Chalamila agusia Katiba mpya, wadau wamjibu

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametaja mambo matatu anayotamani yangepewa kipaumbele kwenye Katiba mpya ikiwamo wasomi wanaomaliza vyuo bila kuwa na ajira kwa muda mrefu walipwe mshahara nusu hadi pale watakapopata ajira rasmi.

Vipaumbele vingine ni wanafunzi wote wa vyuo vikuu wapewe mikopo na kusamehewa gharama za matibabu ya mtu aliyefariki dunia.

Akizungumza na wakazi wa Ilala leo Alhamisi Mei 30, 2024 , Chalamila amesema kinachomshangaza  hadi sasa waliombele kudai Katiba mpya, wanazungumzia zaidi  tume huru jambo analosema ni mipango ya wachache kutaka vyama vyao vishinde uchaguzi waingie madarakani.

“Nilitarajia wangesema mwanafunzi kwenda chuo kikuu haihitaji kuomba mkopo bali apewe mkopo wa lazima, lakini mtu aliyelazwa hospitalini na bahati isiyo nzuri akafariki dunia basi kwa mujibu wa Katibamaiti isidaiwe.

“Nilitarajia waseme kinamama wenye mtaji wa Sh100 milioni wakopeshwe na taasisi za kifedha bila riba hadi pale watakaposimama, lakini waulizeni wanaosema wanataka Katiba mpya wanayataja haya,” amesema Chalamila.

Amesema ukiangalia wengi wanaodai Katiba mpya wamejikita kwenye Tume Huru ya Uchaguzi huku akieleza hakuna tume itazaliwa na Rais wa nchi asiwe na mamlaka nayo.

“Itakuwa si nchi. Lazima Rais awe na nguvu hata ya kuiongoza tume kutimiza wajibu wake, sasa mtumishi wa tume akikosea atawajibishwa na nani? lazima kuwe na Mahakama itakayoweza kukiwajibisha chombo kinachoitwa Tume Huru. Wananchi lazima mjue hakuna uhuru usiokuwa na mipaka,” amesema.

Hata hivyo, mtazamo wake huo umepingwa na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe aliyesema  maoni hayo  lengo lake ni kufifisha jitihada za madai ya Katiba mpya.

“Kwa sababu yote anayoyasema yanaweza kufanyika hata bila Katiba mpya. Ushauri wangu ni kwamba atoe ushauri wa Serikali kufanya mambo hayo kama sio kwamba ana lengo ovu dhidi ya madai ya Katiba Mpya,” amesema Wangwe

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama Demokrasia na Maendeleo Chadema, John Mrema, amemjibu kwakuwa kiongozi huyo yupo ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), maoni yake hayo alipaswa kuwasilisha serikalini yatekelezwe.

Chalamila katika maelezo yake kupitia mkutano huo amesema hata Dar es Salaam kuna wazazi wamewaacha watoto wao huru kimalezi na sasa wanafanya wanavyojiamulia na wengine wamekuwa wadada wanaojiuza huru.

“Tunapozungumzia Katiba ni muhimu tunazungumzia masilahi ya watu ndani ya Taifa letu, si kikundi kidogo kubeba ajenda hiyo na kutaka kuturudi tulikotoka.Tunahitaji ufumbuzi wa mambo,” amesema

Chalamila amesema ufumbuzi wa mambo ni kama kuwawajibisha watendaji wabadhirifu kwa kuwa wanaanzia kwenye jamii ambako kila mmoja amezaliwa.

“Ndani ya Serikali wapo wa aina mbili wapo wenye hofu, uoga na wanatamka neno rushwa na kuukata wizi kutoka moyoni lakini kuna wale wanaotamka hakuna rushwa wala wizi kwa usanii tu lakini  mtamkaji ni mwizi mkuu,” amesema

Amesema makundi hayo yote yapo na kuwataka wananchi kujenga utamaduni wa kumulika nafsi za viongozi watagundua baadhi wanaotamka ni wasanii.

Related Posts