Singida. Joto la uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 limeendelea kufukuta ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), huku Dk Emmanuel Nchimbi akiwaonya wanaopanga safu za wagombea au kujipitisha kuacha mchezo huo.
Dk Nchimbi, ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM amesema hatua hiyo inawanyima usingizi viongozi waliopo kwenye dhamana kutekeleza wajibu wao.
“Tukatae mchezo huu wa kupanga safu na wale wote wanaotaka kugombea kama fursa,” amesema leo Alhamisi, Mei 30, 2024 katika kikao cha ndani cha viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mabalozi hadi mkoa kilichofanyikia mjini Singida.
Si mara ya kwanza onyo kama hilo kutolewa kwa wale wanaojipitisha au kupanga safu za wagombea kwenye chaguzi hizo.
Oktoba 9, 2023, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akiwa wilayani Mkinga, mkoani Tanga aliwaonya makada wa chama hicho walioanza kujipitisha kuacha, vinginevyo wanajimaliza wenyewe.
Abdulla ambaye ni mlezi wa chama hicho Mkoa wa Tanga alisema: “Wabunge na madiwani bado wapo madarakani, waacheni wafanye kazi kwa amani, wasubiri muda mwafaka. Chama hakiruhusu hili.”
Mei 15 2023, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akiwa Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa mikutano wa CCM wilayani humo na kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya kupumzikia wageni alionya wanaoanza kampeni mapema.
Chongolo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe alisema chama hicho kina taratibu na miongozo yake na wale walioanza kutaka nafasi za ubunge na udiwani wanakiuka taratibu.
Kutokana na hilo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa akizungumza na Mwananchi amesema:
“Si mara ya kwanza kwa viongozi wa vyama hasa CCM kukemea majira yanapokaribia, kauli kama hizi huenda huwa kuna ushahidi au wamezoea unapokaribia uchaguzi watu huwa wanajipanga.”
“Lakini mara zote sentensi hiyo haijawahi kuwazuia na kushindwa kujipanga kwa sababu ni sentensi ya majukwaani, unataka kuwafurahisha wanaokusikiliza, njia nzuri anayopaswa kufanya wale anaowajua wanafanya taratibu zisizokubalika na kwa kuwa ni wanachama awaite na kuzungumza nao,” amesema.
Dk Kahangwa amesema hilo litasaidia kukilinda chama ndani.
“Si kuongea tu na watu wataendelea kupita. Kama wao wenyewe ziara yao ni kuangalia maandalizi ya uchaguzi sasa kwa nini wagombea wasijipitishe?” amehoji.
Mhadhiri huyo anaufananisha Uchaguzi Mkuu 2025 na mbio za urais 2030 akisema:
“Kama Rais Samia ataendelea hadi 2030, hawawezi kujiandaa kwa muda mrefu, kwa hiyo watu wanaanza kujipanga kuanzia sasa. Kwa hiyo, kama katibu mkuu ana maanisha basi achukue hatua si kuzungumza tu jukwaani.”
Dk Nchimbi leo Alhamisi, Mei 30, 2024 amesema: “Kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila mmoja, hatuwezi kwenda wote, tunachagua wachache kwenda kutuwakilisha, sasa wakati ukifika tuchague watu ambao watasimama mbele kwa wananchi wetu, si wale wanaotafuta fursa.
“Changamoto tunayokutana nayo kwa sasa ni watu kutoruhusu waliochaguliwa kutimiza wajibu wao, sasa tunaandaa wagombea, wanawanyima usingizi waliopo,” amesema.
“Ukiwauliza kwa nini mnamtaka huyo? utasikia wanasema ana hela huyo, viongozi kataeni kutumika na kutumika ni kubaya,” amesisitiza.
“Tengenezeni ramani ya kupata wagombea wazuri, wapimeni watu wetu kwa uwezo wa kuongea, kutatua kero za wananchi na si fedha. Tuwachague watu kwa kupima uyatari wao wa kuwatumikia,” amesema.
Mwanachama wa chama hicho Kata ya Solya, Bosco Wanguru aliyezungumza na Mwananchi amesema kinachozungumzwa na Dk Nchimbi ndicho kinaendelea na kinasababisha mvutano wa viongozi walipo na wanaotaka kuingia.
Ujumbe wa Makalla kwa viongozi
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla amesema lengo la ziara hiyo katika mikoa mitano ya Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ni kuangalia uhai wa chama kuanzia mabalozi wa chama hicho ambako huko chini ndiko kwenye wanachama.
“Mabalozi ndio msingi wa chama chetu, tunatambua mchango mkubwa unaofanyika ngazi ya chini na kwa taarifa tuliyopewa, Singida itaendelea kuwa ngome ya CCM. Ni mkoa ambao upinzani hauna nafasi,” amesema Makalla.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema mkoa uko salama na uhusiano baina ya chama na Serikali unaendelea vyema.
Amesema uhusiano huo ndiyo unafanya shughuli za maendeleo kuendelea kufanyika.