Lema kutotetea nafasi ya Uenyekiti Kaskazini, makada watofautiana

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini anayemaliza muda wake, Godbless Lema amesema hatagombea tena kiti hicho, katika uchaguzi ujao wa kanda hiyo utakaofanyika Julai.

Lema aliyechaguliwa uenyekiti wa kanda kaskazini mwaka 2019 alitoa msimamo huo jana kupitia akaunti yake ya mtandao wa X zamani Twitter huku akitaja sababu za kufikia uamuzi huo.

Hata hivyo, msimamo huo wa Lema umepokelewa kwa hisia tofauti na makada wa Chadema kanda ya Kaskazini, wakisema wameshutushwa na uamuzi huo, huku wengine wakisema wanaheshimu uamuzi wake.

Jana katika akaunti yake X Lema aliandika; “Kwa ajili ya ustawi wa chama changu na uimara wake katika kujenga misingi bora na muhimu hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na uchaguzi mkuu 2025, sitagombea nafasi ya uenyekiti wa kanda mara hii katika uchaguzi unaokuja.

“Kwa sasa nitafanya wajibu wangu muhimu wa ujenzi wa chama katika kipindi kilichobaki,” ameandika Lema ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.

Msimamo wa Lema umekuja siku moja baada ya juzi aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kushindwa kutetea kiti chake mbele ya Joseph Mbilinyi maarufu Sugu katika uchaguzi uliofanyika jana Mei 29 2024 Makambako mkoani Njombe.

Katika uchaguzi huo, Sugu alimshinda Mchungaji Msigwa kwa kura 54 dhidi ya 52 alizozipata mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, Lema alitumia ukurasa wake wa X kuandika; “Nimefurahi nilipoisikiliza hotuba yako (Msigwa) baada ya uchaguzi wa kanda ya Nyasa kumalizika, umesema thamani yako sio cheo, what you actualy mean, leadership is not a title fantastic message.

“Na pia muhimu zaidi umesisitiza kuendelea kuwa mwanachama senior wa chama na upo tayari kutumwa popote ku share nguvu na uzoefu wako, jambo la baraka sana,” alisema.

Walichokisema makada wa Chadema

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kinondoni, Herny Kilewo amesema ameshtushwa na taarifa hizo, anajipanga kuonana na Lema wazungumze kama ataweza kubadili msimamo.

“Siungi mkono uamuzi wake, kwa hali ya sasa siasa za kaskazini bado zinamhitaji kwa sababu ana nguvu na ushawishi,” amesema Kilewo.

Wakati Kilewo akieleza hayo, mwenyekiti wa kamati ya fedha wa kanda ya Kaskazini, Gervas Mgonja amesema anaheshimu uamuzi na msimamo wa Lema.

“Sijazungumza naye, nimeona katika mitandao ya kijamii, lakini kwa hatua ya sasa naheshimu uamuzi wake,”amesema Mgonjwa.

Spika wa Bunge la Wananchi la Chadema, Suzan Lyimo, amesema kila mtu ana uamuzi wake katika siasa na uongozi.

“Tutaukosa uongozi wake anajua kuhamasisha, nitaongea naye kujua hili,” amesema Lyimo.

Naye, mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), wilayani Arusha Emmanuel Zakaria maarufu ‘Baba Bony’ amesema bado anatafakari uamuzi wa Lema.

Chaguzi kanda za Nyasa, Magharibi na Serengeti

Wakati huo huo, uchaguzi wa kuwania uenyekiti katika kanda tatu za Chadema uliohitimishwa jana ulikuwa moto kutokana na ushindani mkubwa ulikuwepo.

Kanda zilizofanya uchaguzi ilikuwa ni Magharibi (Kigoma, Katavi na Tabora) Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu) na Nyasa (Mbeya, Rukwa, Songwe, Iringa na Njombe). Wakati kanda ya Victoria (Kagera, Geita na Mwanza), ilifanya uchaguzi Mei 25, 2024.

Uchaguzi huo haukuwa mwepesi kama makada wa Chadema walivyodhani.Mathalani katika kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora mchakato huo ulilazimika kurudiwa duru ya pili baada ya wagombea kutofikisha asilimia 50.

Lakini katika uchaguzi huo wagombea walipishana kati ya kura moja au mbili, hali iliyotafsiriwa kuwa mchuano ulikuwa mkali tofauti na chaguzi zilizopita za kanda hasa zile zilizofanyika mwaka 2019.

Wadadisi wa mambo wanasema matokeo chaguzi za kanda hizo umeleta sura mpya za wajumbe wa kamati kuu ya Chadema huku kati ya wagombea watatu waliokuwa wakitetea nafasi zao, mmoja alifanikiwa kupenya ambaye ni Ezekia Wenje wa Kanda ya Victoria.

Katika uchaguzi wa Nyasa, Sugu amemshinda Msigwa kwa tofauti ya kura mbili, wakati Lucas Ngoto Kanda ya Serengeti amembwaga mshindani wake, Gimbi Masaba kwa tofauti ya kura moja.

Kivumbi na jasho kilikuwa kanda ya Magharibi ambako mchakato huo ulirudiwa mara mbili baada ya wagombea Dickson Matata, Martine Mussa, Gaston Garubindi na Ngassa Mboje kushindwa kufikisha asilimia zinazotakiwa.

Duru ya pili ilikuwa Ngasa ambaye alipata kura 32 sawa na asilimia 38, Matata 26 sawa asilimia 32, Garubindi 21 sawa asilimia 25 na Martine kura nne sawa na asilimia 5.

Ndipo uchaguzi ukaamuliwa mawakili Matata na Mboje wachuane wawili huku wengine wakitemwa. Ndipo Matata alipompiku Mboje kwa kura 46 sawa na asilimia 56 dhidi 35 sawa na asilimia 43.3

Related Posts