ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ameonyesha kushtushwa na kiwango bora cha kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki alichokionyesha msimu huu na kuifikia rekodi yake ya mabao 21 aliyoiweka misimu minane iliyopita.
Tambwe aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiichezea Yanga msimu wa 2015/2016 alipofunga mabao 21 na rekodi hiyo imedumu kwa misimu minane ndani ya kikosi hicho hadi msimu huu ilipofikiwa na kiungo nyota, Stephane Aziz Ki.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe alisema kwanza anampongeza nyota huyo huku akishangaa kuona kiungo akifunga idadi kubwa ya mabao.
“Kwangu nampongeza sana kwa sababu sio rahisi tena kwa mchezaji anayecheza nafasi ya kiungo uwanjani. Anastahili heshima kubwa kwa sababu wapo washambuliaji wengi wakubwa na wakali walipita Yanga ila walishindwa hata kuisogelea,” alisema.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea Simba ambayo pia aliwahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014 baada ya kufunga mabao 19, aliweka wazi Aziz Ki kwake ndiye mchezaji bora wa msimu kutokana na mchango mkubwa aliouonyesha.
“Sina shaka kama atachaguliwa mchezaji bora wa msimu (MVP), kwa sababu mabao mengi aliyofunga yameisaidia Yanga kufikia malengo iliyojiwekea, nawapongeza wote walioonyesha kiwango kizuri msimu huu ila Aziz Ki kwangu ndiye amenikosha zaidi.”
Mbali na Tambwe kuzichezea Yanga, Simba ila timu nyingine aliyoichezea hapa nchini ni Singida Fountain Gate aliyoondoka mwaka 2022.
Aziz Ki anayeichezea Yanga kwa msimu wake wa pili hapa nchini tangu alipojiunga nayo 2022 akitokea klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coastal, amekuwa na kiwango bora ambapo ameiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo.
Nyota huyo raia wa Burkina Faso katika msimu uliopita alifunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara, huku akiiwezesha timu yake kutetea ubingw, lakini pia ameifikisha fainali ya Kombe la FA itakapopambana na Azam FC Juni 2, mwaka huu visiwani Zanzibar.