale inapotokea tofauti za migogoro katika ndoa na sio dhambi baba kubeba jukumu la kutunza na kulea familia inapotokea tofauti.

Makala hii imeandikwa kwa ufadhili Bill & Melinda Gates Foundation

Related Posts

en English sw Swahili