MACHO hayaamini yanachokiona kwenye ukurasa wa Instagram wa nahodha wa Simba, John Bocco ambaye msimu huu hakuonekana uwanjani kwa muda mrefu kutokana na majeraha.
Ninachokisoma ni anko John Bocco amewaaga rasmi mashabiki wa timu hiyo kuwa anaachana nayo rasmi baada ya mkataba wake kumalizika akiwa ameitumikia kwa miaka saba.
Kwangu, Bocco hajawaaga Simba pekee bali pia ameuaga umma wa mashabiki wa soka hapa nchini ambao kwa muda mrefu wamekuwa na hisia tofauti dhidi yake tangu alipokuwa akiichezea Azam FC.
Wapo ambao walikuwa wakimshangilia pindi mabao yake yalipokuwa na manufaa kwa timu zao lakini kuna wale ambao walikuwa wakimzomea pale alipokosa mabao au alipofunga mabao ambayo yaliumiza upande wanaoushabikia.
Kwenye jezi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ni mara chache sana Bocco alikutana na nyakati nzuri lakini mara nyingi alijikuta akizomewa na kubezwa na Watanzania wenzake ambao ndio walipaswa kumpa sapoti kubwa.
Pamoja na yote, Bocco alisimama imara na kutotoka mchezoni akajikita katika kutimiza wajibu na majukumu yake kama mchezaji wa kulipwa hali iliyosababisha aendelee kuwa tegemeo kwa timu alizochezea.
Silaha kubwa ya Bocco ambayo imechangia mafanikio yake ni nidhamu ya hali ya juu, pia kumheshimu kila mmoja ndani na nje ya timu jambo lililomfanya ageuke kuwa kipenzi kwa wachezaji wenzake na ndio maana haikushangaza kuona akiwa nahodha kwenye hizo timu.
Ndani ya uwanja amekuwa tishio kwa makipa kiasi cha kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Azam FC, pia ndiye mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara akmpiku Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.
Baada ya kufanikiwa kama mchezaji kuna dalili kubwa akaja kufanikiwa kama kocha maana hiyo timu ya vijana ya Simba chini ya umri wa miaka 17 ambayo yeye ndio anaifundisha, inaupiga mwingi huko kwenye Ligi ya TFF.
Heshima ya Bocco kwenye soka la Tanzania ni kubwa sana hivyo jambo la pekee ni kumwambia asante na kumpa kila la kheri kwa atakachokiamua kama kuwa kocha au kuendelea kucheza.