Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria – Busweru, Samweli Lunzebe kwa tuhuma za kumbaka binti mwenye umri wa miaka 15. Anaripoti Calvin Nyorobi … (endelea)
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda unyama huo mbele ya mtoto mdogo mwenye umri wa miaka minne ambaye ni mdogo wake binti huyo.
Akizungumza na MwanaHALISI jana Alhamis, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema jeshi la polisi linamshikilia mchungaji huyo katika kituo cha Polisi Nyamagana mkoani Mwanza kwa mahojiano zaidi.
“Ni kweli jeshi linamshikilia na kumuhoji kuhusiana na hilo tukio hilo na uchunguzi unaendelea hivyo ukikamilika atafikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Mutafungwa
Aidha, Kamanda Mutafungwa amebainisha kuwa Mchungaji Samweli Lunzebe alikamatwa tarehe 27 Mei mwaka huu kwa tuhuma za kumuingilia kimwili binti huyo mwenye umri wa miaka 15 jambo ambalo linatafsirika kuwa ni ubakaji.
Aidha, akizungumzia tukio hilo ambalo taarifa zake zimesambazwa kwenye mitandao, Kamanda Mutafungwa amesema bado hajapata taarifa hizo.
Mwanahalisi ilipotaka kujua kuhusu Mchungaji Moses Lauwo anayedaiwa kusambaza mahojiano yake na binti huyo pamoja na taarifa za Hospitali Kamanda Mutafungwa alisema “Mimi sijaisikia hiyo sauti na kama unayo ningependa unirushie niifuatilie.
“Lakini niseme kama ipo, si maadili mema ya kumu-‘expose’ shahidi kiasi hicho kwa sababu shahidi baadaye anatakiwa kutoa ushahidi mahakamani katika utaratibu ulioruhusiwa kisheria kimahakama na utaratibu unaolinda faragha za watu”
Tukio hilo liliripotiwa baada ya kusambaa kwa sauti ya mahojiano baina ya Mchungaji Moses Lauwo na Binti huyo ambapo Mchungaji alitaka kujua ilikuwaje akafanyiwa kitendo hicho na Mchungaji Lezebe.
Sauti ya mahojiano ya Mchungaji Lauwo na binti huyo inaendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii ya makundi sogozi sambamba na ripoti ya daktari jambo ambalo pia linatafsiriwa kuwa ni udhalilishaji kwa mtoto huyo.
Akizungumza na binti huyo, Mchungaji Lauwo kupitia sauti hiyo alitaka kujua ni nini kilimtokea binti huyo mpaka akawa na uhusiano wa kimapenzi na Mchungaji Luzebe.
Binti huyo kupitia sauti hiyo alisema kuwa anamfahamu Mchungaji Luzebe kuwa ni baba wa rafiki yake (jina linahifadhiwa).
“Mimi nilifahamiana na mchungaji huyo siku nilipoenda nyumbani kwa rafiki yangu ambaye alinipa namba za simu ya baba yake ambayo huitumia kuwasiliana na marafiki zake. Sasa nilipoipata namba hiyo yeye ndio alianza kunipenda,”
Aliendelea kusimulia kwa kusema kuwa “Baada ya Lunzebe kupata namba yake siku moja nilimpigia ili niongee na rafiki yangu ndipo mchungaji huyo akaanza kunitumia meseji kwenye yangu ya kunitaka niende nyumbani kwake. Sikuenda akanipigia simu akauliza kwanini sikuenda nikamwambia nilibanwa na kazi.
“Simu yangu iliharibika nikamwambia, akaniambia niende atanipa simu,” anasema.
Anasema siku moja alimwambia wakutane eneo linaloitwa National huko mkoani Mwanza ili akamnunulie simu lakini alipoenda na kuonana naye Mchungaji huyo hakwenda kumnunulia simu na kudai amesahau kadi za benki kwenye begi hivyo watakwenda siku nyingine.
“Akaniambia twende huku tukawa tunaenda tu mimi sikujua kuwa tunaenda wapi… kwa sababu hakuniambia kuwa tunaenda nyumba ya wageni tukawa tunaenda tu… kumbe tunaenda guest. Nilikuwa na mdogo wangu, tukaingia mimi na mdogo wangu tukakaa kwenye stuli.
“Akanilazimisha niende kukaa kitandani, nikamuacha mdogo wangu amekaa kwenye stuli mara akaanza kunishikashika kisha akaniingilia kimwili huku mdogo wangu mwenye umri wa miaka minne akiwa amekaa pembeni,” anaeleza binti huyo.
Akizungumza na MwanaHALISI hivi karibuni, Mchungaji Lauwo alisema taarifa za binti huyo kuingiliwa kimwili na mchungaji Lunzebe alizipata kutoka kwa wazazi wa binti huyo.
Mchungaji Lauwo amefafanua kuwa hajasambaza mahojino hayo kwenye mitandao ya kijamii, bali baada ya kumhoji binti huyo ali’share’ na watu ambao wangeweza kumsaidia binti huyo kupata msaada wa kisheria.
Alisema alituma sauti ya mahojiano hayo kwa Mkuu wa Jimbo Kanisa la KKKT Mkoani Mwanza, Obadia Ruhalile ambaye Mchungaji huyo Lunzebe yupo chini yake.
Mchungaji Lauwo aliendelea kueleza kwamba aliamua kumripoti Mchungaji Lunzebe ili mamlaka zinazomsimamia zimchukulie hatua za kisheria.
MwanaHALISI Online lilizungumza na Mchungaji Obadia ambaye alithibitisha kutumiwa sauti hiyo.
“Yeye (Lauwo) alinitumia sauti hiyo lakini bahati mbaya pia alikuwa ameiweka kwenye Group la Wakristo… nikamwambia asiisambaze popote tena kwa sababu nilitaka niisikilize nijue nitachukua hatua gani kama kiongozi, hivyo sijaisambaza popote” alifafanua Mchungaji Obadia
Hata hivyo, alisema kwa kuwa group hilo la whatsap lenye watu wengi, inawezekana wao ndio waliosambaza sauti na ripoti hiyo ya daktari aliyemfanyia uchunguzi binti huyo.