Hayo yamesemwa leo (31/05/2024) jijini Arusha wakati wa kuhitimishwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), baada ya kufanya ukaguzi katika baadhi ya viwanda, wauzaji wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea baadhi ya wafugaji wanaotumia vyakula hivyo.
Akiongoza timu ya ukaguzi, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka TVLA Dkt. Zacharia Makondo amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani na wale ambao wanapuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama.
Dkt. Makondo ameongeza katika utekelezaji wa zoezi hilo, wale wote ambao hawajasajiliwa watawafungia na hawataruhusiwa kufanya shughuli hiyo, huku akibainisha kuwa maabara za kanda zitawezeshwa kuwa na vifaa vya kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa wa kufanywa kwa ukaguzi wa rasilimali za vyakula na vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa salama.
Aidha, amesema baada ya kufanya zoezi hilo kwa ufanisi katika Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini, zoezi hilo litafanywa kwenye kanda zingine kwa ajili ya kuendelea kukagua pamoja na kufanya uchambuzi wa vyakula na rasilimali za vyakula vya mifugo.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mifugo, Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Sallema, amesema wizara inawakumbusha wakaguzi kufanya ukaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha wadau wanafuata sheria.
Bi. Sallema amebainisha kuwa wale ambao wanafunga vyakula vya mifugo au madini katika vifungashio vidogo wahakikishe vinakuwa na lebo na maelezo ambayo yanaendana na mfuko wa awali ambao wameufungua kwani kwa kutofanya hivyo ni kinyume cha sheria na kuashiria udanganyifu.
Pia, amesema wizara inaendelea kuwashukuru wadau kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa na kwamba changamoto zilizobainishwa zitawasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Naye Meneja wa TVLA Kanda ya Kaskazini – Kituo cha Arusha, Dkt. Rowenya Mushi amesema kanda hiyo ambayo inahudumia mikoa mitatu ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro imepata chachu ya kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula vya mifugo juu ya kupima vyakula vyao kuwa na ubora na kuleta matunda kwa wafugaji.
“Chakula bora huwa kinaleta mazao bora kwa wafugaji na hilo ndio lengo kuu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na serikali kwa ujumla, kuhakikisha mfugaji anafuga kisasa na kupata chakula bora kwa ajili ya mifugo yao hatimaye kupata mazao bora na kupata kipato kizuri zaidi na kukuza uchumi.” Alisema Dkt. Mushi
Sambamba na hilo amewasihi wazalishaji wa vyakula vya mifugo kufikisha sampuli ya vyakula vyao katika maabara ya TVLA katika kila toleo kuhakikiwa ubora na kupatiwa elimu na ushauri juu ya vyakula hivyo ili kuleta tija kwa wafugaji wanaotegemea vyakula hivyo.
Baadhi ya wadau wa kuzalisha na kusambaza vyakula vya mifugo pamoja na wafugaji wanaotumia vyakula hivyo, wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kufanya ukaguzi na kuwafafanulia mambo kadhaa yanayohusu vyakula hivyo ili kuimarisha ubora pamoja na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Wameiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutenga muda zaidi wa kufanya ukaguzi zaidi ili kuviondoa sokoni baadhi ya viwanda ambavyo vinazalisha vyakula hivyo katika ubora wa chini na kuwauzia kwa bei ndogo wafugaji wakidhani wamepata unafuu wa bei na kuwasababishia wafugaji kutopata matokeo mazuri ya mazao ya mifugo hiyo.
TVLA inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.