Dodoma. Wabunge wameitaka Kamati ya Bunge ya Bajeti kufanya mapitio upya ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi ili kuongeza fedha kwa wizara hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa jana Mei 29, 2024 aliwasilisha bajeti ya wizara hiyo huku akiomba Bunge lipitishe Sh1.7 trilioni kwa mwaka 2024/25.
Hata hivyo, wabunge wamesema kiwango hicho cha fedha hakitafikia malengo kwa kuwa mvua zimeharibu miundombinu katika maeneo mengi, hivyo ilistahili bajeti kubwa zaidi ya hiyo.
Akichangia mjadala huo leo Alhamisi Mei 30, 2024, mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wabunge kupitia vikao vya Kamati ya Bunge ya Bajeti kushawishi Serikali kuiongezea fedha Wizara Ujenzi katika bajeti ya wizara hiyo.
“Ni kwamba fedha za miradi hazitoshi tumekumbushwa hapa fedha za madeni na riba ukipiga hesabu inafika karibia Sh1 trilioni, kwa hiyo hii wizara ndugu zangu waheshimiwa wabunge wana Sh700 bilioni kwa ajili ya kutekeleza barabara…ukigawa kwa vyovyote vile huyu waziri ana kazi ya kujenga kilometa 500 tu,” amesema Profesa Muhongo.
“Katika mikoa 26 lazima tumuombee fedha na ambao tumekaa bungeni kwa muda kuiombea wizara kuongezewa fedha sio jambo geni wala sio la ugomvi, ni sisi wabunge tuelekeze kwamba kile kipindi cha majadiliano Waziri wa Fedha akikaa na Kamati ya Bunge ya Bajeti lazima waongezewe fedha hawa.”
Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya amesema hakuna kinachoshindikana ndani ya wizara hiyo isipokuwa wanakwamishwa na ufinyu wa bajeti waliyopewa ukilinganisha na majukumu ya kuifungua.
Manyanya amesema kuna wasiwasi Waziri wa Ujenzi akaitwa ‘Aristote’ kwa sababu ya bajeti ya wizara hiyo ambayo ni ndogo kwa kuwa hakuna mtu anaweza kufanya masuala ya kiufundi kwa kuangalia philosophy.
“Waziri ulipokwenda Liwale yule mkandarasi alikwambia fani ya yule mkandarasi wake ni philosophy, sasa nina wasiwasi kwa sababu unapewa majukumu makubwa lakini fedha hupewi, bajeti hii ni ndogo sana na nashukuru spika tupo naye humu ndani bajeti hii ikaangaliwe upya,” amesema.
Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula ametaja miradi mikubwa iliyoonyesha matumaini kwa wananchi ikiwamo kukamilika kwa Daraja la Usagala, meli za Mv Mwanza na Mv Umoja na kuboresha miundombinu ya bandari kuwa kielelezo cha kuwataka wabunge waunge mkono bajeti hiyo ili Serikali itekeleze maeneo yaliyobakia.
Mbunge wa viti maalumu Stella Fiyao amependekeza angalau bajeti ya ujenzi iwe Sh5 trilioni ili itoshe kutekeleza majukumu yake vizuri na kuepuka mzigo wa madeni unaoonekana kuwaelemea akitolea mfano madeni ya makandarasi Sh915 bilioni.
“Waziri kuna changamoto kubwa sana, sisi kama kamati tumeendelea kushauri siku zote kwamba ili tuvuke walau tuwe na Sh5 trilioni kwasababu tunajua, kuna miradi mingi tunaendelea kutekelezwa huko kwenye maeneo yetu,” amesema Stella.
“Tukiangalia kwenye ishu ya bajeti ya miradi ya maendeleo tuna Sh1.7 trilioni, ni nini tunakwenda kufanya? Na tukiangalia mrundikano wa madeni Sh915 bilioni tunadaiwa na makandarasi ni kitu gani tunachokwenda kufanya ili kuhakikisha mahali hapa tunavuka.”
Mbunge viti maalumu, Mary Masanja amesema Waziri Bashungwa alionyesha uzalendo mkubwa katika kipindi kigumu na ilimlazimu kupanda pikipiki ili kuyafikia maeneo magumu jambo ambalo si kawaida kwa waziri.
Hata hivyo, Masanja ameomba Serikali kuongeza fedha katika wizara hiyo ili wananchi waweze kunufaika matunda mazuri ya Serikali yao akidai fedha zilizotengwa kwa 2024/25 hazitoshi.
Akizungumzia magumu yaliyotokana na mvua za El-Nino, mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka amesema kazi iliyofanywa na Bushungwa kwa kutumia chopa na boti ilipeleka matumaini makubwa kwa wananchi wa jimbo lake na mkoa mzima wa Lindi.
Mbunge wa Madaba Dk Joseph Mhagama amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kutenganisha Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi lakini kwa uteuzi wa waziri mwenye maono anayetambua majukumu yake.