Lema abwaga manyanga Chadema kaskazini

MWENYEKITI anayemaliza muda wake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ametangaza kutogombea tena nafasi hiyo ili kulinda maslahi ya chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Lema ametangaza msimamo huo leo Alhamisi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, ikiwa ni siku moja tangu Chadema ianze kufanya uchaguzi wa kutafuta viongozi wa kanda zake.

Lema amesema katika kipindi cha uongozi wake kilichosalia, ataendelea kufanya ujenzi wa Chadema.

“Kwa ajili ya ustawi wa chama changu na uimara wake katika kujenga misingi bora na muhimu haswa katika kipindi hiki tunachoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025, sitagombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda kwa mara hii katika uchaguzi unaokuja. Kwa sasa nitafanya wajibu wangu muhimu wa ujenzi wa Chama katika kipindi kilichobakia,” ameandika Lema.

Msimamo huo wa Lema imekuja siku moja tangu alipompongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, kukubali matokeo ya uchaguzi yaliyomuondoa madarakani na kumuweka Joseph Mbilinyi (Sugu).

Lema aliunga mkono kauli iliyotolewa na Mchungaji Msigwa hapo jana baada ya kuanguka katika uchaguzi wa Kanda ya Nyasa, iliyosema uongozi sio cheo.

“Haitakuwa mpweke kwa muda mrefu sana katika klabu ya wanachama waandamizi, watu wengi tutaungana na wewe katika siku za hivi karibuni pengine kwa style tofauti tu,” aliandika Lema akimpongeza Msigwa.

Related Posts