Ukarabati kivuko cha MV Magogoni kukamilika Desemba

Dodoma. Bunge limeelezwa ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni utakamilika mwishoni mwa Desemba, 2024 na kitaanza kutumika.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema hayo leo Alhamisi, Mei 30, 2024 akijibu swali la msingi la mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile.

Mbunge huyo alihoji ni lini matengenezo ya Mv Magogoni nje ya nchi yatakamilika na kurejeshwa nchini ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.

Kasekenya amesema ukarabati wa kivuko hicho unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, 2024 na kurejeshwa nchini ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Katika swali la nyongeza, mbunge wa viti maalumu Kunti Majala amesema kivuko hicho kimetumia muda mrefu, hivyo watu wa Kigamboni wamekuwa wakipata adha kubwa ya usafiri.

“Lakini Serikali imekuwa na ahadi zisizotekelezeka, mmesema Desemba 2024 kitakwenda kukamilika ni tarehe ngapi? Tunataka tarehe ili wananchi waondokane na adha hii,” amehoji Kunti.

Akijibu swali hilo, Kasekenya amewakumbusha wananchi kuwa ukarabati unaofanyika ni kama kukijenga upya kivuko hicho kwa kuwa kilichoka sana.

“Ndiyo maana kimeendelea kuchukua muda mrefu ili kukiboresha kiwe kivuko cha kisasa. Tunataka kuhakikisha kabla ya mwisho wa Desemba kiwe kimekamilika na kuanza upya kufanya kazi,” amesema.

Katika ripoti maalumu iliyochapishwa na Mwananchi baada ya uchunguzi wa miezi mitatu, ilielezwa kivuko hicho kilipelekwa nchini Kenya, Februari mwaka jana kwa matengenezo kwa kipindi cha miezi sita, yaani hadi Agosti, 2023.

Uchunguzi ulibaini Serikali haikuwa imekamilisha malipo ya mkandarasi kwa ajili ya matengenezo ya kivuko hicho.

Malipo ya awali yaliyopaswa kufanywa tangu Februari, 2023 yamefanyika Februari mwaka huu.

Ilibainika malipo yaliyofanyika Februari ni asilimia 10 ya yote ya Sh7.5 bilioni ambayo mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd anapaswa kulipwa.

Ofisa wa ngazi ya juu kutoka kampuni hiyo ya Mombasa nchini Kenya, aliliambia Mwananchi kuwa, hadi sasa ni kazi za awali tu ndizo zilizoanza kufanyika.

Anaeleza matengenezo hayo yalipaswa kuanza kivuko kilipofika karakana, lakini ilishindikana kwa kuwa Serikali ya Tanzania haikuwa imelipa.

“Matengenezo yanahitaji vipuli na vifaa vingine ambavyo African Marine and General Engineering Company Ltd inapaswa kuagiza kwa fedha, kama hakuna fedha iliyolipwa si rahisi kuanza kazi,” alisema ofisa huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, malipo ya awali yaliyopaswa kufanyika mwaka jana, yamelipwa Februari, 2024.

“Kazi zimeanza lakini ni zile za awali na matengenezo yale yanahitaji kubadilisha kila kitu zikiwamo injini nne, kwa hiyo hatujafikia hata kuagiza injini, ambao nao ni mchakato unaochukua zaidi ya miezi sita,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Lazaro Kalahala alisema shughuli zinaendelea na kivuko kitarejea.

“Serikali inafanya kila namna kuhakikisha matengenezo yanafanyika ili kivuko kirejee na wananchi waendelee kupata huduma,” alisema.

Kivuko cha Mv Magogoni kilichoanza kazi mwaka 2008 kikiwa na uwezo wa kubeba tani 500 ni kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na Magogoni.

Related Posts