Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imeonyesha maambukizi mapya kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 mpaka 24 yameongezeka mara mbili zaidi, huku sababu ikitajwa kuchangiwa na kukua kwa teknolojia.
Mawasiliano hasa ya njia ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii yametajwa kuwa kichocheo cha ongezeko hilo, huku rika la wanaume wa kati ya miaka 30 hadi 60 wakitajwa kuwa chanzo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Jerome Kamwela, ripoti hiyo mpya imeonyesha maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2016/2017 mpaka 30 mwaka 2022/2023.
“Maambukizi mapya katika kipindi hicho yamepungua kutoka 72,000 mpaka 60,000, lakini kwa wasichana wa kati ya miaka 15 mpaka 24 yameongezeka mara mbili, hili jamii inapaswa kuliangalia kwa makini na kuchukua hatua,” anatoa angalizo Dk Kamwela na kuongeza:
“Wavulana maambukizi yamepungua lakini bado wapo kwenye hatari. Maendeleo ya teknolojia yanachangia, wazazi wanapaswa kuwa makini, kabla hujampa binti au kijana wako simu, fikiria nini ataangalia huko na hatujui wanasikiliza nini.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kituo cha Taaluma za Mawasiliano, Benedicto Luvanda anasema maambukizi yameongezeka kati ya vijana walio kwenye balehe, lakini miongoni mwao kwa wasichana yanaonekana yako juu zaidi ukilinganisha na wenzao wa kiume.
“Wasichana wadogo kama wanavyowaita watoto wa 2000 wanavutia wanaume wengi na kwa sababu ya umri wao wanashindwa kuhimili presha za kuingia kwenye mahusiano, hivyo ni rahisi kuwa na wapenzi wengi,” anasema.
Anasema kukua kwa teknolojia kunachangia ongezeka la kasi, maana nyakati za nyuma ilimlazimu mtu kutafuta nafasi ya kukutana moja kwa moja na msichana na kumuongelesha, kwa hiyo labda isingekuwa rahisi.
“Teknolojia imerahisisha. Inawezekana mzazi ukamfungia mtoto wako ndani, lakini kama anaweza kuwa na simu, anaweza pia kuingia kwenye mitandao ya kijamii. Kwa hiyo kwa sasa mtu akimtaka mtu anaomba tu namba na wanasema ukifanikiwa kupata namba tu hiyo stori imeisha, unakuwa na nafasi pana ya kumshawishi huyo mtu kuingia kwenye mtego wako,” anasema.
Luvanda anasema matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la vyombo vya habari watu hujifunza tamaduni tofauti, hivyo watoto wengi wanaanza kutamani kuishi maisha ya wengine.
“Huenda watoto wadogo wanaingia kwenye mahusiano na watu wazima, maana kuna uwezekano wa kuwapa kitu kitakachowafanya waishi vile wanavyotamani, kuliko kuwa na mtu wa umri wao. Pia tabia zilizokuwa si kawaida sasa ni kawaida, kama kuwa na wapenzi wengi, wanajifunza mitandaoni.”
“Wengine wanaangalia picha za ngono wanapata mihemko na wanaona kuna namna wanaweza kufanya, kitu ambacho zamani hakikuwepo.”
Luvanda anasema maendeleo yamefanya wazazi kuwa bize na mambo mengine na kukosa muda wa kuwaangalia watoto, wameacha majukumu muhimu na hii imesababisha mashindano kati ya maarifa waliyonayo wazazi na yale ambayo watoto wao tayari wanayo.
Anasema kuna sababu nyingi, akitaja mojawapo kuanza ngono mapema na kujiweka kwenye hatari kwa kuongeza uwezekano wa kuwa na wenzi wengi kwenye maisha na kuwa hatarini kupata maambukizi.
Luvanda anasema msichana anaweza kuwa na akili akawakwepa wanaume wawili au watatu, lakini akanasa kwa mwingine na baadaye anajikuta kwenye mahusiano na wanaume wengi.
