2023/24 ulikuwa msimu wa rekodi

LIGI Kuu Tanzania Bara ilimalizika wiki hii kwa aina yake huku rekodi kibao zikiwekwa kwenye maeneo mbalimbali. Makocha na wachezaji walikiri ulikuwa ni msimu wenye ushindani zaidi uwanjani, viongozi wakakazia ilikuwa ni ligi ngumu na wenye mamlaka ya soka nchini wakakubali mchezo huo kukua kwa kasi.

Licha ya furaha kwa Yanga na Azam zilizomaliza nafasi mbili za juu, kilio kwa Mtibwa Sugar na Geita Gold zilizoshuka daraja, Majonzi kwa Simba kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na vifijo kwa Coastal Union iliyorejea kwenye michuano ya CAF, kuna rekodi nyingine kibao zimewekwa.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya rekodi adimu ambazo zimejitokeza msimu uliopita ambazo kwa namna moja au nyingine zinashangaza, kufurahisha na kuhuzunisha wana michezo. Shuka nazo…

AZIZ KI AFIKIA REKODI YA TAMBWE

Nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI ameibuka mfungaji bora msimu huu baada ya kufikisha jumla ya mabao 21 na kumpiku aliyekuwa mshindani wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC aliyeshika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 19.

Msimu huu ulikuwa bora zaidi kwa viungo washambualiji kwa sababu licha ya Aziz Ki kufunga idadi hiyo ya mabao, ila amefikia rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21 msimu wa 2015/2016.

SIMBA YAACHANA NA KIPA ‘PRE SEASONS’

Simba ilimsajili kipa, Mbrazil Jefferson Luis kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo hilo ila jambo la kushangaza nyota huyo hakuichezea timu hiyo baada ya kutemwa wakati kikosi hicho kikiwa katika maandalizi ya msimu (pre seasons) huko Uturuki.

Jefferson aliyejiunga na Simba Julai 23, mwaka jana na kupewa mkataba wa miaka miwili, aliachwa kutokana na kugundulika kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara hivyo kuvunjiwa mkataba na kurudi kwao na kujiunga na kikosi cha Athletic Club.

REKODI YAJIRUDIA YA 2015-2016

Katika Ligi ya msimu huu iliyomalizika tumeshuhudia rekodi ya msimu wa 2015-2016 ikijirudia tena na Simba imemaliza nafasi ya tatu na pointi 66 sambamba na Azam FC iliyomaliza ya pili ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika msimu huo, Yanga ilikuwa bingwa kama ilivyokuwa pia msimu huu ikiwa na pointi 73 baada ya kucheza michezo 30 huku Azam FC ikimaliza ya pili na pointi 64, wakati Simba ilishika ya tatu na pointi 62 jambo ambalo limejirudia tena kwa msimu huu kwa maana ya nafasi kwenye msimamo.

Nyota wa Coastal Union, Mkongomani Ley Matampi ameibuka mmoja wa makipa bora msimu huu baada ya kufikisha ‘Clean Sheets’ 15 na kumpiku, Djigui Diarra wa Yanga aliyekuwa na 14 aliyebeba tuzo hiyo kwa misimu miwili mfululizo iliyopita.

Matampi aliyejiunga na Coastal msimu huu akitokea klabu ya Jeunesse sportive Groupe Bazano ni kipa mwenye wasifu mkubwa na uzoefu katika soka la Afrika akiwa na medali ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika alioupata na TP Mazembe mwaka 2017.

Medali hiyo aliipata baada ya Mazembe kuwaondosha Supersports United ya Afrika Kusini kwenye fainali kwa jumla ya mabao 2-1.

Fainali ya kwanza ilipigwa Afrika Kusini na kumalizika kwa suluhu na Matampi hakucheza mchezo huo ila marudiano huko Congo alianza na kuipa ushindi wa mabao 2-1 huku akipita klabu mbalimbali kama DC Motema Pembe na Kabuscorp ya Angola.

KITUKO CHA WACHEZAJI SITA

Katika hali ya kawaida, timu ya Tabora United iliingia na wachezaji wanane tu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, uliopigwa Agosti 16, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex na kumalizika kwa wenyeji kushinda kwa mabao 4-0.

Sababu ya Tabora kuanza na wachezaji wanane ni kutokana na baadhi ya wengine kutokamilishiwa vibali vyao vya kufanyia kazi nchini na walipoumia wawili na kubakia sita, mechi ilimalizika dakika ya 18 tu kutokana na kanuni kutoruhusu mchezo kuchezwa kama wachezaji ni pungufu ya saba.

Coastal Union imekata tiketi ya kuiwakilisha nchi msimu ujao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu baada ya kumaliza nafasi ya nne katika msimamo na pointi 43 kufuatia kushinda michezo 11, sare 10 na kupoteza tisa.

Coastal inayonolewa na Mkenya, David Ouma imefuzu kwa mara ya kwanza tangu iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika mwaka 1989 na kuishia raundi ya kwanza kabla ya kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika 2004. Ilikaaa miaka 35 bila kucheza michuano ya CAF.

MTIBWA YASHUKA BAADA YA MIAKA 28

Mtibwa Sugar ambayo ni iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi mara mbili mfululizo msimu wa 1999 na 2000, imeshuka rasmi daraja ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 28 tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1988 na kupanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) 1996.

