UBORA wa viwanja una nafasi kubwa ya kuzalisha ligi, wachezaji na timu bora na ni jambo lililo wazi hakuna nchi yoyote iliyopiga hatua kisoka ambayo haina viwanja.
Katika kuonyesha umuhimu wa uwanja katika mchezo wa soka, umewekwa kama sheria namba moja kati ya 17 za soka na hakujawahi kuwa na mabadiliko yaliyowahi kuifanya iwe tofauti na hivyo.
Kwa kulinda ubora na hadhi za viwanja ili mchezo wa soka uchezwe katika mazingira yatakayokuwa salama kwa timu na wachezaji, mamlaka za soka duniani zimeweka miongozo ya kufuatwa katika umiliki, matunzo na usimamizi wa viwanja ambayo wadau wa mchezo huo wanawajibika nayo.
Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limeweka miongozo miwili ambayo nchi wanachama wake wanapaswa kuifuata ili kuhakikisha bara hili linakuwa na viwanja vyenye hadhi na ubora na hivyo kutekeleza matakwa ya sheria ya kwanza ya mchezo huo.
Mosi ni muongozo wa utoaji wa leseni kwa klabu za soka wa Caf na pili ni muongozo wa Caf wa viwanja wa soka.
Kanuni ya 30 ibara ya kwanza ya muongozo wa Caf wa usajili wa klabu umelazimisha klabu kuwa na viwanja ili zipate uhalali wa kushiriki mashindano ya klabu ya shirikisho hilo.
“Muomba leseni anapaswa kuwa na uwanja unaowezesha kuandaa mechi za mashindano ambayo timu yake itashiriki. Miongoni mwa mahitaji yafuatayo ni lazima yatekelezwe.
“Muomba maombi awe ni mmiliki kisheria wa uwanja na atacheza mechi zote za nyumbani kwenye uwanja huo katika kipindi chote cha leseni yake.
“Au muomba maombi ya leseni aambatanishe mkataba wa makubaliano na mmiliki wa uwanja atakaoutumia. Mkataba huo lazima uthibitishe uwezekano wa kutumika kwa uwanja katika kipindi chote cha leseni,” inafafanua ibara hiyo.
Ibara ya pili ya kanuni hiyo ya mongozo wa utoaji leseni za klabu wa Caf inalazimisha uwanja kutimiza mahitaji matatu ya msingi ili uweze kutumika na muomba leseni.
Mahitaji hayo ni kukidhi muongozo wa Caf wa viwanja, kanuni za mashindano za Caf na maamuzi mengine ya shirikisho hilo.
Muongozo wa viwanja wa Caf umetoa vigezo kadhaa vinavyopaswa kutimizwa ili uwanja uweze kutumika kwa mechi za mashindano mbalimbali, muongozo ambao ndio unatumika hapa nchini katika kuamua viwanja gani vitumike au visitumike kwa mechi za ligi yetu na mashindano mengine mtawalia.
Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti katika viwanja mbalimbali nchini umebaini viwanja vingi havina sifa ya kutumika kwa mechi za ligi kuu kwa wanaume na wanawake kutokana na kutotimiza mahitaji mengi ya muongozo wa viwanja wa Caf.
Hadi sasa, viwanja vinavyokidhi vigezo vya muongozo wa viwanja wa Caf ili kutumika kwa mechi za ligi nchini ni viwili ambavyo ni Benjamin Mkapa na Azam Complex ambavyo vyote vipo Dar es Salaam. Lakini swali la kujiuliza kwa nini vingine vinatumika?
Kwa mujibu wa muongozo wa viwanja wa Caf, kuna makundi manne ya viwanja ambayo ni A, B, C na D. A ni vile vyenye hadhi ya nyota tano na D ndivyo vyenye hadhi ya chini ambavyo vinaweza kutumika kulingana na mahitaji husika.
Viwanja vya kundi D vinapaswa kutimiza vigezo 17 na kwa hapa Tanzania ni Benjamin Mkapa na Azam Complex pekee vinavyokidhi.
Vigezo hivyo 17 ni eneo la kuchezea kuwa lililosawazishwa na kuwa na usawa, urefu wa nyasi milimita 20 hadi 30, eneo la kuchezea kuwa na mfumo wa kusambaza maji wa sprinkle, eneo la wachezaji wa akiba kupasha misuli nyuma ya mabango ya matangazo na eneo la kupasha liwe na upana wa 3mx30m.
Vingine ni magoli ya ziada, benchi la wachezaji wa akiba linalotosheleza watu wasiopungua 14 wakiwa wamekaa, friji na meza ya masaji.
Ukiondoa hivyo pia kunahitajika maji moto na baridi chumba cha huduma ya kwanza na matibabu, kifaa cha kuamsha mapigo ya moyo, kipima joto cha kidigiti, mashine ya kutolea fotokopi na skana, angalau siti za kukaa mashabiki 5,000, chumba chenye angalau viti 15 kwa ajili ya mkutano wa waandishi wa habari na kwa ajili ya usalama wa wachezaji na mashabiki.