“Takwimu hizi zinaashiria wengi wana mahusiano na waliowazidi umri, kama wangekuwa na mahusiano na watu wa umri wao labda maambukizi ya VVU yasingekuwa makubwa pia, maana kwa watoto wa kiume wa umri huu maambukizi yapo kidogo,” anasema na kuongeza;
“Kama watoto wa kike kwenye huu umri wana kiwango kikubwa cha maambukizi, inatuambia kwamba wana mahusiano na watu wengine ambao hawapo kwenye umri wao…
“Unajua ni rahisi mtoto wa kike kukwepa kufanya ngono na mtoto wa rika lake, lakini anapokuja mtu mzima ushawishi unakuwa mkubwa zaidi, anashindwa kukwepa pale anapojiingiza kwenye uhusiano na mtu mkubwa.”
Luvanda anasema hata katika matumizi ya kondomu watu wazima hujiachia wakiamini wale wasichana wapo salama, wakisahau kuwakinga, kwani wao wameshakuwa na wapenzi wengi, hata wasichana huamini watu wazima wapo salama.
Anataja sababu nyingine kuwa ya kibaolojia: “Msichana yuko upande wa kupokea, kama ana mahusiano na mtu mwenye VVU ambaye hatumii dawa, uwezekano wa kupata maambukizi ni mkubwa sana kwa sababu za kimaumbile.”
Wakati takwimu hizo zikitajwa, wasichana wao wanasema ugumu wa maisha na kutokuwa karibu na wazazi kunachangia kuingia katika mahusiano wasiyoyatarajia.
Aneth, mwenye miaka 19 anasema alijikuta katika mahusiano na mwanamume mwenye zaidi ya miaka 40 kupitia rafiki yake.
“Aliniomba nimsindikize mahali, nilifanya hivyo na huko alienda onana na mtu wake. Huyo mwanaume alikuwa na wenzake, mmoja akaanza kutaka kuzungumza na mimi kupitia simu ya rafiki yangu, awali sikupenda.
“Siku mbili baadaye alipiga simu na rafiki yangu akitaka nikamsikilize hata kama sitakubaliana naye. Kufika huko aliacha kunitongoza akanipa simu janja ya gharama, akasema ameona ni vema niwe nayo. Alinipa Sh100,000 kama fedha za vocha akaondoka, baada ya wiki chache nilijikuta nimekubali ombi lake,” anasema.
Mapito haya ya mahusiano na watu waliowazidi umri, yanafanana na yale ya Anjela (si jina halisi) mwenye miaka 21 ambaye tayari ana maambukizi ya VVU.
“Nilijihusisha kimapenzi na mmoja wa wahadhiri wangu nikiwa mwaka wa kwanza. Baadaye nikiwa mwaka wa tatu nilijihusisha na mwingine, sijui nani kati yao alinipa maambukizi, lakini wasiwasi wangu kwa mmojawapo ambaye alitaka nifanye hivyo ili kuongeza ufaulu na nilifahamu fika alifanya kwa wengine pale chuoni,” anasema, akikiri kuwa mahusiano yao yalianzishwa kupitia simu ya mkononi.
Wakati changamoto hiyo ikitajwa, wazazi wanasema si rahisi kumweleza mtoto kuhusu masuala ya afya ya uzazi na namna ya kujikinga.
“Unajua unaweza kumwambia mtoto wako kuwa usifanye kitu fulani, kumbe yeye alishafanya muda mrefu na alishakuwa mtaalamu, anajua kila kitu kuliko vile unavyomwambia na huwezi kuwadanganya kwa kuwa maarifa yetu yalijengwa kwenye uongo na vitisho, lakini watoto wa sasa hivi wanajua hili ni kweli na hili siyo kweli,” anasema Othman Musa, mkazi wa Dar es Salaam.
Mkazi wa Morogoro, Linda Shayo anasema katika dunia ya utandawazi ni ngumu kumchunga mtoto.
