TCAA yakabidhi vifaa kwa shule ya msingi Mnete-Mtwara

Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA imekabidhi vifaa vya shule na vya ofisi katika Shule ya Msingi Mnete iliyopo mkoani Mtwara ikiwa ni msaada kwa jamii.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo vyenye thamani ya Milioni Kumi (10) Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Mwanahamisi A. Munkunda ameishukuru TCAA kwa kuona hitaji na kuchukua hatua ya kuleta vifaa hivi ambavyo ni muhimu sana na vitachangia kwa kasi maendeleo ya elimu.

 

Vifaa hivyo ni pamoja na madawati 20 ya wanafunzi, meza na viti saba kwa ajili ya ofisi ya walimu pamoja na mashine ya kutoa kopi.

“Leo ni siku njema siyo tu kwa Shule ya Msingi Mnete bali kwa Wilaya ya Mtwara kwani vifaa hivi vitarahisisha utendaji kazi wa waalimu pamoja na kuwapunguzia mzigo wazazi” amesema Mhe. Mwanahamisi

Sambamba na hilo Mhe. Mwanahamisi ametoa wito kwa uongozi wa elimu kuanzia ngazi ya Kata hadi shuleni kuvitumia vifaa hivi kwa weledi na kuvitunza ili vidumu na kuendelea kuhudumia sekta hiyo muhimu.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TCAA Bw. Yessaya Mwakifulefule amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutenga muda wake na kuja kushiriki tukio hili na kuahidi kuwa Mamlaka itaendelea kuchangia katika maendeleo ya elimu kwani ni eneo ambalo umuhimu wake ni mtambuka kwa taifa letu.

 

TCAA imeendelea kuwa mdau mkubwa wa elimu kwa kutoa msaada wa namna hiyo ambapo imeshatoa msaada wa shilingi milioni 8.8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya Msingi Rada iliyopo mkoani Songwe, vitanda 26 kwa shule ya sekondari ya Azania, ilitoa pia shilingi Milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo kwa shule ya Msingi Mzambarauni ya jijini Dar es Salaam.

Related Posts