Kukosekana kwa eneo bora la kuchezea linaonekana kukabili viwanja vingi vinavyotumika kwa mechi za ligi kuu na mashindano mengine ingawa vipo baadhi ambavyo havina changamoto hiyo.
Kutokana na kuwa na nyasi bandia, viwanja vya Azam Complex, Majaliwa (Lindi) na Kaitaba uliopo Kagera, vimeonyesha kukidhi mahitaji ya kutumika kwa mujibu wa muongozo wa viwanja wa Caf kama vilivyo vile vya Benjamin Mkapa, Mkwakwani (Tanga) na Highland Estates (Mbeya) ambavyo vina nyasi za asili.
Viwanja hivyo tajwa vyenye nyasi asili vinaonekana kukidhi vigezo kutokana na nyasi zake kukatwa vizuri kwa angalau kimo kinachohitajika, pia kuwa na msawazisho ambao unaruhusu mpira kutembea vizuri.
Viwanja vingine vilivyo salia kwenye eneo la kuchezea havitimizi muongozo na vinatumika kama huruma tu kutokana na uhaba wa changamoto ya viwanja nchini.
Baadhi maeneo ya kuchezea hayako katika msawazisho mzuri unaoweza kufanya mpira utembee vyema, havina uwezo wa kuondoa kwa haraka maji pindi mvua inaponyesha na baadhi vina vipara kwenye baadhi ya maeneo.
Mkandarasi wa Uwanja wa Azam Complex, Victor Ndozero anafichua sababu za uwanja huo kutotunza maji na kuwa na ubora wa eneo la kuchezea.
“Nyasi bandia za Uwanja wa Azam Complex ni za kizazi cha tano ambazo ndio za kisasa zaidi na zimewekwa katika namna ambayo hauwezi kutunza maji hata mvua inyeshe kiasi gani. Chini kuna mfumo mzuri wa utoaji maji uwanjani ambao umewekwa kulinganisha na viwanja vingine,” alisema Ndozero.
Uwezo duni wa viwanja katika kuondoa maji pindi mvua inaponyesha ulijidhihirisha katika mchzo wa ligi kuu baina ya JKT Tanzania na Yanga ambao siku ya kwanza uliopangwa kufanyika Aprili 23 haukuchezeka kutokana na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kuamriwa kuchezwa kesho yake kutokana na uwanja huo kujaa maji yaliyotokana na mvua iliyokuwa ikinyesha mfululizo katika maeneo tofauti nchini.
“Mchezo wa @ligikuu ya @nbc_tanzania kati ya @jkt_tanzania_fc na @yangasc uliokuwa uchezwe leo kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, umeahirishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 39:13 ya Ligi Kuu kuhusu Mwamuzi na Bodi itatoa taarifa ya ratiba ya mchezo huo,” ilifafanua taarifa ya bodi ya ligi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini mbali na suala la ubora wa eneo la kuchezea, viwanja vingi havikidhi mahitaji mengine ya msingi yaliyoorodheshwa kwenye muongozo wa viwanja wa Caf.
Ni viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex ambavyo vinatimiza vigezo vingine 16 vya muongozo wa viwanja na vilivyobakia ambavyo ni Meja Jenerali Isamuhyo, Sokoine, Liti, Highland Estates, Jamhuri Dodoma, Jamhuri Morogoro, Manungu, Majaliwa, CCM Kirumba, Mkwakwani, Ali Hassan Mwinyi, Kaitaba, Lake Tanganyika na Kambarage, vinaonekana kutimiza tu mahitaji machache kati ya hayo 16 na utimizaji huo ni wa kutofautiana.
Kigezo cha kuwa na siti ambazo angalau watu 5,000 wanaweza kuketi wakiwa wanatazama mpira kinaonekana kutotimizwa na viwanja vya Manungu na Meja Jenerali Isamuhyo.
Ofisa habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru aliliambia Mwanaspoti mpango uliopo ni kuongeza majukwaa katika Uwanja wa Manungu Complex ingawa sio jambo litakalofanyika kwa haraka.
“Mtibwa Sugar ni timu yenye malengo makubwa na miongoni mwa mpango uliopo ni kufanya muendelezo wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wetu wa Manungu Complex kwa kuongeza majukwaa ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kujitokeza katika mechi zetu,” alisema Kifaru.
Katika viwanja vya CCM Kirumba, Sokoine, Lake Tanganyika, Mkwakwani, Liti, Jamhuri Dodoma, Kambarage, Mwadui Complex, Ali Hassan Mwinyi, Kaitaba na Mkwakwani, hakuna mabenchi ambayo watu 14 au zaidi wanaweza kukaa wakati mchezo ukiwa unaendelea na hivyo kufanya wachezaji kukaa chini au kuwekwa viti vya kawaida vya muda hasa pale kunapokuwa na mechi dhidi ya timu kubwa.
