Rufiji. Benki ya CRDB imekabidhi msaada wa mbegu za mahindi zenye thamani Sh50 milioni, kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika msimu wa masika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Benki hiyo imekabidhi kilo 7,148.857 za mbegu za kisasa za mahindi, zitakazosambazwa kwa wananchi ili wazitumie katika msimu ujao wa kilimo ili kuhakikisha wanakuwa na chakula cha uhakika.
Akikabidhi msaada huo uliopokewa na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma CRDB, Tully Mwambapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Foundation amesema taarifa za athari za mafuriko zimewagusa wengi na hivyo wametoa msaada huo utakaosaidia kurudisha shughuli za kilimo kwa uhakika.
“Majanga yana athari kubwa zinazorudisha nyuma uchumi wa watu na maendeleo ya taifa kwa jumla. Mara zote, hutukuta hatujajipanga kukabiliana nayo au hatuna uwezo wa kuyazuia yasitokee.
“Hii ndio sababu iliyoishawishi CRDB pamoja na kampuni zake tanzu kushirikiana bega kwa bega na Serikali, kukabiliana na majanga pindi tu yanapotokea ili kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika,” amesema Tully.
Tully amesema walipopata maombi ya uhitaji wa mbegu hizo kutoka kwa Waziri wa Tamisemi na Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko, hawakufikiria mara mbili kwa kuwa waliona ni jambo jema litakalowasaidia waathirika kupunguza athari walizopitia na kurejesha hali zao kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele ameishukuru CRDB akisema kitendo ilichokifanya cha kuwakumbuka na kuwakimbilia waathirika wa mafuriko yaliyotokea ni cha kizalendo na kinachopaswa kuigwa na wengine.
“Moyo wangu na kichwa changu kama ilivyo kwa wana Rufiji wengi leo, vimejaa shukrani nyingi. Tunawashukuru CRDB kwa kutukimbilia kipindi hiki kigumu. Msaada huu umekuja wakati muafaka kwa kuwa utatusaidia kujikwamua kutoka katika athari za mafuriko kwa kupunguza gharama za kilimo hivyo kutuhakikishia mavuno msimu ujao,” amesema Meja Gowele.
Amesema mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu zimesababisha mafuriko ambayo yameharibu mazao shambani na hata baadhi ya biashara, hivyo kuwarudisha wananchi wengi kwenye umaskini.
Sambamba na msaada huo, imetoa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kwa wanawake na vijana wilayani humo, ili kuwaandaa kwa ajili ya kunufaika na mtaji wezeshi utakaosaidia kuinua uchumi wao.
Tully amesema mafunzo hayo yanaratibiwa na Programu ya Imbeju ambayo mpaka sasa imeshawajengea uwezo zaidi ya wajasiriamali 350,000 pamoja na kuwapa mtaji wezeshi wa Sh10 bilioni nchini.
“Kupitia programu ya Imbeju leo hii tutakwenda kutoa mafunzo kwa wanawake na vijana juu ya namna gani programu hii inaweza kuwasaidia kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi ikiwamo biashara na kilimo.
“Wataalamu wetu watatoa mafunzo ya ujasiriamali na kuainisha fursa zinazoambatana na programu hii, ikiwamo ile ya matumizi ya nishati safi kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya chakula maarufu kama mama lishe,” amebainisha Tully.
Kuhusu mafunzo kwa wajasiriamali hao, Meja Gowele amesema anaamini maarifa watakayoyapata yatakuwa na manufaa makubwa kwa washiriki, familia zao na jamii nzima kwa jumla.