Ngorongoro Kreta, Arusha.
TAASISI ya Caribbean Naples Zoo kutoka Nchini Marekani imetoa msaada wa gari mbili kwa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi wa faru na Wanyama wengine katika hifadhi hiyo.
Mkurugenzi wa Caribbean Naples Zoo Bw. Tim Tetzlaff amesema taasisi yao ni wadau wa shughuli za uhifadhi ambapo baada ya kutembelea Tanzania miaka ya nyuma kwa shughuli za Utalii walifurahishwa na juhudi za uhifadhi wa wanyamapori hasa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa gari mbili.
“Sisi ni wadau wakubwa wa shughuli za uhifadhi na kwa mara ya kwanza tulikuja Tanzania kwa shughuli za utalii, taasisi yetu ikafurahishwa na uhifadhi hasa wa faru na Wanyama wengine katika hifadhi ya Ngorongoro, hivyo kutoa gari hizi mbili kunalenga kuunga mkono juhudi za Serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika uhifadhi endelevu” ameseba Bw. Tetzlaff.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye ameishukuru taasisi hiyo na kuahidi kuwa NCAA kupata magari mawili kutoka taasisi hiyo imeongeza nyenzo kwa askari wa uhifadhi katika ulinzi wa Faru na Wanyama wengine na kusaidia kuongeza uhifadhi na utalii katika Kreta ya Ngorongoro.
“Hifadhi ya Ngorongoro ndio eneo pekee lenye Wanyama adimu kama faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili, tumeendelea kuwalinda, kuwatunza na kuwahifadhi ambapo idadi yao inaendelea kuongezeka, kupata magari mawili kwa wadau wa Caribbean Naples Zoo kumeongeza nguvu kwa askari wetu kupata vitendea kazi muhimu katika shughuli za ulinzi wa kila siku” ameongeza Dkt. Doriye.