Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamshikilia mwanamke mmoja na mtu mwingine anayedaiwa ni hawala yake kwa tuhuma za mauaji ya mme wa mwanamke huyo kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Watuhumiwa hao ambao majina yao hayajatajwa wanadaiwa kumuua Victor Mwakapenda (41), mkazi wa mtaa wa Ilembo, Mbozi mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustino Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.
Kamanda Senga amesema marehemu alitoweka nyumbani tangu Aprili 30 mwaka huu akiwa na mke wake na mwili wake kuokotwa Mei 9, mwaka huu katika msitu wa Mpoloto uliopo Kijiji cha Igale Mbeya Vijijini.
Amesema baada ya kuukuta, mwili huo ulipelekwa kwenye Hospitali ya Ifisi jijini Mbeya na kuhifadhiwa mpaka ndugu zake walipoutambua na kukabidhiwa Mei 29 mwaka huu.
Kamanda Senga amesema mpaka sasa wanawashikilia watu wawili wanaosadikiwa kuhusika na tukio hilo, akiwepo mke wa marehemu na dereva mmoja wa pikipiki, lakini hakuwataja akisema bado wapo kwenye uchunguzi.
“Ni kweli tunawashikilia watu wawili ambao inadaiwa walikuwa na uhusiano na siku ambayo marehemu alitoweka nyumbani, dereva huyo bodaboda ndiye aliyembeba na mke wake akiwepo, hivyo uchunguzi unaendelea,” amesema Kamanda Senga.
Akizungumza na Mwananchi, mjumbe wa Shina namba moja mtaani hapo, Aliki Songa amesema “sisi tunasikitika kwa mauaji ya mwenzetu na kifo chake kinahusishwa na wivu wa mapenzi kati ya marehemu na mke wake”.
“Tunashukuru Jeshi la Polisi kuwashikilia watu hawa, kwani sisi kama wananchi hatujawahi kushuhudia tukio la namna kama hili, hivyo kama unaona umechoka kukaa na mwenzako bora uachane naye kuliko kusababisha kifo, ni mbaya sana,” amesema Songa.
Akizungumza msibani hapo, kaka wa marehemu aliyejitambulisha kama Mwakapenda amesema kifo cha mdogo wake hakivumiliki na kama walikuwa na ugomvi wangemfikisha kwenye vyombo vya sheria kuliko kumuua kinyama.