NMB yawatangazia fursa vijana wenye bunifu mbalimbali

BENKI ya NMB imeshiriki kwenye maadhimisho ya elimu, ujuzi na ubunifu yanayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlaly huku ikitoa fursa kwa vijana wenye bunifu mbalimbali kwenda kufanya majaribio kwenye mfumo maalum wa majaribio katika benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Hayo yalisemwa na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ambapo alisema kwamba benki hiyo inatambua umuhimu wa ubunifu katika maendeleo ya nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf Mkenda (kushoto) akipokea maelezo ya Benki ya NMB kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus (kulia) alipotembea banda la Benki hiyo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlaly.

Baraka alisema kwamba wao kama benki pamoja na ufadhili wa maonesho hayo, pia wanatoa Jukwaa Maalumu na kuwakaribisha vijana kufanya ubunifu kwani Benki ya NMB imekuwa ikifadhili maendeleo ya kibunifu na miradi hiyo.

“Kwa niaba ya Benki ya NMB niwaambie kwamba tunatambua umuhimu wa ubunifu na ndio maana tumeungana nanyi katika wiki hii kwa kuwa elimu ndio inachochea ubunifu sisi kama Benki pamoja na mfadhili tunatoa jukwaa maalumu kuwakaribisha vijana kuja kufanya ubunifu kufanya maendeleo ya kibunifu na miradi itakayo kuwa bora zaidi basi tutaifadhili,” alisema meneja huyo wa kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Hata hivyo, alisema Benki kufanya hivyo inasaidia kuleta chachu ya kuendelela kuleta mendeleo ya ubunifu Tanzania hivyo wataendelea kuwaunga mkono kuhakikisha maendeleo ya sekta hiyo yanapiga hatua kubwa.

“Mh Waziri niwakaribishe vijana wenye bunifu mbalimbali waje kufanya majaribio yao kwenye benki ya NMB tuna jukwaa la NMB Sandbox zuri ambalo linatoa nafasi nzuri ya bunifu tupo tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha ubunifu unaleta chachu ya maendeleo ya kiuchumi hapa nchini,” alisema.

Awali, akizungumza wakati akifungua maadhimisho hayo, Profesa Mkenda alisema Serikali ipo katika mchakato wa kujenga shule 100 za mafunzo ya Amali nyanja ya ufundi nchi nzima ili kuwawezesha vijana wa kitanzania kuweza kujiajiri au kuajiriwa kupitia ujuzi watakaopata kupitia vyuo hivyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema dunia ya sasa ina mabadiliko makubwa hasa kwenye masuala ya sayansi na teknolojia ujuzi na ubunifu hivyo ni wakati wa vijana wa Kitanzania kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Awali, Katibu mkuu wizara ya elimu sayansi na teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema wanafunzi 27 walishinda shindano la ujuzi na ubunifu ngazi ya vyuo ambao watafanyiwa mchakato na kupatikana wanafunzi 3 wa fani tofauti ambao watakwenda kushiriki mashindano ya kikanda na kimataifa mapema mwaka 2025.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema bunifu zinazoibuliwa katika maeneo mbalimbali nchini  zitengenezwe katika uhalisia ili kuleta tija kwa jamii na kiuchumi.

Mwenyeji wa maadhimisho hayo ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani amesema mkoa wa Tanga umepokea Sh2.6 trilioni kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu ambapo shule mpya 27 zimejengwa pamoja na vyuo vya kati ambavyo vipo katika hatua mbalimbali.

Related Posts