Msimu huu timu hiyo imeshinda michezo mitano tu kati ya 30, sare sita na kupoteza 19, ikiwa mkiani mwa msimamo na pointi 21.

Msimu huu ni timu tano tu kati ya 16 zilizomaliza na makocha walioanza nao msimu ambazo ni Yanga (Miguel Gamondi), Azam FC (Youssouph Dabo), KMC (Abdihamid Moallin), Mashujaa (Abdallah Mohamed ‘Baresi’ na Malale Hamsini wa (JKT Tanzania).

Singida Fountain Gate ndio timu inayoongoza kwa kufukuza makocha ambapo ilianza na Mholanzi, Hans Van de Pluijm, akaja Mjerumani, Ernst Middendorp, akafuata Mbrazili, Ricardo Ferreira aliyetimuliwa kisha akatua Msauzi, Thabo Senong.

Baada ya hapo Msauzi huyo aliondolewa pia kutokana na matokeo mabovu na timu hiyo ikamtangaza Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuchukua mikoba ingawa hakudumu kwani aliondoka na kikosi hicho kufundishwa na Ngawina Ngawina aliyemaliza nacho msimu.

Timu nyingine ni Ihefu iliyonolewa na makocha watatu tofauti na alianza Zubery Katwila kisha akatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mganda, Moses Basena ambaye pia hakudumu kwani aliondoshwa na kikosi hicho kumalizia msimu na Mecky Maxime.

Namungo ilianza msimu na Mrundi, Cedric Kaze aliyeondoka mwanzoni baada ya matokeo mabaya na kukabidhiwa aliyekuwa kocha msaidizi, Denis Kitambi ambaye alisepa na mikoba kukabidhiwa Mkongomani, Mwinyi Zahera.

Kikosi kingine kinachofuata kwa kutimua makocha wengi ni Tabora United ambayo ilianza msimu na Mserbia, Goran Kopunovic ila aliondoka na kukabidhiwa Mfaransa, Denis Laurent Goavec ambaye hakudumu na nafasi yake kuchukuliwa na Mrundi, Masoud Djuma.

YANGA UNBEATTEN MIAKA MITATU

Yanga imefikisha miaka mitatu bila ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa mwenyeji tangu mara ya mwisho kwa mabingwa hao kupoteza kwa bao 1-0, dhidi ya Azam FC lililofungwa na Mzimbabwe, Prince Dube, mechi iliyopigwa Aprili 25, 2021.

Kwa maana hiyo, tangu Yanga ipoteze mchezo huo na Azam FC imefikisha miaka mitatu, mwezi mmoja na siku nne ikiwa ni sawa na jumla ya siku 1,129 na kuanzia hapo imecheza michezo 47 ikiwa nyumbani na kati yake imeshinda 42 na kutoka sare mitano. Rekodi hizo ni baada ya mechi za mwisho za ligi.

Katika michezo hiyo 47 Yanga imefunga jumla ya mabao 110 na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara 18 huku ushindi mkubwa kwao ukiwa wa 5-0 dhidi ya Kagera Sugar Aprili 11, 2023, (5-0) v KMC (Agosti 23, 2023), (5-0) v JKT Tanzania (Agosti 29, 2023).

Ushindi mwingine mkubwa kwa Yanga ni wa mabao 5-0, dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Machi 3, mwaka huu.

Msimu huu fedha za zawadi kwa washindi kuanzia bingwa wa Ligi Kuu Bara hadi wa 16, zimeongezeka tofauti na misimu iliyopita na Yanga imejikusanyia kiasi cha Sh600 milioni. Msimu jana ilipata kitita cha Sh500 milioni.

Azam FC iliyomaliza ya pili msimu huu katika Ligi Kuu Bara imepata Sh300 milioni tofauti na msimu uliopita ambao timu iliyomaliza nafasi hiyo ilikuwa ikipata Sh250 milioni huku iliyokamata ya tatu ambayo ni Simba imepata Sh255 milioni.

Kwa msimu huu tumeshuhudia makipa wengi wakiwa ni wageni tofauti na misimu ya nyuma na wengi wao walikuwa ni wazawa tu.

Hali hii imechangiwa na ukuaji wa soka letu kwani hata timu za daraja la chini au kati zina uwezo wa kusajili makipa kutoka nje ya nchi.

Katika timu 16, nane zina makipa wa nje ambazo ni Yanga (Djigui Diarra – Mali), Simba (Ayoub Lakred- Morocco), Azam FC (Mohamed Mustafa-Sudan) huku wakiwa na wengine ambao ni majeruhi kikosini, Ali Ahmada wa Comoros na Abdullah Idrissu kutoka Ghana, Coastal Union (Ley Matampi-DRC).

Timu nyingine ni Namungo (Jonathan Nahimana-Burundi), Kagera Sugar (Alain Ngeleka-DRC), Tabora United (John Noble-Nigeria) na Mtibwa Sugar (Justin Ndikumana-Burundi).

Kwa upande wa timu zenye wazawa ni KMC (Wilbol Maseke), Ihefu (Aboubakar Khomeiny), Mashujaa (Erick Johora), Tanzania Prisons (Yona Amos), Singida FG (Benedict Haule), Dodoma Jiji (Aron Kalambo), JKT Tanzania (Yacoub Suleiman Ali) na Geita Gold (Samson Sebusebu).

Related Posts