MSIMU wa 2020/2021, Gwambina FC ya Mwanza ilishuka daraja ikiwa ndio kwanza imeshiriki Ligi Kuu kwa msimu mmoja baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi iliyokuwa na timu 18.
Kulikuwa na matumaini makubwa kwa timu hiyo ambayo maskani yake ilikuwa kule Misungwi, Mwanza angalau ingedumu Ligi Kuu kwa misimu kadhaa lakini ndani ya muda mfupi ikarejea shimoni.
Sababu iliyowafanya wengi wajenge imani kwa Gwambina ingetoboa ni kitendo cha mmiliki wake kujenga uwanja ambao timu hiyo iliutumia kwa mechi zake za nyumbani, pia mpango wa kuwa na timu imara ya vijana ambao iliuandaa.
Hata hivyo, vyote havikuisaidia Gwambina na muda huu unaposoma andiko hili kutoka kijiweni, Gwambina ilishindwa hata kuhimili ligi ya Championship ikashushwa hadi ligi ya mkoa.
Misimu michache baadaye timu nyingine ambayo nayo ilikuwa na uwanja wake tena mzuri tu ya Ihefu nayo ikawasononesha wakazi wa Mbalali ambao tayari walishaanza kuufaidi uhondo wa Ligi Kuu.
Wamiliki wa timu hiyo wakaamua kuiuza timu kwa kibopa mmoja wa serikali ikahamishwa kutoka huko Mbalali, Mbeya na kupelekwa Singida ambako sasa inakaribia kubadilisha jina na itaitwa Singida Black Stars.
Hii inamaanisha wakazi wa Mbalali kwa sasa wanaishia kuutazama Uwanja tu wa Highland Estates lakini Ligi Kuu wanaishia kuitazama kwenye chaneli za Azam TV.
Msimu huu huu ambao Ihefu imewanyima uhondo mashabiki ambao wanatoka maeneo yaliyokuwa yanauzunguka Uwanja wa Highland Estates, timu nyingine yenye uwanja ya Geita Gold nayo imeshuka daraja.
Sio Geita Gold na Mtibwa Sugar inayomiliki uwanja wa Manungu Complex nayo imeangukia ligi ya Championship baada ya kushika mkia kwenye msimamo wa ligi.
Kushuka kwa hizi timu zenye viwanja sio jambo la kufurahia maana tunabakiwa na timu ambazo zinatumia viwanja vya kukodi ambavyo mmiliki akiamua mechi isichezwe timu, TFF na Bodi ya Ligi wanakuwa hawana mamlaka ya kuvitumia.