Unachopaswa kukijua kuhusu mzio

LEO nitafafanua tatizo la mzio ambalo wengi hulifahamu kwa jina la ‘aleji’ (allergy). Hili tatizo husumbua sana baadhi ya watu. Mzio au magonjwa ya mzio, ni hali mbalimbali zinazosababishwa na mnyumbuliko usio na kifani wakati seli za mwili wako unapokataa kitu ambacho kwa mtu wa kawiada hakina madhara.

Mzio hujitokeza kwa alama /dalili mbalimbali na huleta matokeo yenye ishara nyingi mwilini. Dalili zinaweza kujumuisha macho kuwa mekundu, upele unaowasha, kupiga chafya, kukohoa, mafua, upungufu wa kupumua, au uvimbe.

Aina kuu za mizio

*Aina ya kwanza ni ile inayosababishwa na kitu ambacho kiko nje ya mwili wako na husababishwa na mazingira ya nje ya mwili wako.

*Aina nyingine ni ile ambayo iko ndani ya mwili wako ambayo inaweza kuletwa na kinasaba (genetic) cha kurithi au na kitu kilichoko ndani ya mwili wako.

Vitu vinavyosababisha mzio kwa watu wenye mzio huitwa alejeni (allergen) au alejeni pingamizi. Wakati kitu chochote kinaweza kuwa alejeni lakini kuna vitu vingine vinakuwa alejeni zaidi kupita kiwango cha kawaida.

Alejeni zinaweza kuwa vumbi na mazingira yaliyochafuliwa kwa poleni (unga wa mimea na maua), vipodozi na marashi ya kujipaka au ya kupuliza, vyakula mbalimbali kama mayai, njugu/ karanga, kemikali zitumikazo kuhifadhia vyakula na vinywaji ambazo mtu huzila kwenye chakula au huzinywa wakati akinywa vinywaji hivyo.

Mzio unaweza kusababishwa na mabaki machafu ya kemikali kutoka viwandani, moshi wa magari machakavu na makukuu utokao kwenye eksozi, mwanga wa jua, nyuzi za nguo zinazotengenezwa viwandani, baadhi ya dawa kama penicillin na kadhalika, viuatilifu, manyoa/ sufu ya ngozi za wanyama, wadudu mbalimbali kama mchwa na mende, manyoa ya paka na mbwa na harufu itokanayo na rangi mbali mbali.

Dalili nyingi za mzio za awali hujitokeza kama maambukizi/ mchochota wa aina fulani na au kama uvimbe bila maumivu na wakati mwingine huambatana na maumivu. Sehemu iliyoathirika huwa nyekundu na wakati mwingine panakuwa na muwasho wa aina fulani na homa huenda ikawepo.

Kupiga chafya na kuwepo kwa harara/ vipele vidogo dogo kwenye ngozi ni kitu ambacho huonekana zaidi kwa watu wanaougua pumu (asthma). Kuwa na sehemu kwenye mwili ambayo ni nyekundu na imevia pia inaweza kuwa dalili ya mzio.

Magonjwa ya kawaida ambayo huambatana na mzio yanaonekana zaidi katika maeneo manne katika mfumo wa mwili wa binadamu.

*Mfumo wa njia ya hewa hususan mafua, mafindofindo, pumu na mzio wa poleni.

*Mfumo wa njia ya chakula magonjwa ni madonda mdomoni, vidonda vya tumbo, hewa kujaa tumboni, kuharisha, msokoto na maumivu ya tumbo.

*Mfumo wa misuli na mifupa magonjwa ya mzio hujitokeza kwenye magoti, vifundo, viungio na jointi, maumivu makali kwenye misuli, viungio na vifupa vya uti wa mgongo hudhoofika na kuwa vyepesi.

*Kwenye  ngozi, mwenye mzio anaweza kuwa na ngozi yenye mabaka mabaka na ukakasi, nywele zikanyofoka akawa na hali kama ya mba au mapunye kichwani mwake, akajikuna na akapata chunusi na vipele vyenye usaha na kule kwenye sehemu za siri kwa babu na bibi kukawa na muasho na ngozi kuwa ngumu.

Hakuna tiba

Wasomaji wa makala hii nigependa muelewe kwa kinaga ubaga kuwa hakuna tiba ya kudumu na iliyo maalum kwa mzio. Tatizo la mzio ukishalipata ujue kuwa una ugonjwa  sugu. Kwa wakati mwingine kwa watoto wenye mzio unaosababishwa na alejeni maalum, jinsi wanavyokuwa kwa umri, wengine wanapata nafuu na uwezekano upo wakapona mzio wao, ukatoweka kabisa katika miili yao.