Ni viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex pekee ambavyo vina friji, mashine ya fotokopi na skana, mashine ya kushtua mapigo ya moyo, chumba cha wanahabari chenye viti vinavyoweza kukaliwa na waandishi angalau 15.
Mtendaji mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema kuwa nia ya kuufanya Uwanja wao wa Azam Complex kufikia vigezo vya kimataifa ndio imepelekea uwe na sifa zinazokidhi vigezo vinavyohitajika kwa mujibu wa muongozo wa viwanja wa Caf.
“Kila wakati tumekuwa tukiboresha uwanja wetu kwa mujibu wa maelekezo ya Fifa, Caf na TFF na hilo ndilo limechangia Azam Complex kuwa kimbilio kwa timu za ndani na nje ya Tanzania pindi zinapokuwa na mechi za mashindano mbalimbali.
“Uwekezaji kwenye uwanja unahitaji gharama kubwa ya fedha hivyo naushukuru uongozi wa Azam FC kwa mchango mkubwa wa fedha ambao umekuwa ukitoa katika kuhakikisha ukarabati na matunzo ya mara kwa mara yanafanyika kwenye Uwanja wetu ili uendelee kuwa bora zaidi,” alisema Popat.
Popat alisema timu hiyo ina malengo ya kujenga uwanja mkubwa zaidi.
Adhabu ya kufungiwa viwanja kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni inaonekana kugusa zaidi viwanja ambavyo havina eneo zuri la kuchezea ama vile ambavyo havina mazingira wezeshi kwa kituo cha luninga chenye haki ya kuonyesha maudhui ya ligi kuu lakini kiuhalisia viwanja vingi vinapaswa kufungiwa kwa kukosa vigezo vingine muhumi kama vilivyotajwa katika muongozo wa viwanja wa Caf.
Hadi sasa, viwanja sita tu tu kati ya 16 vilivyoonja adhabu ya kufungiwa na bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB) ambavyo ni Jamhuri Morogo, Kambarage Shinyanga, Ali Hassan Mwinyi Tabora, Liti Singida, Highland Estates Mbeya na Uhuru Dar es Salaam.
Uwanja Uhuru ulifungiwa kwa kutokuwa na eneo zuri la kuchezea na kutotoa mazingira mazuri kwa warushaji picha za matangazo ya luninga kama ilivyokuwa kwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro, lakini vilivyobakia vinne ambavyo ni Liti, Kambarage, Ali Hassan Mwinyi na Highland Estates.
Akizungumzia suala la ubora wa viwanja, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa kuanzia msimu ujao watakuwa wakali kwa viwanja ambavyo havitokidhi mahitaji ya kikanuni na muongozo ambao umewekwa ili kukuza ubora na thamani ya ligi.
“Tutakuwa wakali zaidi kuhusu miundombinu ya viwanja. Tumetoa muda mrefu sana. Kuna vitu tunaongeza, tunakuza hadhi ya viwanja vyetu. Kwa hiyo msije mkashangaa kwamba tumehamasisha watu wajenge viwanja vyao lakini basi sio kiwanja tu kuna vitu vingi na tumewaachia.
Wale ambao tumewaachia wana miaka mingi wamebakia palepale hawajaenda zaidi tunaweza kuwaweka pembeni.
Kwamba hivi viwanja hapana kwa sababu tumewaruhusu labda tumewapa moyo lakini kuwaruhusu wamebweteka wamesimama palepale.
Kwa hiyo hilo nilizungumze tu kama rais wa shirikisho, kamati zangu nimezipa maelekezo kwamba kidogo waongeze hadhi.
Sasa hivi sisi sio Tanzania ile tuliyokuwa tunaifikiria ni Tanzania ya mpira ambao unaangaliwa na dunia nzima hivyo hatuwezi kufanya majaribio ambayo yanaweza kututia madoa,” alisema Karia.
Mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Almas Kasongo alisema kuwa changamoto za viwanja zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha vinakuwa na ubora zaidi siku za usoni.
“Kama mnavyoona msimu huu hakujawa na malalamiko mengi kuhusu viwanja hivyo baada ya msimu kumalizika tutafanya tathmini na pale penye mapungufu tutahakikisha tunafanya marekebisho kwa kiasi kikubwa ili kuimarisha zaidi ligi yetu.
“Suala la viwanja ni miongoni mwa yale ambayo bodi ya ligi iko makini nayo na inafuatilia kwa karibu ili kama kuna changamoto zifanyiwe kazi kwani lengo ni kuboresha zaidi na kukuza thamani ya ligi yetu,” alisema Kasongo.