Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inashiriki maonesho ya 27 ya Wiki ya Unywaji maziwa Kitaifa jijni Mwanza huku ikiwataka wafugaji kutembelea banda la benki hiyo kwa ajili ya kupata taarifa za fursa mbalimbali kwa ajili yao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumza muda mfupi baada ya uzinduzi rasmi wa maonesho hayo, Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Alphonce Makoki alisema benki hiyo inatoa mikopo ya riba nafuu kwa wafugaji na kuwataka wafugaji waliopo kanda ya ziwa na maeneo ya Jirani kuchangamkia fursa.
Alisema TADB ni mdau mkubwa kwenye sekta ya mifugo na inatambua umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya taifa na kuongeza kuwa benki hiyo inatoa mitamba bora kwa wafugaji ambayo inasaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa.
“Kupitia mitamba tunayotoa wafugaji wanaweza kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa lita 8 hadi 10 kufikia lita 20 na kuendelea. Maziwa yanapokuwa mengi yanasaidia viwanda vyetu kuweza kusindika na kuuza zaidi,” alisema