Kiongozi wa kuandaa Katiba mpya CCM hajazaliwa

HABARI kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipo tayari kukaa meza moja ya mazungumzo na vyama mbalimbali kwa lengo la kufanya mjadala wa Katiba pamoja na maridhiano ni mgeni pekee wa siasa za Tanzania masikio yake yanaweza kusisimkwa na kuamini, maana kiongozi wa kuandaa Katiba Mpya kutoka chama hicho hajazaliwa. Anaandika Bupe Mwakiteleko … (endelea).

Wamewachezea wapinzani na wanaharakati kiasi cha kutosha; wametudanganya tusio wanachama wa vyama vya siasa kiasi cha kutosha, wamewachelewesha Watanzania kiasi cha kutosha na wamejipotezea uaminifu kiasi cha kutosha.

Wanatumia kauli kwamba “Ukiona unasifiwa na mpinzani wako, jiulize umekosea wapi?” Hawataki kusifiwa bali kufurahia wapinzani wanapolia, wanapolalamika, wanapokimbia nchi kuokoa uhai wao, wanapolilia marekebisho ya sheria na Katiba mpya. Miaka yote wameahidi Katiba mpya kuzuga halafu wanasingizia uchumi hauruhusu, mara hatukuwahi kuahidi wakati wa kampeni, mara ratiba imebana.

Safari hii aliyetoa ahadi ya kufanya majadala wa Katiba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’ katika mkutano wa Demokrasia Tanzania kwa mwaka 2024 uliofanyika wiki iliyopita katika hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar, ambapo amesema vyama hivyo viondoe hofu na kutoaminiana.

Dk. Dimwa akionekana kuwa mwangalifu wa maneno anayotumia anasema: “Hii ni nchi yetu sote, ni lazima tuwe na maridhiano ya pamoja. Tuaminiane tufikie kwenye Katiba mpya itakayojali masilahi yetu. Sisi vyama vya siasa tukiridhiana ndiyo tukabadilishe kwa kuwa wananchi wanatusikiliza.”

“Tutajenga vipi Taifa letu kama kila mmoja atakuwa na hofu? Kama hatukai pamoja hatutaweza kupiga hatua na kufikia maridhiano tunayotarajia. CCM tuko tayari kusaka Katiba mpya kwa masilahi ya Taifa letu, tunaviomba vyama vya siasa vije mezani tuzungumze na tufikie malengo tuliyokusudia.”

Rais mstaafu Jakaya kikwete na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Mohamed Ali Shein wakiwa wameinua juu Katiba inayopendekezwa katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini Dodoma tarehe 8 Oktoba 08, 2014. Kulia ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Samuel Sitta akifuatiwa na Makamu wake Samia Suluhu Hassan.

Kama mtenda dhambi aliyeokoka, Dk. Dimwa amesema kuwa Katiba ni ya wote si ya vyama vya siasa hivyo ni vema wadau wote wakashirikishwa kikamilifu kupitia majukwaa mbalimbali.

“CCM tunaviomba vyama vya siasa virejee kwenye mazungumzo, visiende nje kueleza kile tunachojadiliana kabla ya kufikia makubaliano maana tutavuruga amani, utulivu na umoja wetu” amesema.

“CCM iko tayari baada ya uchaguzi tuendelee na mchakato wa Katiba, wapinzani waondoe hofu katika jambo hili, tukae meza moja tukubaliane ya namna ya kuijenga nchi yetu,” amesema.

Hebu tumuulize Dk. Dimwa, wakati rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi akikataa kuandikwa kwa Katiba mpya badala yake aliridhia viwekwe viraka maeneo wanayotaka, alikuwepo nchini au alikuwa ughaibuni?

Mwaka ule rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akiunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba alikuwepo nchini au alikuwa ughaibuni? Wakati Bunge Maalum la Katiba (BMK) linaundwa na linajadili rasimu ya Jaji Warioba alikuwepo nchini au alikuwa ughaibuni?

Pia, wajumbe wa BMK kutoka Zanzibar walipogeuza ukumbi kuwa uwanja wa matusi ya nguoni yeye alikuwepo? Kwa hiyo alitaka wajumbe wenye akili zao timamu wabaki katika Bunge lile la hovyo?

