Wizi wa misalaba makaburini wawashitua Shinyanga

Shinyanga. Usemi wa “Kufa Kufaana” unakamilisha dhana ya kinachoendelea mjini Shinyanga kutokana na kukithiri kwa wizi wa misalaba kwenye makaburi.

Wakati wananchi wakiomboleza kuwapoteza wapendwa wao na kuwasitiri vema kwa kujengea makaburi na kuweka misalaba juu yake kulingana na imani zao, watu wasiojulikana wamekuwa na ujasiri wa kuiba misalaba hiyo.

Misalaba inayolengwa zaidi  ni ile ya chuma ambayo huuzwa kama chuma chakavu, tofauti na maeneo mengine ambapo hata ile ya mbao huibwa kwa kutumika kama kuni kwa mama lishe.

Katika manispaa ya Shinyanga, wizi umeripotiwa katika Mtaa wa Dome, Kata ya Mdembezi, jambo linalotajwa kuchochewa na biashara ya vyuma chakavu.

Kutokana na tatizo hilo wakazi wa Kata ya Ndembezi wameiomba Serikali kuchukuwa hatua kali kwa wananchi watakaobainika kuiba misalaba makaburini.

Wakazi wa eneo hilo waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa makaburi katika eneo hilo kwa kubomoa vigae vilivyotumika kuyajengea ili kufanikisha wizi huo.

Mkazi wa Mtaa wa Dome, Wencesilaus Modest amesema wamekuwa na utaratibu wa kwenda kusafisha makaburi na wanapofika hukuta mengi hayana misalaba huku mengine yakiwa yameondolewa vigae.

Amesema tatizo hilo linachangiwa na uwepo wa biashara ya vyuma chakavu ambapo baadhi ya watu wamekuwa hawana hofu ya Mungu na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili.

“Hili tatizo limekuwa kubwa, mwanzoni hali haikuwa hivi lakini sasa makaburi mengi hayana misalaba na mengine yamevunjwa, wanachukua nondo kwenye misalaba ya zege na ile ya chuma wanaenda kuuza kama vyuma chakavu,” amesema Modest.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Edina Joseph amesema licha ya misalaba pia kumekuwa na wizi wa vigae ambavyo vimekuwa vikiuzwa nmtaani kwa ajili ya kuweka jikoni, kwenye korido na vyooni.

Ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga uzio maeneo ya makaburi ya umma ili kukomesha tatizo hilo.

“Biashara ya vyuma chakavu imeibua mambo mengi, sasa hivi hata mtaani ukiacha nje jiko la chuma au sufuria hata kama limepasuka kidogo hulikuti, watu wanaiba na sasa wamehamia hadi makaburini, wanavunja, wanaiba misalaba,” amesema Edina.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Solomoni Najulwa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, tatizo alilosema amesema linasababishwa na uwepo wa biashara ya vyuma chakavu.

Amesema wizi iliokuwa ukifanyika mwaka 2015, watu walikuwa wanaiba misalaba ya mbao na kwenda kuuza kama kuni lakini walifanikiwa kuwadhibiti kupitia ulinzi shirikishi, sasa baada ya kuibuka biashara ya vyuma chakavu, watu wanavunja makaburi na kuchukua misalaba ya chuma.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani alipoulizwa alisema wamepata taarifa ya wizi wa misalaba makaburini na wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivyo.

Amesema kupitia msako na doria wamekamata vipande vya nondo 250 kwa watu wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu, lakini si misalaba na uchunguzi unaendelea maeneo mbalimbali ili kukomesha wizi huo.

Akizungumzia umuhimu wa kutunza makaburi, Paroko wa Parokia ya Shinyanga Mjini, Padri Anatory Salawa amesema jamii haijawajibika kutunza makaburi, hali ambayo imekuwa ikisababisha kuwa sehemu ya maficho ya wahalifu.

Amesema vitendo vya wizi wa misalaba makaburini ni uhalifu kama mwingine kutokana na tamaa ya mali, bila kuangalia mali hiyo inatafutwa maeneo gani na inachangiwa na malezi na maadili ya kutokuheshimu sehemu takatifu.

Padri Salawa amesema vitendo hivyo vya wizi makaburini unafanywa na watu ambao hawana hofu ya Mungu.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyabiashara wa vyuma chakavu mjini Shinyanga, John Alphonce amesema wanafanya kazi hiyo kwa kuzingatia maadili kwa kununua vyuma chakavu ambavyo vimeisha na si misalaba.

Amesema biashara ya vyuma chakavu inawaingizia kipato lakini wapo baadhi wanaonunua vitu ambavyo havitakiwi na akaiomba Serikali kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kuwabaini.

Related Posts