Mbunge amtaka waziri asimpige ‘sound’

Mbunge wa viti maalumu, Cecilia Pareso amemtahadharisha Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa kwamba amechoka kupigwa ‘sound’ (maelezo) kuhusu ujenzi wa Barabara ya Mang’ola-Lalago hadi mkoani Simiyu yenye urefu wa kilometa 129.

“Ni barabara ya muda mrefu sana ambayo mlituahidi mtajenga kwa kiwango cha lami kilometa 129 kwa upande wetu wa Karatu kabla ya kuunga upande wa Simiyu, mmeahidi, mmekuwa mkituambia sijui usanifu unafanyika, upembuzi yakinifu miaka na miaka toka wabunge waliopita, toka 1995 mpaka leo mnatuahidi,” amesema Pareso wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi.

“Mheshimiwa (Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa) natamani kusiki kauli kuhusu barabara  hii wakati unahitimisha hoja yako, lakini usije ukatupiga ‘sound’ hapa tumeshapigwa ‘sound’ muda mrefu sana. Tunatamani na wananchi wanatamani kusikia ni lini kwa uhakika barabara  hii mtajenga kwa kiwango cha lami, hata kwa kuanza kilometa chache kwanza fungueni,” amesema Pareso.

Pareso ametaja Barabara ya Karatu-Mbulu kwamba walipelekewa mkandarasi kusaini mkataba, lakini hadi sasa hakuna kilichoendelea.

“Mliishakuja mkasaini pale mkatuletea makandarasi pale tukafanya kasherehe  kadogo, mpaka leo ndio maana nasema mnatupiga ‘sound’, mpaka leo hakuna, najua kwa upande ule wa Manyara imeshaanza lakini kwa upande wetu bado, ni lini au tuendelee kusikiliza habari ya upembuzi yakinifu, sijui mchakato, siku hizi mmetuletea na hichi kitu kinaitwa EPC + F (Engineering, Procurement, Construction and Financing).

“Yaani kila siku mnatupiga maneno maneno fulani hivi ambayo yanatupa matumaini, lakini kule ‘field’ hakuna kinachotokea. Lakini, kumbuka Karatu ni kitovu cha utalii. Watalii wanakwenda kule kuangalia Wahadzabe ndiko waliko. wanapatikana kule,” amesema.

Pareso pia amezungumzia ubora wa barabara ya Makuyuni mpaka lango la Ngorongoro kwamba ina umri wa miaka 20 lakini haina hata tobo.

“Ni miongoni mwa barabara ‘the best’ katika nchi, ina miaka 20, ukipita  pale haina hata tobo haina. Ilikuwa imepewa muda wa matazamio wa miaka 15 imeshaisha, sasa hivi ina miaka 20, ni barabara nzuri na bora sana.

“Nataka nikuulize huyu mkandarasi aliyejenga hapa na hawa makandarasi wanaojenga barabara za siku hizi, hivi kuna utaalamu ule ule au kuna utaalamu umeongezeka. Utaalamu wa siku hizi barabara haina hata miezi imeshaanza kuwa na matobo.

“Tunaweka fedha nyingi, tunatumia fedha nyingi za Watanzania walipa kodi, lakini barabara ni chakavu ni mbovu inatengenezwa kiujanja ujanja mnno,” amesema.

Related Posts