Mzio ni hali ya mwili kuchukia kitu ambacho hakina madhara. Poleni (unga wa maua) vumbi la fangasi, vumbi la nyumbani, mayai, maziwa ya ng’ombe, samaki, ngano, vumbi la nickel, chrome, na penisilin vitu hivi havina madhara kwa watu wote, isipokuwa kwa wale tu wenye mzio wa vitu hivyo.

Unga wa poleni kutoka kwenye mauwa na mimea na vumbi la nyumbani vina uwezekano wa kumfanya mgonjwa apige sana chafya na kupata pumu (asthma). Vyakula kama mayai, maziwa ya ng’ombe, samaki, ngano vinaweza kuleta vipele vidogodogo na msokoto wa tumbo na kuharisha.

Vumbi la nickel na chromium linaweza kuleta shida kwenye ngozi na dawa ya penicillin inaweza kuleta mzio, mshtuko ambao unaweza kusababisha mgonjwa kupoteza fahamu endapo ana mzio wa dawa hiyo.

Kitu kinachosababisha mzio katika mwili wa binadamu huitwa allergen au antigen. Kile kinachozalishwa na mchakato huo wa mzio huitwa kinga mwili pingamizi (antibody). Wakati antigen na antibody vinapokutana mwilini na kusababisha muungano huo, hatua hiyo ya mgongano wa antigen na antibody ndio unaozalisha mzio.

Katika hali hiyo ya mkusanyiko huo uletao mzio kuna kitu kinachozalishwa huitwa ‘histamine’ na kingine kinachozalishwa huitwa ‘serotonin’ na kemikali nyingine pia hutengenezwa. Vitu hivyo vyenye matokeo hayo maalum huleta dalili zote za mzio kama vile kukakamaa na kutetemeka kwa misuli kama mtu mwenye dalili za degedege hafifu, hapa ndipo mtu mwenye pumu zinaanza kujitokeza kwa kuwa atashindwa kutoa hewa kwenda nje ya mapafu yake.

Kwa wale wenye mafua ya mara kwa mara njia zao za  pua na hewa  zinaingiliwa na kamasi na mafua hususan wakati wa kipindi cha hali ya ubaridi. Mtu anayekuwa na hali ya mzio anapata ngozi nyekundu na pia anaweza kupata harara itakayowasha.

Dawa kama piriton, cetrizine, phenergan na hydrocortisone ndizo zinazotumika endapo mgonjwa ataonesha dalili za mzio unaosababishwa na histamine ambayo hujitokeza wakati wa mzio.

Pamoja na kuandika kuhusu dawa hizo, ninasisitiza muone daktari wako akuandikie kile unachostahili kupata na sio kujinunulia dawa kiholela. Mzio mkubwa na waghafla ni hatari katika maisha ya binadamu na unapotokea unaweza kuleta hali ya taharuki na mgonjwa akashindwa kupumua.

Inapofikia hatua kama hiyo msaada wa dharura katika tiba inabidi upatikane haraka iwezekanavyo. Hali kama hiyo inaweza kutokea kwa mgonjwa aliye na mzio wa dawa ya penicillin, mwenye mzio wa dawa ya Aspirin na kuna mzio kwenye baadhi ya vyakula ingawaje sio kitu cha kawaida.

Ingawaje ugonjwa wa mzio unaweza kurithiwa kwenye familia, lakini kinachorithiwa ni mzio na sio aina fulani ya mzio. Mfano hai mzazi anaweza kuwa na pumu, na mwanaye mmoja anaweza kuwa na eczema (aina ya ugonjwa wa ngozi unaosababishwa na mzio) na mwanaye mwingine akawa anapiga chafya mara kwa mara wakati anapokua, na huenda baadaye akaugua pumu ukubwani.

Katika tiba endelevu, cha msingi ni kuacha na kuepuka kile kinachokudhuru katika mchakato wa kupata mzio. Kuacha kula au kugusa kile kinachokudhuru. Utakapoimarisha kinga yako kwa lishe kamili na kufanya mazoezi ya mwili na viungo na kupima afya kabla hujaugua, hapo utakuwa mjasiria afya kwa utashi wako na sio kubahatisha.

*Dk. Ali Mzige ni mtaalamu wa afya ya jamii na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005. Sasa ni mkurugenzi wa Mshangai Polyclinic Korogwe. amzigetz@yahoo.com. 0754495998.

Related Posts