“Watoto wangu nimewafanya kuwa marafiki, wananieleza changamoto zao nyingi na niliwaambia wasichana lazima wanipe mahitaji yao na kile wanachotamani. Najitahidi kumudu gharama, bila hivyo watadanganyika,” anasema Linda.
Anaongeza kuwa bahati mbaya wazazi hawawezi kusema ukweli kama ambavyo mtu anaweza kuuona kwenye mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. “Naona wazazi tusipokuwa makini hizi changamoto zitakuwa ni kubwa zaidi baadaye.”
Mapema wiki hii, Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es Salaam, ASP David Mwakinyuke aliwataka wazazi nchini kuacha kuwaogopa watoto wao na badala yake wanapaswa kuwafanya marafiki ili wafahamu kila changamoto inayowakabili.
“Nawaomba sana tuache kuwaogopa watoto kwa sababu wajomba au ndugu zako hawamuogopi mwanao na dunia ya sasa inahitaji tuwaambie watoto hii nyeusi na hii nyeupe ukiendelea kumuogopa utakuja naye pale kwetu (Kituo cha Polisi), usimuogope, ongea naye sema naye ili afahamu yaliyopo duniani,” alisema Mwakinyuke.
Maambukizi kwa kundi rika balehe yanapoongezeka, wasichana na wazazi hawajui iwapo wanaweza kuwashitaki wale waliowaambukiza watoto wao kwa makusudi.
Mkuu wa kitengo cha sheria Tacaids, Davis Misingo anasema mtu yeyote anayefanya mapenzi na msichana aliye chini ya umri wa miaka 18 amembaka, kwa sababu ili mapenzi yaweze kufanyika lazima kuwe na utambuzi wa kile kinachofanyika na utambuzi huo anayeweza kuufanya ni mwenye miaka 18 kwenda juu.
Hata hivyo, anasema Sheria Ukimwi na. 28 ya mwaka 2008 na marekebisho ya sheria ya Ukimwi na.14 ya mwaka 2019 inaeleza kuwa ni kosa kumwambukizi mtu VVU kwa makusudi.
“Kwa hiyo nafasi ya wao kuweza kushtaki bado ipo pale pale, kwa sababu jinai haifi, kwanza walifanyiwa vitendo vya kikatili kwa maana ya kubakwa, pili waliambukizwa kwa makusudi. Kama watathibitisha kwa ushahidi kwamba waliambukizwa kwa makusudi bado wana nafasi ya kushitaki,” anasema Misingo.
Akielezea dondoo kuhusu malezi na matunzo ya watoto na familia, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Makundi Maalumu, Sebastian Kitiku anasema wazazi wanapaswa kutambua kuwa watoto wanakabiliwa na aina nyingine ya ukatili mitandaoni.
Anasema utafiti unaonesha watoto 67 katika 100 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wanatumia bidhaa za mawasiliano, ikiwa pamoja na simu janja, kompyuta janja na runinga janja zenye intaneti na wanne kati ya 100 walifanyiwa ukatili, ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya ngono.
“Wanne kati yao walilazimishwa kujihusisha na vitendo vya ngono, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao na kurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi nyingine,” anasema.
Kitiku anasema simu na vifaa vingine vya kielektroniki wanavyotumia watoto hupatiwa na wazazi, ndugu wa karibu bila kujua madhara wanayokumbana nayo watoto bila kusimamiwa matumizi yake.
Anasema wazazi wanapaswa kuwaepusha watoto kwenda kwenye maeneo hatarishi kwa usalama wake akiwa peke yake, kwa kuwa anaweza kufanyiwa vitendo visivyofaa.
“Mzazi hakikisha mtoto hatumii vifaa vya kielektroniki kama simu, intaneti na luninga bila uangalizi wa karibu ili kumwepusha kujiingiza kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili wa mtandaoni.
Kitiku anasema ni vema kumwelekeza mtoto kutimiza wajibu wake, kuheshimu na kupokea maelekezo ya wazazi au walezi na walimu, kwani ndio msingi wa utii, uadilifu na uzalendo ili kujenga misingi imara ya ustawi na maendeleo yake.