Aidha, wakati uongozi wa BMK chini ya mwenyekiti wake Samweli Sitta na makamu wake Samia Suluhu Hassan wanakabidhi Katiba inayopendekezwa, iliyotokana na mjadala wa hovyo, kwa Kikwete na Dk. Mohamed Shein alikuwepo nchini au alikuwa ughaibuni?

Dk. Dimwa anaendeleza msimamo wa CCM wa kutembea na porojo “talk the talk” bila kuonesha dhamira kwa matendo ya “walk the walk”. CCM wanataka porojo siyo kupiga mwendo kuhusu Katiba mpya.

Dk.Dimwa anasema Katiba mpya na maridhiano yatapatikana kama vyama vya upinzani vitakuwa na dhamira njema kufanikisha mambo hayo. Halafu akarudia ngonjera zilezile za kuwatupia lawama wapinzani kwa makosa waliyofanya CCM mwaka 2014.

Dk. Dimwa anasema, “Walipokimbia kwenye Bunge walitupa majina mabaya ambayo mpaka sasa yanatuumiza, hili la Katiba wenzetu hawakuwa na nia njema ya kuendelea nalo. Haya mabadiliko tunayoyataka muda ni mdogo wa kwenda kubadilisha Katiba, tukipita baada ya uchaguzi wa 2025 tutabadilisha Katiba na sheria ili tuipate iliyo bora zaidi”.

Ni kweli wapinzani walisusia, lakini iko wapi Katiba waliyoiandaa CCM wenyewe? Wakati wapinzani wanatoka nje ya BMK, CCM hawakujua kwamba ule ulikuwa mshkeli mkubwa? Ni lini walipata akili kwamba Katiba inayopendekezwa waliyoiandaa kwa mbwembwe haikuwa inaakisi maoni ya walio wengi? Na ikiwa wamelijua hilo, kwa nini hawakuwaomba radhi Watanzania?

Habari kwamba CCM wako tayari kukaa meza moja ya mazungumzo na vyama mbalimbali kwa lengo la kufanya mjadala wa Katiba na maridhiano ni mwendawazimu pekee masikio yake yanaweza kusisimkwa na kuamini.

Kiongozi huyo pia amesema kuwa Katiba nzuri si suluhisho la matatizo waliyonayo wananchi bali kinachofanywa na chama chake ni kuwapelekea wananchi maendeleo ndipo yaje mengine.

Maneno hayo ya Dk. Dimwa yanaibua mkanganyiko maana wakati mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan anasema “Wananchi wanadai Katiba yao” Dk. Dimwa ameshikilia msimamo wa enzi za John Magufuli akisema, “Katiba si kipaumbele cha wananchi, kule Makunduchi, Konde na kwingineko wanachohitaji ni maendeleo. Hili la Katiba CCM ndiyo kinara wa mageuzi na kila mara imekuwa mstari wa mbele.”

Rais Samia alitoa kauli inayovutia masikioni huku akielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kufanyia kazi suala hilo. Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam tarehe 4 Aprili mwaka huu katika hotuba yake baada ya kuapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Rais Samia Suluhu Hassan

Akitoa maelekezo mahsusi kwa Naibu Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, Rais Samia alisema, “Wewe (Sagini) ni mzoefu serikalini. Nenda kasaidie katika Katiba na sheria. Kipindi hiki tulichonacho watu wanadai Katiba yao, nenda kasaidiane na waziri, nina imani utafanya vizuri.”

Mnamo Juni 22, 2022, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alitangaza chama hicho kimekubali kufufua mchakato wa Katiba Mpya, wakiwa na angalizo kwamba uzingatie maslahi ya taifa.

“CCM tunasisitiza umuhimu wa kuwapo Katiba, mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kwa maslahi mapana ya taifa na maendeleo kwa ujumla,” alisema Shaka ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Wakati wa mkutano wa mwaka jana wa Bunge la Bajeti, serikali ilitangaza kuongeza takriban Sh. bilioni tisa katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2023/24, ili kukwamua mchakato wa Katiba mpya uliokwama Aprili 2, 2015, kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30, mwaka huo.

Related Posts