Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema uchafuzi wa mazingira katika miji, majiji halmashauri bado changamoto, akiwataka viongozi wa maeneo kuongeza nguvu katika usimamizi wa kukabiliana na suala hilo.
Mbali na hilo, Dk Mpango uharibifu wa misitu bado changamoto licha ya kuwepo kwa vyombo vya kuishauri Serikali kuhusu masuala ya utunzaji wa rasilimali hiyo, ukiwemo Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Makamu huyo wa Rais amesema hayo leo Ijumaa Mei 31, 2024 wakati akifungua kongamano la wadau wa mazingira lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), likiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka.
“Tuna vyombo vingine kama NEMC na Tafori (Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania) lakini pamoja na kuwepo kwa sheria ndogo za serikali za mitaa, inasikitisha sana kuona katika miji yetu mingi taka zimejaa kila kona.
“Waziri na katibu mkuu wanaosimamia sera, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na majiji wanayaona haya, lakini hatua hazichukuliwi. Ukiwauliza NEMC wanasema hawana meno kisheria,” amesema.
Dk Mpango amesema wamepiga kelele za kutosha kuhusu usimamizi, utunzaji na usafi wa mazingira, akisema kama sheria ndio kikwazo, ameagiza zitizamwe ili kuipa meno NEMC na halmashauri kuwa nguvu na kuwawajibisha.
“NEMC na taasisi zingine husika, nendeni mkaangalie sheria zenu nipate mrejesho ili nijue kikwazo ni nini, lakini niwasihi Watanzania tuache mazoea ya kukata miti na kutupa taka ovyo, si ustaharabu wa kufanya kila mahali kuwa jalala la taka,” amesema Dk Mpango.
Amewataka Watanzania kujenga ustaharabu wa kuweka mazingira safi na ya kijani huku akizikumbusha mamlaka ya serikali za mitaa kuhakikisha kampuni zinazopewa zabuni za kuzoa taka zinakuwa na uwezo kufanya shughuli hiyo kwa ufanisi.
“Zipo baadhi ya kampuni zinashindwa kutekeleza majukumu waliyopewa kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha, viongozi wa mikoa na halmashauri chambueni nani mnayempa kazi ya kuzoa taka,” amesema Dk Mpango.
Dk Mpango amesema siku ya mazingira mwaka 2024 inajielekeza kwenye “Urejeshaji wa ubora wa ardhi, kukabiliana na hali ya jangwa na ustahimilivu dhidi ya ukame” kaulimbiu ambayo inaitaka Tanzania kuchukua hatua madhubuti zitakazosaidia kuhimili ukame.
Awali akimkaribisha Dk Mpango, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo amesema kongamano hilo la sita limekuwa na mwonekano tofauti na mengine yaliyopita miaka ya nyuma.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi amesema kongamano hilo linajadili masuala ya mazingira na litatoka na mikakati ya pamoja ya kuzitambua na kuzishughulikia changamoto kubwa zilizopo za mazingira na kuzigeuza kuwa fursa.
“Tanzania na dunia kwa ujumla zinakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, upotevu wa baionuai, uchafuzi wa mazingira na upungufu wa maliasili, jambo linaloathiri maisha yetu ya kiafya, makuzi, kiuchumi na mahusiano.
“Kuelekea siku ya mazingira dunia NEMC imeona ni muhimu kwa wadau kupata taswira nzima ya hali ya mazingira duniani na hapa nchini ili kuwa na uelewa kuhusu umuhimu wa siku ya mazingira duniani,” amesema Dk Semesi.
Dk Semesi amesema mazingira ni sekta mtambuka inayohitaji nguvu ya pamoja katika usimamizi wake na NEMC ina jukumu la kuyalinda na kuyahifadhi kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.