HONGERA sana Azam FC kwa kujihakikishia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiungana na Yanga iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika.
Nimeamua kuwapongeza Azam kwa vile wana muda mrefu sana ambao wamekaa bila kushiriki mashindano hayo makubwa kwa klabu hapa Afrika.
Kiufupi jamaa wameipambania hasa nafasi hiyo ya kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa na wamestahili kuipata, tuwape haki yao tu japo ni wanyonge kihistoria kwenye soka la nchi yetu.
Sasa baada ya Azam kufanikisha hilo, kuna watu wameanza kuibeza timu hiyo wakidai katika Ligi ya Mabingwa Afrika itaishia kuwa msindikizaji tu kwa vile imekuwa haifui dafu kwenye mashindano ya klabu Afrika kwa kutazama kumbukumbu ya nyakati tofauti ilizowahi kushiriki.
Nadhani haipaswi kuwa hivyo, ni mapema sana kuhisi Azam itakwama tena kwani ukiangalia mipango yake inaonekana ina nia ya dhati ya kuhakikisha safari hii haiwi mnyonge na inafuta historia mbaya iliyoweka miaka ya nyuma.
Mfano wa hilo tunaweza kuuona katika usajili ambao inaendelea kuufanya kwa kusajili mapema wachezaji wa kigeni ambao sio wa kuokoteza bali wanatoka katika mataifa makubwa kisoka na wa daraja la juu.
Imechukua watu wawili kutoka Colombia ambao wote walikuwa wakizitumikia timu za Ligi Kuu huko mmoja akiwa kiungo mkabaji na mwingine akiwa wa nafasi ya ushambuliaji ambao wanakwenda kuongeza nguvu katika kikosi chao msimu ujao.
Imenyakua mmoja kutoka Ligi Kuu ya Mali na kwa mujibu wa maelezo ya mabosi wao, wana mpango wa kuongeza wengine wazawa ambao wana ubora wa juu na uzoefu wa kutosha wa mechi za ndani na mashindano ya kimataifa.
Inawezekana zamani ilituangusha lakini kwa namna inavyosuka mipango yake kwa ajili ya msimu ujao, nashawishika kusema Azam itakuwa na nafasi kubwa ya kuwashangaza wale wanaoona inakwenda kushiriki tu.