KUNA usajili wa kushtua unaoweza kujitokeza kwenye dirisha lijalo la usajili wa Ligi Kuu Bara. Jean Baleke kwenda Yanga.
Mkongomani huyo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al-Ittihad ya Libya, aling’ara na Simba na kutema kwenye dirisha dogo huku mashabiki wakijiuliza bado ni nini kimetokea.
Endapo kama dili la Baleke likiti, basi straika wao Joseph Guede huenda akapewa mkono wa kwaheri au kutolewa kwa mkopo.
Guede msimu uliomalizika na mabao sita, alijiunga na Yanga kwa usajili wa dirisha dogo, akitokea klabu Tuzlaspor ya Uturuki, mwanzo wake haukuwa mzuri ingawa alimaliza kwa kishindo, pamoja na hilo viongozi wa klabu hiyo, wanaonekana wana imani ndogo naye na huenda wakacheza karata ngumu kwenye dirisha hili lakini itategemea na upatikanaji wa Baleke.
Kiongozi huyo wa Yanga alizungumza na Baleke kwa muda mrefu lakini inadaiwa kwamba mchezaji huyo bado anasita kufanya maamuzi kutokana na uswahiba wake na watu wa Simba ingawa kiuhalisia amemuweka wazi kwamba hataki kuendelea kubaki Libya kwani hajapenda mazingira yalivyo na hali ya usalama.
Rafiki wa karibu na Baleke, aliliambia Mwanaspoti kwamba kigogo huyo wa Yanga amekuwa akimpigia simu mchezaji huyo kwa nyakati tofauti, tangu akiwa Simba na baada ya kuondoka na amemuahidi donge nono akija Jangwani.
Inaelezwa pamoja na Baleke kutoonyesha uharaka wa kuikubali ofa ya Yanga, zipo timu nyingine ambazo zinahitaji huduma yake na huenda msimu unaokuja asiwepo kwenye timu anayoitumikia kwa sasa.
Baleke alijiunga Simba kwa usajili wa dirisha dogo, msimu wa 2021/22 alimaliza na mabao manane na 2022/23 pia alimaliza na mabao manane, nje na Yanga timu nyingine anayohusishwa nayo ni Ihefu.