SIKU chache tangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litangaze tuzo za soka kwa msimu wa 2023-2024 zitatolewa wakati ya Ngao ya Jamii ya uzinduzi wa msimu wa 2024-2025, wadau wameibuka wakionekana kuwaganyika juu ya uamuzi huo.
Taarifa ya TFF kuhusu tuzo hizo kusogezwa mbele ilieleza sababu kubwa ni kuziboresha zaidi tofauti na misimu iliyopita japo kanuni ya 11:11 ya Ligi Kuu Bara inayohusu vikombe na tuzo inataka zifanyike siku tatu baada ya fainali ya FA.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alisema wakati msimu mpya unapoanza kila kitu kinatakiwa kujulikana mapema, hivyo jambo kubwa analoliona kwake ni kukosekana kwa mgawanyo wa majukumu kwa wahusika.
“Kila msimu lazima uishe na mambo yake, kuna uwezekano kukawa na vitu vitakavyoathiri tuzo hizo kwa sababu ikitokea kwa mfano Stephane Aziz Ki akawa mchezaji bora ila akasajiliwa Simba, wanatakiwa kuangalia mambo ya namna hiyo mbeleni,” alisema.
Angetile aliongeza kuwa Bodi ya Ligi inatakiwa iwe huru kwani itasaidia kuondoa mkanganyiko wa mambo ya namna hiyo na kama haitoshi mchezaji anapoondoka katika timu husika na akashinda tuzo haitakuwa na mvuto zaidi tofauti na alivyokuwepo.
Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema kutokana na TFF kueleza sababu za kusogeza mbele tuzo hizo ni kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho, hana shida na hilo kwani lengo ni mabadiliko makubwa na ya kisasa.
“Ninaposikia jambo linafanyiwa maboresho huwa sina wasiwasi kabisa kwa sababu nategemea kuona vitu vya tofauti zaidi na nilivyoona mwanzoni, kwangu nasubiri kuona kitakachotokea hivyo ukiniuliza sioni mantiki ya kuwapinga,” alisema.
Mmoja wa wachezaji anayecheza Ligi Kuu Bara ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini alisema sio sawa kwa tuzo hizo kusogezwa mbele kwa kuwa zitakosa mvuto kutokana na wachezaji wengi wanaweza kuondoka timu walizokuwa wanazi-chezea.
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda alikaririwa akisema tuzo zilizoahirishwa sio zao kwa vile hata kanuni zinazokaririwa na wadau zinahusiana na ligi wakati tuzo za TFF zinagusa hadi Ligi Kuu ya Wanawake, Championship na Kombe la Shirikisho (FA) linalomalizika wikiendi hii.
Rais wa TFF, Wallace Karia pia akihojiwa na kituo kimoja cha redio alikiri hizo ni tuzo za TFF na kilichofanywa ni kutaka ziwe bora, hivyo kutaka wadau kutulia.
Tuzo za msimu uliopita zilitolewa jijini Tanga wakati wa Fainali ya Kombe la FA, Yanga ilipata 12 zikiwemo za kikosi bo-ra, aliyekuwa nyota wake Fiston Mayele alichukua ya mfungaji bora, bao bora la msimu, mchezaji bora wa jumla yaani MVP.
Kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra alishinda tuzo mbili za kipa bora wa FA na Ligi Kuu ilhali Dickson Job akipata ya beki bora wakati Bakari Mwamnyeto akiwa mchezaji bora wa FA na wote waliingia katika kikosi bora. Nasreddine Nabi alikuwa kocha bora huku Clement Mzize akishinda mchezaji bora kijana.
Simba ilishika nafasi ya pili tuzo nyingi ikiongozwa na Saido Ntibazonkiza aliyebeba tatu – mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17, mchezo wa kiuungwana na kiungo bora huku akiingia kwenye kikosi bora. Wengine ni Henock Inonga, Mohammed Hussein, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Clatous Chama.
Tuzo ya mchezaji bora chipukizi ilienda kwa Lameck Lawi wa Coastal Union huku mchezaji bora wa Championship akiwa wa JKT Tanzania, Edward Songo wakati kamishina bora wa Ligi Kuu akiwa Isack Munisi.
Tuzo ya mwamuzi bora wa Ligi ya Wanawake (WPL) ilienda kwa Ester Adalbert, wakati mwamuzi msaidizi ni Glory Tesha.
Mwamuzi bora wa Ligi Kuu Bara alikuwa Jonesia Rukyaa huku msaidizi ikienda kwa Frank Komba.
Tuzo ya seti bora ya waamuzi ilikwenda kwa Jonesia Rukyaa, Zawadi Yusuph, Athuman Rajabu na Ally Simba katika mechi ya Geita Gold na Dodoma Jiji.
Mfungaji Bora wa WPL ni Jentrix Shikangwa (Simba Queens) mabao 17.
Kocha wa JKT Queens, Ally Ally alishinda tuzo ya kocha bora wa WPL huku mchezaji bora akiwa ni Donisia Minja. Chipuki-zi bora wa WPL ilienda kwa Winfrida Charles wa Alliance Girls huku kipa bora alikuwa ni Najat Abbas wa JKT Queens.